Ndoa ya Neuer yaingia mdudu
Muktasari:
- Vyombo vya habari nchini Ujerumani viliripoti kuwa wanandoa hao walitengana muda mfupi baada ya kupata mtoto wao wa pili mwezi Agosti mwaka huu.
MUNICH, Ujerumani: MKE wa kipa wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Manuel Neuer, Anika, ametoa kauli kali kwenye mitandao ya kijamii kufuatia uvumi unaodai kuwa mumewe alimsaliti wakati akiwa mjamzito.
Vyombo vya habari nchini Ujerumani viliripoti kuwa wanandoa hao walitengana muda mfupi baada ya kupata mtoto wao wa pili mwezi Agosti mwaka huu.
Neuer, mwenye umri wa miaka 40, baadaye alipigwa picha akiwa nchini Brazil na mwanamke ambaye utambulisho wake haujafahamika. Gazeti la Bild lilidai kuwa mwanamke huyo ana umri wa miaka 23 na ni mtaalamu wa tiba ya viungo ambaye amewahi kufanya kazi na kipa huyo.
Neuer alisafiri kwenda Amerika Kusini baada ya kupata jeraha la kuchanika kwa sehemu ya kano ya mguu wake wa kulia wakati wa mchezo wa Bundesliga dhidi ya Mainz, Novemba 7.
Pia, taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Ujerumani zilidai kuwa Neuer na mwanamke huyo walikuwa pamoja nchini Sicily mwishoni mwa Septemba.
Anika, mwenye umri wa miaka 26, ambaye ni mchezaji wa zamani wa mchezo wa mikono (handball) na jina lake la awali la ukoo ni Bissel, aliamua kuzungumza baada ya uvumi huo kusambaa kwa kasi mitandaoni.
Katika hatua hiyo, alishiriki ujumbe uliokosoa vikali kitendo cha mwanaume kumsaliti mwanamke wakati wa ujauzito, ukieleza kuwa ni ukatili mkubwa zaidi.
Ujumbe huo ulieleza kuwa ni jambo lisilokubalika mwanaume kumsaliti mwanamke anayebeba mtoto wake, huku akishuhudia mabadiliko ya mwili wake, uchovu na changamoto mbalimbali anazopitia wakati wa ujauzito.
Pia, ulisisitiza kuwa mwanamke anayestahili kupendwa, kulindwa na kupewa msaada wakati huo huishia kukabiliana na maumivu yanayosababishwa na usaliti wa mwenza wake.
Ujumbe huo ulieleza kuwa kitendo hicho si kosa la bahati mbaya, bali ni uamuzi wa ubinafsi, ukosefu wa huruma na heshima kwa mwanamke anayebeba mtoto wake.
Neuer na Anika wana watoto wawili wa kiume. Mtoto wao wa kwanza, Luca, alizaliwa Machi 2024, huku jina la mtoto wao wa pili likiwa halijawekwa wazi.
Mwaka 2025, Anika alitangaza kusitisha kucheza handball katika ngazi ya kulipwa ili kupata muda zaidi wa kuwa na familia yake.
Katika taarifa yake wakati huo, alisema uamuzi huo haukuwa rahisi kutokana na upendo wake kwa timu na mchezo huo, lakini alihitaji muda zaidi wa kumlea mtoto wake.
Alisisitiza kuwa hakuuchukulia uamuzi huo kama mwisho wa safari yake ya handball, bali mapumziko yaliyolenga kumpa nafasi ya kuipa familia kipaumbele.
Wakati akitangaza uamuzi huo, alisema angewakumbuka wachezaji wenzake na mchezo huo, hivyo alitaka kufurahia mechi zake za mwisho na kumaliza msimu kwa mafanikio.