Kidagaa! Man United yampa Carrick mechi ya Chelsea
Muktasari:
- Vyanzo vya ndani ya klabu hiyo vimesema Carrick amepewa nafasi ya kubadili hali ilivyo, huku wachezaji na benchi la ufundi wakijipanga kurekebisha makosa baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Bournemouth katika mchezo uliopita Old Trafford.
LONDON, ENGLAND: MICHAEL Carrick ataendelea kuwa kocha wa Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea Jumamosi, licha ya timu hiyo kupitia kipindi kigumu cha matokeo mabaya, ikiwa imetimiza mechi nane bila ushindi na kushika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi.
Vyanzo vya ndani ya klabu hiyo vimesema Carrick amepewa nafasi ya kubadili hali ilivyo, huku wachezaji na benchi la ufundi wakijipanga kurekebisha makosa baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Bournemouth katika mchezo uliopita Old Trafford.
Carrick aliwasili katika kituo cha mazoezi cha Carrington saa 1:30 asubuhi Jumanne kusimamia mazoezi ya siku hiyo. Wachezaji wa United walikuwa mapumzikoni Jumatatu, lakini walirejea mazoezini saa 4:00 asubuhi kujiandaa na mchezo wa Jumamosi utakaopigwa saa za mchana kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Hata hivyo, viongozi wa United bado hawajaamua kikamilifu kuhusu makocha wanaoweza kuchukua nafasi ya Carrick.
Kocha Antonio Conte, Eddie Howe na Julian Nagelsmann ni miongoni mwa majina yanayozungumziwa, lakini vyanzo vya klabu vinasema hawajashawishika kuwa machaguo hayo yanafaa.
Chanzo kimoja kilichonukuliwa na taarifa hiyo kimesema: “Makocha bora hawatakuja.”
United haijaanzisha mazungumzo rasmi na Conte. Howe, kwa upande wake, amefanya uchunguzi wa awali kuhusu klabu hiyo kutokana na uwezekano wa kupewa ofa, huku mkurugenzi wa usajili wa United, Christopher Vivell, akiwa na uzoefu wa kufanya kazi na Nagelsmann katika mfumo wa klabu za Red Bull.
Kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler, anaonekana kutokuwa tena chaguo la karibu kutokana na gharama kubwa ya fidia ambayo United ingelazimika kulipa ili kumchukua.
Kocha wa Aston Villa, Unai Emery, pia anapendwa na baadhi ya watu ndani ya United. Hata hivyo, ana mkataba na Villa Park hadi mwaka 2029, jambo linaloweza kufanya gharama za kumleta Old Trafford kuwa kubwa.
Pia, Emery anashikilia cheo cha “manager” Aston Villa, tofauti na United ambayo imekuwa ikisisitiza kutumia cheo cha “head coach” tangu Sir Jim Ratcliffe alipokuwa mmiliki mwenza wa klabu hiyo Februari 2024.
Tofauti hiyo ya mamlaka iliwahi kuzua mvutano kati ya mkurugenzi wa soka Jason Wilcox na aliyekuwa kocha wa United, Ruben Amorim. Msimu uliopita, Wilcox alijifananisha na “manager”, jambo lililomkera Amorim na kuchangia kufutwa kwake kazi ghafla Januari.
United ililipa euro milioni 10, ili kuvunja mkataba wa Amorim na Sporting Lisbon Oktoba 2024.
Klabu hiyo ilitumia pauni milioni 2.5 pekee kumchukua Erik ten Hag kutoka Ajax mwaka 2022, huku Molde ikipokea pauni 500,000 kwa ajili ya kumruhusu Ole Gunnar Solskjaer kuondoka Machi 2019.
David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho na Carrick walichukuliwa na United bila klabu hiyo kulipa ada ya kuwanunua.
Kwa sasa, macho yataelekezwa kwa Carrick kuona kama ataweza kubadili mwenendo wa matokeo na kuimarisha nafasi yake, wakati uongozi wa United ukiendelea kutathmini chaguo zake za muda mrefu.