Carrick: Sijaaga Manchester United
Muktasari:
- Carrick, mwenye umri wa miaka 45, alionekana kuguswa na hali ya timu yake baada ya kipigo hicho, akizunguka uwanjani kuwashukuru mashabiki huku akiweka mkono kifuani. Tukio hilo lilizua hisia kwamba huenda alikuwa akitoa salamu za mwisho kabla ya kuondoka kwenye nafasi yake ya ukocha.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Michael Carrick, amesisitiza kuwa hakuwa akiwaaga mashabiki baada ya timu yake kuchapwa mabao 3-0 na Bournemouth katika mchezo wa Ligi Kuu England, EPL, uliopigwa Uwanja wa Old Trafford.
Carrick, mwenye umri wa miaka 45, alionekana kuguswa na hali ya timu yake baada ya kipigo hicho, akizunguka uwanjani kuwashukuru mashabiki huku akiweka mkono kifuani. Tukio hilo lilizua hisia kwamba huenda alikuwa akitoa salamu za mwisho kabla ya kuondoka kwenye nafasi yake ya ukocha.
Hata hivyo, Carrick alikanusha tafsiri hiyo, akisema: “Sikuwa nikiwaaga mashabiki. Kwa kweli, sikutarajia aina hiyo ya sapoti kutoka kwao, lakini siku zote nimehisi upendo na uhusiano mzuri nilio nao na mashabiki.”
Ameongeza kuwa anathamini sana sapoti anayoipata kutoka kwa mashabiki, licha ya timu hiyo kupitia kipindi kigumu.
Kauli hiyo imekuja wakati mustakabali wa Carrick ndani ya Manchester United ukiwa shakani kufuatia matokeo mabaya yanayoendelea kuikabili timu hiyo.
Kipigo dhidi ya Bournemouth kilikuwa cha sita kwa United katika michezo 12 ya msimu huu, hali iliyoongeza presha kwa uongozi wa klabu hiyo kuhusu uwezekano wa kufanya mabadiliko mengine ya benchi la ufundi.
Matokeo hayo pia yamezidisha hofu ya United kuendelea kushuka kwenye msimamo wa EPL, huku uongozi ukikabiliwa na shinikizo la kutafuta suluhisho la haraka.
Akizungumzia uwezekano wa kutimuliwa, Carrick amesema anaelewa uzito wa hali iliyopo, lakini hajui uamuzi ambao uongozi utaufanya kuhusu hatma yake.
“Naelewa kabisa hali tuliyopo. Sitarajii chochote kwa upande wowote. Ninaendelea na majukumu yangu kama kawaida. Ninaipenda klabu hii na nitafanya kile ninachoamini kuwa bora kwa ajili yake,” amesema.
“Ni hali ngumu na hakuna sababu ya kuikwepa. Sijui mambo yataendaje au nini kitafuata. Ninaipenda kazi yangu na ninahisi jukumu nililonalo. Itabidi tusubiri tuone.”
Kocha huyo alikubali kuwajibika kwa matokeo mabaya ya timu yake, akisema amejitahidi kufanya kila linalowezekana kuzuia hali hiyo, lakini mambo hayajaenda kama alivyotarajia.
“Bila shaka, ninachukua jukumu. Naheshimu nafasi niliyonayo na uwajibikaji ni wangu. Nimejaribu kufanya kila ninachoweza ili tusifikie hapa, lakini kwa sababu mbalimbali tumeshindwa kuzuia hali hii,” ameongeza.
Carrick pia amesema inauma kuona klabu aliyodumu nayo kwa muda mrefu ikipitia wakati mgumu kiasi hicho.
Alifichua kuwa bado hajafanya mazungumzo ya kina na Mtendaji Mkuu wa klabu, Omar Berrada, pamoja na Mkurugenzi wa Soka, Jason Wilcox, kuhusu mustakabali wake.
Kwa mujibu wa Carrick, viongozi hao walimfikia baada ya mchezo kama ilivyo kawaida, lakini hakukuwa na mazungumzo maalumu kuhusu hatma yake.
HOWE, NAGELSMANN WATAJWA
Wakati hatma ya Carrick ikizidi kuwa na utata, taarifa zimeeleza kuwa baadhi ya kampuni za kamari zilisitisha kwa muda dau kuhusu uwezekano wa kocha huyo kufutwa kazi.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kuwa wagombea wa kuchukua nafasi yake ni Eddie Howe na Julian Nagelsmann.
