Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli ya mke wa Fury yazua utata

Muktasari:

  • Utata huo ulizuka baada ya kampuni ya Netflix kutumia sehemu ya mahojiano ya Paris katika kutangaza makala maalumu ya dakika 90 kuhusu maisha ya Fury, ambapo alidai kuwa mumewe ana tatizo la afya ya akili linalohusishwa na ugonjwa wa Schizophrenia.

LONDON, UINGEREZA: PAMBANO linalosubiriwa kwa hamu kati ya mabondia nyota wa Uingereza, Tyson Fury na Anthony Joshua nusuru livurugika kutokana na mkanganyiko kuhusu taarifa za afya ya akili za Fury, zilizotolewa na mkewe Paris na baadaye kupingwa na mwanamke huyo.

Utata huo ulizuka baada ya kampuni ya Netflix kutumia sehemu ya mahojiano ya Paris katika kutangaza makala maalumu ya dakika 90 kuhusu maisha ya Fury, ambapo alidai kuwa mumewe ana tatizo la afya ya akili linalohusishwa na ugonjwa wa Schizophrenia.

Katika mahojiano hayo, Paris alisema: “Ana Schizophrenia ya kiwango cha chini, lakini hata hivyo sikuweza kuelewa. Nilijiuliza, inawezekanaje? Nilidhani watu wenye matatizo makubwa ya akili ndio wana Schizophrenia.”

Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa, hasa kutokana na masharti ya Bodi ya Ngumi ya Kulipwa ya Uingereza (BBBoC), yanayomzuia bondia kushiriki pambano ikiwa anasumbuliwa na matatizo fulani ya kisaikolojia, yakiwemo sonona, Schizophrenia au Hypermania.

Hata hivyo, mkanganyiko huo uliongezeka baada ya Fury mwenyewe kuthibitisha kuwa aliwahi kufanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa na Schizophrenia pamoja na ugonjwa wa Bipolar.

Akizungumzia hali hiyo wakati wa kuitangaza makala hiyo, Fury alisema: “Nilikwenda kwa mtaalamu anayeongoza katika eneo hilo na kugundulika kuwa nina Schizophrenia na Bipolar. Nimejifunza kuwa huwezi kuondokana kabisa na changamoto za afya ya akili, bali unaweza kujifunza namna ya kuzidhibiti na kuishi nazo.”

Alhamisi jioni, mwandishi wa habari za ngumi wa Daily Mail Sport, Jeff Powell, aliripoti kuwa taarifa hizo zilikuwa zimezua sintofahamu kuhusu uwezekano wa Fury kushiriki pambano lililopangwa kufanyika Desemba 11.

Ripoti hiyo ilifuatiliwa na vyombo vingine vya habari nchini Uingereza, huku suala hilo likianza kuibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa pambano hilo.

Katibu Mkuu wa BBBoC, Robert Smith, alisisitiza kuwa Fury hataruhusiwa kuingia ulingoni hadi madaktari wa bodi hiyo watakapojiridhisha kuwa hakuna hatari kwa afya yake.

Alisema: “Tyson hataruhusiwa kuingia ulingoni isipokuwa madaktari wetu waridhike kuwa hakuna hatari kwa afya yake.”

Hali hiyo iliwaweka katika wakati mgumu waandaaji wa pambano pamoja na Netflix, ambao walilazimika kufanya mabadiliko ya haraka katika makala hiyo saa chache kabla ya kuanza kuonyeshwa duniani kote.

Sehemu iliyokuwa na kauli ya Paris kuhusu madai ya mumewe kuwa na Schizophrenia iliondolewa, huku Netflix ikieleza kuwa taarifa mpya zilikuwa zimepatikana.

Taarifa hizo mpya zilihusisha ufafanuzi wa Paris aliyoutoa baada ya kuzuka kwa mjadala huo, akibadilisha kauli yake ya awali.

Katika maelezo yake, alisema: “Nilikumbuka mazungumzo ya miaka mingi iliyopita tulipokuwa tukizungumzia hali ya Tyson, ndipo nilipotumia neno ‘Schizophrenic’.

“Ingawa Tyson aliwahi kuonyesha baadhi ya dalili zinazohusishwa na Schizophrenia, hana ugonjwa huo na hajawahi kugundulika kuwa nao.”

Aliongeza kuwa masuala ya afya ya akili ni changamani na wakati mwingine si rahisi kupata maneno sahihi ya kuelezea hali ya mtu, hasa unapokuwa unaishi na mtu unayempenda anayepitia changamoto hizo.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Paris ilizua mkanganyiko zaidi kwa sababu ilitofautiana na maelezo ya Fury mwenyewe, ambaye alikuwa amesema alifanyiwa uchunguzi na mtaalamu wa afya na kugundulika kuwa na magonjwa hayo mawili.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo lilikuwa tishio kwa maandalizi ya pambano hilo, ambalo lilitarajiwa kuwa miongoni mwa mapambano makubwa zaidi katika historia ya ngumi za kulipwa nchini Uingereza.

Netflix ilitarajia kuwa na watazamaji milioni 60, huku rais wa kampuni ya uendelezaji wa ngumi ya Zuffa Boxing, Dana White, akitabiri kuwa pambano hilo lingevutia mapato ya tiketi ya pauni milioni 26 katika Uwanja wa Principality.

Aidha, mabondia hao walitarajiwa kugawana kitita cha pauni milioni 150.

Hivyo, uwezekano wa pambano hilo kufutwa ungekuwa pigo kubwa kwa waandaaji, kampuni ya utangazaji na wadau wa mchezo huo.