KASHA: Van Gaal akataa kumrudisha Ronaldo kambi ya Old Trafford
Muktasari:
Alfredo Duro, mwandishi anayeheshimika nchini Hispania juzi usiku akiwa katika kipindi maarufu cha televisheni ya El Chiringuito nchini humo alidai kwamba kocha wa Manchester United, Louis van Gaal alikataa kumnunua Cristiano Ronaldo mwezi uliopita.
PENYE chuki penyeza fitina. Wakati mashabiki wa Manchester United wakiomboleza kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Swansea ugenini, mwandishi mmoja nchini Hispania amezidi kuchochea hasira Old Trafford.
Alfredo Duro, mwandishi anayeheshimika nchini Hispania juzi usiku akiwa katika kipindi maarufu cha televisheni ya El Chiringuito nchini humo alidai kwamba kocha wa Manchester United, Louis van Gaal alikataa kumnunua Cristiano Ronaldo mwezi uliopita.
Duro amedai kwamba wakala wa Cristiano Ronaldo, Jorge Mendes alipaa hadi jijini Manchester mwezi uliopita kwa ajili ya kukutana na skauti wa Manchester United, Martin Ferguson ambaye ni mdogo wake kocha wa zamani wa Man United, Sir Alex Ferguson.
Mendes alitoa ofa kwa Ferguson kumnunua Ronaldo kwa mara nyingine klabuni hapo, lakini wakati Ferguson alipokwenda kutoa wazo hilo kwa Van Gaal, mdachi huyo alimkatalia hapo hapo kwa madai kwamba hamhitaji Ronaldo.
Stori ya Ronaldo kurudi Old Trafford imekuwa ikipamba moto katika vyombo vya habari vya Uingereza tangu msimu uliopita na Septemba mwaka jana, baadhi ya mashabiki wa Man United walisafiri mpaka Hispania wakiwa na bango linalomsihi Ronaldo arudi Manchester likiwa limeandikwa ‘Rudi nyumbani’.
Uvumi wa Ronaldo kurudi Old Trafford ulipotea katika miezi ya karibuni, lakini sasa unaweza kufufuka kutokana na stori hii ya mwandishi Alfredo Duro, ambaye ni mmoja kati ya waandishi wanaoheshimika nchini Hispania.
Habari hii itakuwa kama chumvi katika kidonda kwa Van Gaal, ambaye inadaiwa pia katika kipindi cha majira ya joto mwaka jana, alizitosa fursa za kuwanunua staa wa Barcelona, Cesc Fabregas na staa wa Bayern Munich, Toni Kroos.
Wakati Fabregas alitimkia Chelsea ambako sasa ni mchezaji muhimu akiwa anapika mabao mengi ya timu hiyo huku akiongoza katika orodha ya wapiga pasi za mabao, Kroos anang’ara Real Madrid na amekuwa mchezaji wa kudumu Santiago Bernabeu.
Sasa madai kwamba Van Gaal alimpotezea Ronaldo kurudi Old Trafford yanaweza kuzua kasheshe kubwa kwa kocha huyo Mdachi, ambaye anasifika kwa tabia yake ya kuvuruga wachezaji mastaa tangu akiwa katika klabu za Barcelona na Bayern Munich.