Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo sita fainali ya Copa Libertadores 2026

FAINALI Pict

Muktasari:

  • Fainali hiyo inakutanisha klabu kutoka mataifa mawili yenye historia kubwa ya soka. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni nguvu zimeelemea upande wa Brazil, ambazo zimetwaa mataji saba ya mwisho mfululizo. Palmeiras ina nafasi ya kuongeza mafanikio hayo.

RIO DE JENEIRO, BRAZIL: PALMEIRAS ya Brazil na Estudiantes ya Argentina zinakutana leo Jumamosi katika fainali ya Copa Libertadores ya Shirikisho la Soka Amerika Kusini (CONMEBOL), itakayochezwa Uwanja wa Centenario mjini Montevideo, Uruguay, kuanzia saa 5:00 usiku.

Fainali hiyo inakutanisha klabu kutoka mataifa mawili yenye historia kubwa ya soka. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni nguvu zimeelemea upande wa Brazil, ambazo zimetwaa mataji saba ya mwisho mfululizo. Palmeiras ina nafasi ya kuongeza mafanikio hayo.

Mbele yake kuna Estudiantes de La Plata, klabu yenye historia kubwa katika mashindano hayo. Kiwango cha Fernando Muslera, safari ya kocha Abel Ferreira na urithi wa familia ya Verón ni mambo yanayoongeza mvuto wa fainali hii.


FAI 01

BRAZIL KUWA KINARA WA MATAJI?

Brazil haijawahi kuongoza peke yake kwa idadi ya mataji ya Copa Libertadores. Mara mbili imefikia kilele hicho kwa sare; mwaka 1963 ilikuwa na mataji mawili sawa na Uruguay, na mwaka 2025 ilikuwa na mataji 25 sawa na Argentina.

Klabu za Brazil zina rekodi ya kutwaa mataji saba mfululizo. Ushindi wa Palmeiras utaifanya nchi hiyo kufikisha mataji 26 na kuipita Argentina. Mafanikio hayo yamechangiwa na Flamengo iliyotwaa mataji matatu, Palmeiras mawili, pamoja na Fluminense na Botafogo zilizotwaa taji moja kila moja.


MUSLERA KUREJESHA HESHIMA

Kipa Fernando Muslera anataka kutumia fainali hii kurejesha heshima yake baada ya kupitia kipindi kigumu akiwa na timu ya taifa ya Uruguay. Katika Kombe la Dunia 2026, Uruguay ilikusanya pointi mbili katika Kundi H na kutolewa.

Hata hivyo, akiwa na Estudiantes amebadili taswira hiyo. Kipa huyo mwenye miaka 40 ameiongoza timu yake kufika fainali, akifanya vizuri katika hatua za mtoano. Hakuruhusu bao katika michezo yote miwili ya nusu fainali na mchezo wa marudiano wa robo fainali.

Mchango wake mkubwa ulionekana katika nusu fainali dhidi ya mabingwa watetezi Flamengo, Uwanja wa Maracana. Baada ya timu hizo kutoka sare katika michezo miwili, Muslera aliokoa penalti tatu kati ya tano za Flamengo kwenye mikwaju ya penalti, ikiwamo ya Jorginho. Akawa kipa wa tatu kuokoa penalti tatu katika mikwaju ya nusu fainali au fainali, akifuata José Cevallos na René Higuita.


FAI 04

FERREIRA KUANDIKA HISTORIA

Palmeiras inawania kuwa klabu ya Brazil inayoshiriki rekodi ya kutwaa mataji mengi zaidi ya Copa Libertadores. Ina mataji matatu, ikiwa nyuma ya Flamengo yenye manne. Kocha Abel Ferreira ameiongoza Palmeiras kutwaa mawili kati ya mataji hayo na sasa ana nafasi ya kuongeza jingine.

Ferreira alianza kuifundisha Palmeiras katika hatua ya 16 bora mwaka 2020. Tangu wakati huo ameiongoza kucheza mechi 77 za Copa Libertadores, akishinda 49, kutoka sare 18 na kupoteza 10.

Ushindi katika fainali utamfikisha kwenye ushindi wake wa 50 na kumfanya kuwa kocha wa tatu kufikia idadi hiyo baada ya Renato Gaúcho na Marcelo Gallardo.

