Kama babu! Pochettino anapita njia ya Ferguson
Muktasari:
- Pochettino ana kazi kubwa ya kuifanya Man United irudi katika ubora wake, ikiwamo kuongeza uwezo wa kimwili wa wachezaji, kuanzisha mfumo wa kucheza kwa presha kubwa (high pressing), kupunguza makosa binafsi yanayojirudia, kukabiliana na majeraha pamoja na adhabu za kusimamishwa kwa wachezaji.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA mpya wa Manchester United, Mauricio Pochettino ameanza kuonyesha dalili za kufuata falsafa ya aliyekuwa kocha mashuhuri wa klabu hiyo, Sir Alex Ferguson, kwa kujenga mazingira ya kuwaunganisha wachezaji wake katika hali ya kupambana na kile anachoamini ni upinzani kutoka nje ya klabu.
Pochettino ana kazi kubwa ya kuifanya Man United irudi katika ubora wake, ikiwamo kuongeza uwezo wa kimwili wa wachezaji, kuanzisha mfumo wa kucheza kwa presha kubwa (high pressing), kupunguza makosa binafsi yanayojirudia, kukabiliana na majeraha pamoja na adhabu za kusimamishwa kwa wachezaji.
Pia anatakiwa kufanya kazi ndani ya bajeti ndogo ya usajili, kurejesha utambulisho wa timu na kusimamia ratiba ngumu ya mechi zinazochezwa kila baada ya siku tatu au nne.
Hata hivyo, tofauti na mtangulizi wake Michael Carrick, ambaye alionekana kupendelea kutuliza hali na kuepuka mijadala mikubwa nje ya uwanja, Pochettino ameanza kuchukua msimamo mkali dhidi ya maamuzi ya waamuzi.
Mbinu hiyo imeonekana kuungwa mkono na watu mbalimbali ndani ya klabu, huku ikikumbusha namna Ferguson alivyokuwa akitumia migogoro ya nje ya uwanja kuwaunganisha wachezaji wake.
Pochettino amekuwa akimkubali Ferguson kwa muda mrefu na mwaka 2016 alipata nafasi ya kukutana naye katika chakula cha mchana cha faragha. Mazungumzo yao yalikuwa miongoni mwa matukio muhimu yaliyomjenga katika safari yake ya ukocha.
Ferguson aliwahi kumweleza umuhimu wa kocha mkubwa kusimamia mambo mawili kwa wakati mmoja; ushindi ndani ya uwanja na vita ya kisaikolojia nje ya uwanja.
Kwa mujibu wa falsafa hiyo, ushindi nje ya uwanja ni muhimu sawa na ushindi unaopatikana ndani ya dakika 90.
Pochettino mwenyewe aliwahi kusema: “Sir Alex Ferguson anawakilisha kila kitu ninachokithamini kwa kocha, meneja na mwanadamu. Anaakisi maadili yangu na ninamheshimu sana.”
Dalili za falsafa hiyo zimeanza kuonekana tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuiongoza United.
VITA NA WAAMUZI VYAZIDI KUCHUKUA KASI
Katika mchezo dhidi ya Liverpool, Pochettino alikerwa na kadi nyekundu aliyoonyeshwa Leny Yoro, akiamini kuwa beki huyo hakustahili kutolewa nje.
Baadaye, jopo huru la tathmini lilibatilisha uamuzi huo kwa kura zote tano, lakini mkuu wa ProRef, Howard Webb, aliendelea kutetea uamuzi wa awali wa mwamuzi.
United haikuishia hapo, kwani klabu hiyo ilionyesha kutoridhishwa na namna suala hilo lilivyoshughulikiwa na sasa imepeleka malalamiko yake kwa Ligi Kuu England.
Pochettino pia alidai kuwa bao la kwanza la Liverpool lililofungwa na Dominik Szoboszlai halikupaswa kuhesabiwa kutokana na kile alichodai kuwa ni kuingiliwa kwa mpangilio wa ukuta wa mabeki wakati wa mpira wa adhabu.
Akizungumzia suala hilo kwa kejeli, amesema:
“Labda sheria zimebadilika wakati nilipokuwa Marekani? Kwa nini hawakulikagua? Bao hilo lilipaswa kufutwa. Nipo hapa kuwatetea wachezaji wangu na klabu yangu.”
