Alcocer aahidi jambo Ufaransa Kombe la Dunia U-17
Muktasari:
- Ushindi huo uliifanya Ufaransa kumaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa Kundi D na kufuzu 32 bora, ikiwa ni majibu mazuri baada ya kiwango ambacho timu hiyo ilionyesha katika mechi iliyopita dhidi ya Saudi Arabia.
KOCHA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Jose Alcocer amesema mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi kwa kikosi hicho kinachoshiriki Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17, baada ya kuonyesha ubora kwa kuifunga Uruguay mabao 3-0 katika mechi ya mwisho ya Kundi D.
Ushindi huo uliifanya Ufaransa kumaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa Kundi D na kufuzu 32 bora, ikiwa ni majibu mazuri baada ya kiwango ambacho timu hiyo ilionyesha katika mechi iliyopita dhidi ya Saudi Arabia.
Alcocer amesema kikosi chake kilihitaji kubadilika dakika 30 na kuonyesha mechi tofauti dhidi ya Uruguay, jambo lililofanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Nahodha wa Ufaransa, Aymen Amaaouch alikuwa miongoni mwa walioonyesha ubora kwa kufunga bao la kwanza dakika ya 22.
Amaaouch amesema hawakuwa na ubora dakika 15 za kwanza na walipoteza nafasi nyingi za wazi.
“Tulifanya mazungumzo na tulitaka kuwa makini zaidi tunapokuwa mbele ya lango. Tulijua tuna uwezo wa kutengeneza nafasi. Wachezaji wapya walipoingia wameongeza nguvu mpya kwenye timu. Kila mmoja alitimiza wajibu wake na alikuwa na mchango. Daima ni jambo la kipekee kufunga bao, hasa katika mchezo wenye uzito kama huu,” amesema Amaaouch.
Mfungaji wa bao la pili, Aly Traore amesema alitumia akili baada ya kugundua kipa wa Uruguay alikuwa ametoka golini kwake na kuamua kupiga shuti lililopita katika kimo cha kichwa.
“Nilimuona kipa akitoka kwenye lango. Niliamua kupiga shuti katika kimo cha kichwa sababu inakuwa vigumu kwa makipa kulizuia na mbinu hiyo ilifanikiwa vizuri,” amesema Traore.
Alcocer alifurahishwa na viwango vya vijana wake akisema walicheza kwa ubora wa hali ya juu kutokana na uwezo wa kufunga mabao matatu huku wakilinda lango lao kutoruhusu bao.
“Nadhani vijana walifanya vizuri. Huo ulikuwa mchezo halisi wa Kombe la Dunia. Tulikuwa karibu sana na ukamilifu; tumefunga mabao matatu na kupata clean sheet,” amesema Alcocer, ambaye alikiri kuwa Uruguay ilikuwa mpinzani mgumu na hakukuwa na tofauti kubwa ya ubora kati ya timu hizo.
Akizungumzia hatua ya mtoano, kocha huyo amesema kuanzia hapo ushindi ndio utakaokuwa muhimu zaidi na mashindano yanaanza upya na kila mchezo utakuwa na uzito wake.
“Tukiweza kudumisha kiwango hiki cha uchezaji, mambo yanaweza kuwa mazuri sana kwetu mbele,” amesema Alcocer.