Pia ana nafasi ya kuwa kocha wa tatu kutwaa Copa Libertadores mara tatu. Osvaldo Zubeldía alifanya hivyo akiwa na Estudiantes, huku Carlos Bianchi akitwaa mara tatu na Boca Juniors na mara moja akiwa na Vélez Sarsfield.


FAI 02

URITHI WA FAMILIA YA VERÓN

Familia ya Verón ina nafasi ya pekee katika historia ya Estudiantes. Juan Ramón Verón alitwaa mataji matatu mfululizo ya Copa Libertadores akiwa na klabu hiyo kati ya 1968 na 1970. Pia aliifungia Manchester United bao Old Trafford Oktoba 1968, lililosaidia Estudiantes kutwaa Kombe la Mabara.

Mwanawe Juan Sebastián Verón alirejea Estudiantes mwaka 2006 akiwa na dhamira ya kuirudisha klabu hiyo kileleni mwa soka la Amerika Kusini. Alitimiza azma hiyo mwaka 2009 alipokuwa nahodha wa timu iliyotwaa taji lake la nne la Copa Libertadores.

Sasa, miaka 17 baadaye, Verón anaweza kuongeza ukurasa mwingine katika historia ya familia akiwa rais wa klabu. Alianza kushika nafasi hiyo mwaka 2014 na kurejea tena Aprili 2024. Chini ya uongozi wake, Estudiantes imetwaa mataji matano ya ndani ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitatu.


TIMU MBILI ZINAZOFANANA

Fainali hii huenda isiwe ya pasi nyingi, kumiliki mpira kwa muda mrefu au chenga nyingi. Palmeiras hupendelea kumiliki mpira, wakati Estudiantes huweka mkazo katika presha kwa wapinzani. Hata hivyo, timu hizo zinafanana katika kutumia mipango inayozingatia uhalisia na kubadilika kulingana na mpinzani.

Kwa kasi ya kuelekea langoni, Palmeiras ina wastani wa mita 1.5 kwa sekunde, huku Estudiantes ikiwa na mita 1.7. Katika hatua za mtoano, Palmeiras imekuwa na wastani wa kumiliki mpira wa asilimia 44 dhidi ya 40 za Estudiantes.

Estudiantes haijawahi kuwa nyuma kwa bao katika mechi sita zilizopita, wakati Palmeiras imetumia dakika 31 ikiwa katika nafasi ya kupoteza. Takwimu hizo zinaonyesha namna timu hizo zinavyofanana katika mbinu na uwezo wa kubadilika kulingana na hali ya mchezo.


FAI 03

SOSA KUKAMILISHA SAFARI YAKE

Kwa José Sosa, kutwaa Copa Libertadores kutakuwa kama kulipiza deni la kihistoria. Kiungo huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha Estudiantes kilichotwaa ubingwa wa Apertura 2006 pamoja na Juan Sebastián Verón. Pia alifunga bao katika mchezo wa mchujo dhidi ya Boca Juniors lililoisaidia timu kutwaa taji lake la kwanza la ligi baada ya miaka 23.

Kiwango chake kilimuwezesha kujiunga na Bayern Munich mwaka 2007, hivyo akakosa kushiriki mafanikio ya Estudiantes kutwaa Copa Libertadores 2009. Aliporejea kwa mkopo mwishoni mwa mwaka huo, FIFA ilikataa kuidhinisha usajili wake.

Alirejea rasmi mwaka 2010, lakini safari ya timu kutetea ubingwa iliishia robo fainali baada ya kutolewa na Internacional.

Baadaye alitumia miaka 12 akicheza nje ya Argentina katika klabu zilizojumuisha Napoli, Atlético Madrid na AC Milan. Agosti 2022, akiwa na miaka 37, alirejea Estudiantes kwa mara ya tatu.

Ushiriki wake katika kampeni ya Libertadores msimu huu umekuwa mdogo, lakini alijitokeza katika nusu fainali kwa kufunga penalti iliyosaidia Estudiantes kufuzu.

Sasa akiwa na miaka 41, Sosa, anayefahamika kwa jina la utani El Principito (Mfalme Mdogo), anakaribia kuweka historia. Estudiantes ikishinda, atakuwa mchezaji wa Argentina mwenye umri mkubwa zaidi kutwaa Copa Libertadores, akiwa na miaka 41 na siku 162.

Baada ya kukosa mafanikio ya mwisho ya klabu mwaka 2009, sasa ana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Amerika Kusini na kukamilisha safari yake ya kihistoria.