Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wezi wakurupushwa nyumbani kwa Yamal

YAMAL Pict

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa hizo, nyumba hiyo yenye thamani ya Pauni 9.5 milioni (takribani Sh33 bilioni) ilivamiwa na watu wawili waliokuwa wamejifunika nyuso kwa kofia na mavazi maalumu.

NYUMBA ya kifahari ya nyota wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Lamine Yamal, iliyopo jijini Barcelona, imevamiwa na watu waliodhaniwa kuwa wezi saa chache tu baada ya mchezaji huyo kuisaidia Hispania kuifunga Ufaransa na kutinga fainali ya Kombe la Dunia 2026. 

Polisi wa eneo la Catalonia, wamefungua uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, nyumba hiyo yenye thamani ya Pauni 9.5 milioni (takribani Sh33 bilioni) ilivamiwa na watu wawili waliokuwa wamejifunika nyuso kwa kofia na mavazi maalumu.

Wezi hao walionekana wakipanda ukuta wa nyumba hiyo iliyopo katika kitongoji cha kifahari cha Esplugues de Llobregat.

Hata hivyo, jaribio lao la kuingia ndani halikufanikiwa baada ya walinzi binafsi wa Yamal kugundua harakati zao mapema na kuwatimua kabla hawajatekeleza uhalifu wao.

Inaelezwa kuwa, tukio hilo lilitokea majira ya saa 10 alfajiri kwa saa za Hispania siku ya Jumatano, Julai 15, 2026. 

YAMA 01

Kufuatia tukio hilo, Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai kimechukua jukumu la kuendelea na uchunguzi, kikitumia picha zilizorekodiwa na kamera za usalama (CCTV) zilizowekwa katika eneo la nyumba hiyo ili kuwabaini wahusika.

Nyumba hiyo ya kifahari ina historia yake, kwani awali ilikuwa ikimilikiwa na beki wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Gerard Pique pamoja na aliyewahi kuwa mpenzi wake, mwanamuziki maarufu wa Colombia, Shakira.

Taarifa zinadai Yamal aliinunua nyumba hiyo hivi karibuni.

Nyumba hiyo yenye ukubwa wa futi za mraba 3,800, ina huduma nyingi za kifahari ikiwemo mabwawa ya kuogelea ya ndani na nje, uwanja wa tenisi pamoja na studio ya kurekodia muziki. 

Yamal mwenyewe amewahi kuchapisha picha za nyumba hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram.

Inaelezwa kuwa, Yamal siyo mchezaji wa kwanza wa soka kulengwa na wahalifu katika miezi ya hivi karibuni, kwani mastaa maarufu kadhaa wamejikuta wakikumbwa na matukio ya aina hiyo, hasa wanapokuwa mbali na makazi yao kwa ajili ya mashindano au majukumu ya timu zao.

YAMA 02

Miongoni mwa wachezaji wa Barcelona waliokumbwa na matukio kama hayo ni kipa Joan Garcia, ambapo mapema mwaka huu nyumba yake ilivamiwa wakati akiwa nchini Saudi Arabia akishiriki mashindano ya Spanish Supercopa.

Katika tukio hilo, watu wawili waliovaa mavazi meusi waliingia ndani na kuiba.

Naye beki Pau Cubarsi wa timu hiyo aliwahi kuporwa saa ya thamani kubwa nyumbani kwake alipokuwa mazoezini na timu yake baada ya kipindi cha sikukuu za Krismasi mwaka jana.

Taarifa zinaeleza kuwa, makundi ya wahalifu yamekuwa yakitumia taarifa za ratiba za wanasoka kujua wanapokuwa nje ya nchi au mbali na makazi yao kisha kuvamia nyumba zao yakiamini hakuna watu.

Mfano mwingine unaotajwa ni staa wa Manchester City, Jack Grealish ambaye mwaka 2023 alipoteza vito na mali nyingine zenye thamani ya takribani Pauni 1 milioni baada ya nyumba yake kuvamiwa. Hadi sasa polisi hawajawakamata wahusika wa tukio hilo.

Pia Raheem Sterling, nyota wa zamani wa timu hiyo na Chelsea, aliwahi kuwa mwathirika wa matukio matatu tofauti ya uvamizi wa nyumba. 

Moja ya matukio hayo lilimlazimu kuondoka haraka katika Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar ili kurejea nyumbani baada ya familia yake kukumbwa na tukio hilo.

Kwa upande wa Yamal, tukio hilo linaonekana kufunika kwa kiasi na furaha yake ya kuifikisha Hispania fainali ya Kombe la Dunia 2026.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 alikuwa mmoja wa wachezaji walioonyesha kiwango bora katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ufaransa, ushindi uliowapeleka Wahispania kwenye mechi ya mwisho ya mashindano hayo.