Kimeumana huko! Real Madrid kutua FIFA
Muktasari:
- Habari hii imeibuka baada ya Dean Huijsen kuonyeshwa kadi nyekundu ya utata dhidi ya Real Sociedad Jumamosi, kwa madai kwamba alinyima mchezaji wa timu pinzani nafasi ya wazi ya kufunga goli.
MADRID, HISPANIA: MABOSI wa Real Madrid wanajiandaa kuwasilisha malalamiko FIFA kutaka kuchunguzwa kwa waamuzi wa La Liga baada ya kudai wanatendewa isivyo haki kutokana na uamuzi wa kadi nyekundu dhidi ya wachezaji wao.
Habari hii imeibuka baada ya Dean Huijsen kuonyeshwa kadi nyekundu ya utata dhidi ya Real Sociedad Jumamosi, kwa madai kwamba alinyima mchezaji wa timu pinzani nafasi ya wazi ya kufunga goli.
Madrid ilikuwa tayari mbele kwa bao moja wakati Mikel Oyarzabal alipowekewa pasi katika dakika ya 32 na kuanza kukimbia kwa kasi, akimwacha nyuma Huijsen ambaye aliamua kumvuta Oyarzabal kwa makusudi na akaonyeshwa kadi nyekundu moja kwa moja, licha ya kwamba Eder Militao alionekana kuwa na nafasi nzuri ya kumzuia Oyarzabal.
Lakini miamba hiyo ya Hispania kupitia kituo chao rasmi, Real Madrid TV, ilidai kwamba uamuzi mgumu kama huo umekuwa kawaida kwao wanapokutana na waamuzi wa La Liga, na sasa wanataka FIFA kufahamu hali hiyo.
Klabu hiyo ilitangaza nia ya kutuma taarifa kamili inayoonyesha tofauti ya rekodi ya kadi nyekundu kati yao na mahasimu wao wakubwa, Barcelona.
Tamko la klabu lilisema: "Real Madrid inatayarisha ripoti ya kila kitu kilichotokea katika raundi nne za kwanza za La Liga na pia kilichotokea msimu uliopita. Ripoti hiyo, ambayo itawasilishwa FIFA, inaonyesha kile kinachoendelea katika soka la Hispania kuhusiana na waamuzi."
Vigogo hao wanadai kuwa utafiti unaonyesha Barcelona wamenufaika mara nyingi na uamuzi wa kadi nyekundu, huku Madrid wakipata hasara, tofauti na ilivyo katika mashindano ya Ulaya.
Kwa mujibu wa tovuti ya Marca, Madrid wanasema ni mara mbili tu katika ligi kwenye kipindi husika ndio timu zilizocheza dhidi yao zilionyeshwa kadi nyekundu wakati wapinzani wao Barcelona wakipata faida ya kadi nyekundu zisizopungua 65 ambazo zilionyeshwa kwa timu ilizocheza nazo.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, takwimu zinaonyesha tofauti ni ndogo zaidi, Barcelona ikiwa imepata faida mara 12 wakati Madrid 13, jambo ambalo linawaaminisha mabosi wa Madrid kwamba kuna shida kwa waamuzi wa La Liga.
Madai haya makali ni mwendelezo wa vita vya muda mrefu kati ya Madrid na waamuzi wa ligi hiyo.
Rais wa Madrid, Florentino Perez, kwa nyakati tofauti amekuwa akionyesha wazi kwamba kuna upendeleo kwa wapinzani wao hata kuonyesha uwezekano wa kugomea baadhi ya mechi au ligi yenyewe.
Mwezi Aprili, Real Madrid TV ilitoa video ikionyesha makosa ya mwamuzi Ricardo de Burgos Bengoetxea, hali iliyomfanya aite mkutano na waandishi wa habari na kulia hadharani akisema: "Kuona mwanangu akirudi nyumbani kutoka shule analia kwa sababu watoto wenzake wamesema baba yake ni tapeli ni jambo gumu mno kuvumilia."
Hata hivyo, madai haya hayajawazuia Madrid kufanya vizuri msimu huu ikiwa imeshinda mechi zote nne za mwanzo ambazo mbili kati ya hizo ilimaliza ikiwa na wachezaji pungufu.