Kinda Argentina afariki dunia
Muktasari:
- Nunez alikuwa akiichezea timu ya FC Ezeiza dhidi ya Deportivo Muniz katika mchezo wa ligi ya vijana, ambapo mpira uliokuwa ukiondolewa kwa nguvu na beki wa timu pinzani ulimpiga kichwani akiwa karibu naye na kumfanya aanguke chini.
Mchezaji chipukizi wa soka nchini Argentina, Abel Nunez, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 18 baada ya kupata jeraha kubwa kichwani kufuatia kupigwa na mpira uliopigwa kwa nguvu wakati wa mechi.
Nunez alikuwa akiichezea timu ya FC Ezeiza dhidi ya Deportivo Muniz katika mchezo wa ligi ya vijana, ambapo mpira uliokuwa ukiondolewa kwa nguvu na beki wa timu pinzani ulimpiga kichwani akiwa karibu naye na kumfanya aanguke chini.
Alikimbizwa hospitalini kwa matibabu, ambapo madaktari walibaini kuwa alikuwa amevunjika fuvu la kichwa na damu kuvuja ndani ya kichwa. Alifanyiwa upasuaji wa dharura, lakini baadaye alifariki dunia kutokana na majeraha hayo.
Mchezo huo ulisimamishwa mara moja kufuatia tukio hilo.
Uongozi wa FC Ezeiza ulithibitisha kifo chake, ukieleza kuwa wamepata pigo kubwa na kutoa pole kwa familia, marafiki, wachezaji wenzake pamoja na watu wote waliokuwa karibu naye.
Kwa upande wake, Deportivo Muniz pia ilitoa salamu za rambirambi, ikisema kuwa hakuna maneno yanayoweza kuelezea ukubwa wa msiba huo.
Tukio hilo limeutikisa ulimwegu wa soka nchini Argentina, huku jumbe mbalimbali za maombolezo zikiendelea kutolewa kumuenzi kijana huyo aliyekuwa na ndoto na matarajio makubwa ya maisha ya soka.