Pochettino aicharukia VAR
Muktasari:
- Kauli hiyo imekuja baada ya Chama cha Soka England (FA) kubatilisha kadi nyekundu aliyoonyeshwa beki wa United, Leny Yoro, katika mchezo ambao timu hiyo ilifungwa mabao 4-0 na Liverpool Jumapili iliyopita.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Mauricio Pochettino ameikosoa vikali mifumo ya teknolojia ya usaidizi wa marefa (VAR) katika Ligi Kuu England, akieleza kuwa haifanyi kazi ipasavyo licha ya uwepo wa teknolojia hiyo kusaidia kupunguza makosa ya waamuzi.
Kauli hiyo imekuja baada ya Chama cha Soka England (FA) kubatilisha kadi nyekundu aliyoonyeshwa beki wa United, Leny Yoro, katika mchezo ambao timu hiyo ilifungwa mabao 4-0 na Liverpool Jumapili iliyopita.
Licha ya United kushinda rufaa yake ya kupinga adhabu hiyo, Pochettino hakufurahishwa na maelezo ya mkuu wa ProRef, Howard Webb, aliyemuunga mkono mwamuzi Sam Barrott kwa uamuzi wa kumtoa nje Yoro.
Pochettino, ambaye alishuhudia kikosi chake kikifungwa vibaya na Liverpool katika mchezo wake wa kwanza akiwa kocha wa United, baada ya Yoro kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya nane, alisema haikubaliki hali kama hiyo kutokea wakati VAR ipo.
“Nimevunjika moyo sana kwa sababu naamini jambo kama hili halipaswi kutokea. Tunaweza kukubali kuwa mwamuzi anaweza kufanya kosa kutokana na hisia na namna anavyouona mchezo. Wakati mwingine mtazamo au nafasi aliyokuwepo inaweza kuathiri uamuzi wake.
“Lakini kama tuna VAR, walikuwa wanafanya nini? Je, tutarudia mchezo? Je, tutapata nafasi ya kucheza tena tukiwa na vifaa na mazingira sawa, timu zote zikiwa na wachezaji 11 dhidi ya 11? Hapana,” .
Kocha huyo alisisitiza kuwa ni muhimu mamlaka husika kutafakari upya namna mfumo huo unavyotumika ili kuhakikisha teknolojia inatimiza kusudi lake.
“Ni lazima tutenge muda wa kupitia upya tukio hilo. Tuna gari la kiwango cha juu sana, lakini tunahitaji watu wenye uwezo wa kuliendesha vizuri. Tunapenda teknolojia, tunakubali ipo, lakini swali ni je, wanaitumiaje?” .
Katika tukio lililoibua mjadala huo, Yoro alionyeshwa kadi nyekundu wakati matokeo yakiwa 0-0 baada ya kumchezea vibaya mshambuliaji wa Liverpool, Alexander Isak.
Hata hivyo, kulikuwa na utata kuhusu tukio hilo kwa kuwa Isak alikuwa amegusa mpira kwa uzito kabla ya kuangushwa na haikuwa wazi kama angeweza kuufikia mpira huo kabla ya kipa wa United, Senne Lammens.
Akizungumza katika kipindi chake cha Mic’d Up, Webb alieleza kuwa Barrott alifanya uamuzi sahihi wa kumwonyesha Yoro kadi nyekundu.
Kauli hiyo imewakera viongozi wa United, ambao wanatarajia kuwasilisha malalamiko yao moja kwa moja kwa Ligi Kuu England na ProRef kuhusu maelezo hayo.