Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kane ajifunga Bayern Munich

KANE Pict

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ujerumani, Kane anatarajiwa kulipwa kiasi cha pauni 400,000 (zaidi ya shilingi bilioni 1.4)  kwa wiki kupitia mkataba huo mpya, mshahara unaotajwa kuwa mkubwa zaidi kwa kiwango cha msingi kwa mchezaji barani humo.

MUNICH, UJERUMANI: NAHODHA wa timu ya taifa ya England, Harry Kane, ameongeza mkataba wake wa kuitumikia Bayern Munich hadi mwaka 2029, hatua inayotarajiwa kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa fedha nyingi zaidi barani Ulaya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ujerumani, Kane anatarajiwa kulipwa kiasi cha pauni 400,000 (zaidi ya shilingi bilioni 1.4)  kwa wiki kupitia mkataba huo mpya, mshahara unaotajwa kuwa mkubwa zaidi kwa kiwango cha msingi kwa mchezaji barani humo.

Uamuzi wa Kane kuendelea kusalia Bayern umemaliza matumaini ya mashabiki waliokuwa wakitamani kumuona akirejea Ligi Kuu England ili kujaribu kuvunja rekodi ya mabao ya Alan Shearer.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33, alikuwa akiingia kwenye miezi sita ya mwisho ya mkataba wake wa awali, lakini sasa ameamua kuendelea kuandika historia ndani ya miamba hiyo ya Ujerumani.

KAN 01

Tangu alipojiunga na Bayern akitokea Tottenham Hotspur mwaka 2023, Kane amefunga mabao 156 katika mechi 161 alizoichezea klabu hiyo.

Msimu uliopita ulikuwa wa kipekee kwake baada ya kufunga mabao 73 katika mechi 65 alizocheza akiwa na klabu na timu ya taifa, kiwango kilichomuweka mbele ya nyota kama Kylian Mbappe na Lamine Yamal katika tuzo ya Ballon d'Or.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba mpya, Kane amesema amejisikia kuwa nyumbani tangu alipojiunga na Bayern na hana mpango wa kuondoka kwa sasa.

KAN 03

"Ninahisi niko nyumbani kabisa Bayern Munich. Ninaipenda klabu, mashabiki na jiji la Munich. Tuna kikosi kizuri na kocha mzuri Vincent Kompany," amesema Kane.

Ameongeza kuwa familia yake imezoea maisha ya Ujerumani na ana hamu ya kuendelea kutwaa mataji akiwa na klabu hiyo.

"Familia yangu yote ina furaha hapa. Nilikuwa na hamu ya kusalia. Sasa ninatazamia mustakabali na nataka kushinda mataji mengi zaidi na klabu hii kubwa," amesema.

Kane alijiunga na Bayern akiwa bado hajawahi kutwaa taji kubwa katika ngazi ya klabu, lakini amefanikiwa kubadilisha historia hiyo kwa kushinda mataji mbalimbali ndani ya misimu yake miwili ya kwanza.

Miongoni mwa mafanikio yake ni mataji mawili ya Bundesliga, Kombe la DFB na mataji mawili ya German Super Cup.

Mbali na mafanikio ya timu, amekuwa akikusanya tuzo binafsi, ikiwemo kutambuliwa kama mfungaji bora wa Bundesliga katika misimu yote miwili na kutwaa Golden Shoe mara mbili kama mmoja wa wafungaji bora barani Ulaya.

KAN 02

Kwa upande wa timu ya taifa, Kane ameendelea kuwa mhimili muhimu wa England, akiwa tayari ndiye mfungaji bora wa muda wote wa nchi hiyo kwa mabao 91, tofauti ya mabao 38 dhidi ya Wayne Rooney anayeshika nafasi ya pili.

Pia anashiriki rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi kwa England akiwa na Peter Shilton, wote wakiwa na mechi 125.

Kane, ambaye ameishi Ujerumani pamoja na mke wake Kate na watoto wao wanne tangu mwaka 2023, amesema familia yake imefurahia maisha mapya nchini humo.

Alieleza kuwa watoto wake wameanza kuzoea mazingira ya shule na maisha ya kila siku, jambo lililochangia familia nzima kuifanya Munich kuwa nyumbani.

Kwa mkataba huo mpya, Bayern imeonyesha wazi kuwa Kane ni sehemu muhimu ya mipango yake ya muda mrefu, huku nyota huyo akipewa jukumu la kuendelea kuiongoza klabu hiyo katika harakati za kutwaa mataji zaidi ndani na nje ya Ujerumani.