Hata hivyo, hakuna uamuzi rasmi uliotangazwa kuhusu uwezekano wa Manchester United kufanya mabadiliko ya kocha.
Mashabiki wa United walionyesha kumuunga mkono Carrick baada ya kipigo hicho, lakini wakati huohuo walielekeza hasira zao kwa wamiliki wa klabu, viongozi wa soka na baadhi ya wachezaji.
NEVILLE AWASHAMBULIA WACHEZAJI
Hata hivyo, beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu namna wachezaji walivyocheza, akiwatuhumu kushindwa kujituma ipasavyo.
Akizungumza kupitia Sky Sports, Neville amesema baadhi ya wachezaji wamekuwa wakiamua wenyewe wakati wa kucheza kwa bidii na wakati wa kupunguza juhudi zao.
“Wameacha kujituma na wamefanya hivyo mara kadhaa. Wanaamua wenyewe lini wawashe moto na lini wazime, kama bomba la maji,” amesema Neville.
Naye beki Harry Maguire, ambaye alikiongoza kikosi hicho katika mchezo huo, alikiri kuwa wachezaji hawafanyi vya kutosha kuisaidia timu.
Maguire alipewa jukumu la unahodha baada ya Bruno Fernandes kuondolewa kwenye kikosi kufuatia ukosoaji wake kuhusu mbinu za kocha.
“Kwa sasa sisi kama wachezaji hatufanyi vya kutosha. Michael alibadilisha kabisa mwelekeo wa msimu wetu uliopita, tulicheza soka zuri na kupata matokeo mazuri. Msimu huu hatujafanya vizuri kama watu binafsi,” amesema Maguire.
Ameongeza kuwa kila mchezaji anapaswa kujitathmini na kujiuliza anaweza kufanya nini zaidi kwa manufaa ya timu.
WACHEZAJI WAMEKATA TAMAA
Beki mwingine wa zamani wa United, Ashley Young, ambaye alishinda taji la EPL na klabu hiyo msimu wa 2012/13, aliwashutumu wachezaji kwa kuonekana kukata tamaa.
Young amesema tatizo la United haliwezi kuendelea kulaumiwa kwa makocha pekee, kwa kuwa wachezaji wengi wameendelea kubaki ndani ya kikosi licha ya mabadiliko ya benchi la ufundi.
“Tumekuwa na makocha tofauti katika misimu ya hivi karibuni, lakini wachezaji ni wale wale. Kumekuwa na mabadiliko machache, lakini hawaonyeshi chochote,” amesema.
“Leo ilionekana kana kwamba wamekata tamaa. Hawamkimbilii kocha huyu wala kuonyesha utayari wa kupambana. Mashabiki wanastahili mengi zaidi na inaonekana wazi kuwa kocha ameachwa kwenye wakati mgumu na wachezaji wake.”
Mchambuzi Jamie Carragher naye amesema nafasi ya Carrick imekuwa ngumu kutetewa baada ya matokeo hayo, ingawa baadhi ya wadau wanaamini kuwa uongozi wa klabu nao unapaswa kulaumiwa.
FERNANDES NAYE AINGIA MJADALA
Licha ya lawama kuelekezwa kwa wachezaji, mamlaka ya Carrick ndani ya kikosi nayo imeanza kuhojiwa, hasa baada ya kauli za Martinez na Fernandes kuhusu mbinu za timu.
Fernandes alikosolewa baada ya kueleza kuwa United wakati mwingine hushindwa kuwabana wapinzani kwa presha ya juu, jambo linalowapa nafasi ya kujenga mashambulizi kwa utulivu.
Alipoulizwa kama alimaanisha kuwa Carrick na benchi lake walikosea mbinu, Fernandes amesema hilo ni suala la kocha na benchi lake kulijibu.
Kauli hizo zilichangia mjadala kuhusu uhusiano kati ya kocha na wachezaji wake, huku Fernandes akiachwa nje ya kikosi kilichokutana na Bournemouth.
Gwiji wa zamani wa United, Wayne Rooney, naye aliwakosoa vikali wachezaji wa sasa, akiwaita wabinafsi na kuwashutumu kwa kukwepa kuwajibika wanapokabiliwa na matokeo mabaya.
Rooney amesema baadhi ya wachezaji wanapokosa mambo wanayotaka, huanza kulaumu wengine badala ya kujitathmini na kuangalia namna wanavyoweza kuisaidia timu.