DRAMA YA LISBON YAMKERA ZAIDI
Baada ya tukio la Anfield, United ilisafiri kwenda Lisbon kwa mchezo mwingine ambao uliibua malalamiko makubwa dhidi ya mwamuzi Szymon Marciniak.
Katika mchezo huo, bao la Amad lilifutwa kwa madai ya faulo iliyofanywa na Youri Tielemans, licha ya Pochettino kuamini kuwa hakukuwa na kosa lolote.
Tielemans alipewa kadi ya njano katika tukio hilo, kabla ya baadaye kutolewa kwa kadi nyekundu.
United pia ilinyimwa bao ambalo lingeweza kuwa la ushindi baada ya mwamuzi kufuta bao hilo kwa madai ya Patrick Dorgu kumfanyia faulo kipa wa wapinzani.
Mbali na hilo, mwamuzi huyo alitoa penalti dhidi ya Lisandro Martinez katika tukio ambalo Pochettino aliamini kuwa lilitokana na kudanganywa.
Kocha huyo alionekana kukasirika mno akiwa eneo lake la ufundi, akipinga maamuzi aliyoyaona kuwa hayakuwa ya haki.
Kwa sasa, Pochettino anasubiri huenda apokee tena msamaha kutoka kwa mamlaka husika, lakini kwa mtazamo wa uchambuzi huu, kila tukio kama hilo linaendelea kuimarisha mazingira ya kikosi chake kujiona kuwa kinapambana na dunia nzima.
AWALINDA WACHEZAJI WAKE
Kinachovutia zaidi katika mbinu za Pochettino ni namna anavyowalinda wachezaji wake hata pale wanapofanya makosa makubwa.
Katika mchezo wa Lisbon, kipa Senne Lammens alifanya makosa mawili yaliyosababisha madhara kwa timu, lakini badala ya kumshambulia hadharani, Pochettino alimfariji uwanjani na kumtetea mbele ya waandishi wa habari.
Hali hiyo imekuwa tofauti na namna ambavyo makosa ya baadhi ya wachezaji yalivyokuwa yakichukuliwa kama sehemu ya lawama kwa timu nzima.
Beki Noussair Mazraoui pia alionekana kufanya makosa ya upangaji wa nafasi wakati wa bao la kwanza la Sporting, sawa na yaliyofanywa na Matthijs de Ligt katika mchezo dhidi ya Liverpool.
Licha ya makosa hayo na United kumaliza michezo miwili mfululizo ikiwa na wachezaji 10, Pochettino ameendelea kuonyesha mshikamano na kikosi chake.
Wachezaji sasa wanaonekana kuwa na kocha anayewapa nguvu na anayesimama nao wakati wa changamoto, jambo linaloweza kusaidia kurejesha imani iliyokuwa imeanza kupotea.
FERGUSON ALITUMIA MBINU HIYO
Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Ryan Giggs, aliwahi kueleza mwaka 2022 namna Ferguson alivyokuwa akiwajenga kisaikolojia wachezaji wake kwa kuwafanya waamini kuwa kila mtu alikuwa akitaka waishindwe.
Giggs amesema: “Alitushawishi kuwa Manchester United ndiyo timu ambayo kila mtu anapenda kuichukia. Alitufanya tuhisi kwamba kila mtu anataka tumalize nafasi ya pili na kwamba ni sisi dhidi ya dunia nzima.”
Ameongeza kuwa Ferguson alikuwa akitengeneza mazingira ya changamoto ambayo wachezaji walitakiwa kuyakubali na kupambana nayo.
Sasa Pochettino anaonekana kuanza kutumia mbinu kama hiyo, akisimama mbele ya wachezaji wake na kuibeba timu katika nyakati ngumu.
Ingawa bado kuna maswali kuhusu uwezo wake wa kurejesha makali ya Manchester United, dalili za falsafa mpya zimeanza kuonekana.
Na wakati Ferguson akitazama maendeleo ya mwanafunzi wake huyo kutoka jukwaani, huenda anafurahishwa kuona baadhi ya mbinu zilizompa mafanikio Old Trafford zikianza kutumika tena.