Jumba bovu! Fernandes amgeuka Carrick
Muktasari:
- Kiungo Fernandes ambaye anafahamika kwa kupenda soka kwa dhati na kufuatilia kwa karibu masuala ya kiufundi, hakuficha kutoridhishwa kwake na mbinu zilizotumiwa na Carrick katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
ROMA, ITALIA: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes amemkosoa kocha wake Michael Carrick kuhusu mbinu za mchezo baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 4-1 na Como katika kipigo kilichoibua maswali kuhusu mustakabali wa kocha huyo, huku United ikifikisha mechi saba bila ushindi.
Kiungo Fernandes ambaye anafahamika kwa kupenda soka kwa dhati na kufuatilia kwa karibu masuala ya kiufundi, hakuficha kutoridhishwa kwake na mbinu zilizotumiwa na Carrick katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza na TNT Sports baada ya kipigo hicho, nahodha huyo amesema uamuzi wa benchi la ufundi kutowataka wachezaji kuwabana wapinzani mmoja mmoja uliipa Como nafasi ya kucheza kwa uhuru na kupata ujasiri zaidi.
"Ni uamuzi wa benchi la ufundi kutowataka wachezaji kuwabana wapinzani mmoja mmoja, wakati mwingine kuacha nafasi nyuma na kujaribu kuipata mipira. Lakini unapoiruhusu timu kama hizi kumiliki mpira kwa muda mrefu, zinapata ujasiri," amesema Fernandes.
Alipoulizwa moja kwa moja kama Carrick alikosea mbinu, Fernandes alijibu: "Hilo ni jukumu la kocha na benchi lake la ufundi kulitathmini, si langu. Wakati mwingine unatakiwa kuwa jasiri zaidi unaposhambuliwa, kuchukua hatari ya kuwabana wapinzani juu na kuwafanya washindwe kucheza kwa utulivu."
Kauli hiyo iliongeza presha kwa Carrick, ambaye alikabiliwa na maswali kuhusu mustakabali wake baada ya kipigo hicho. Akijibu kauli za nahodha wake katika mkutano na waandishi wa habari, kocha huyo alisisitiza kuwa mbinu pekee haziwezi kuisaidia timu ikiwa wachezaji hawajitumi.
"Unaweza kutumia mfumo wowote au mbinu zozote, lakini kama hukimbii, husongi mbele wala kurudi nyuma, huwezi kushinda," amesema Carrick.
Kocha huyo pia aliomba radhi kwa mashabiki 700 waliosafiri kuishuhudia timu yao ikicheza, akieleza kuwa kiwango kilichoonyeshwa hakikukubalika kwa klabu yenye historia na hadhi ya Manchester United.
Carrick alieleza kuwa aliguswa na namna timu ilivyocheza na aliona ni muhimu kuwafuata mashabiki baada ya filimbi ya mwisho ili kuwapa pole na kuonyesha kuwa alielewa maumivu yao.
"Ninapaswa kuwaomba radhi mashabiki. Ninaipenda klabu hii kama mtu mwingine yeyote, kama si zaidi, kutokana na nafasi niliyonayo na thamani ninayoipa klabu hii. Kucheza kwa namna ile hakukubaliki," amesema.
Ameongeza kuwa alitaka mashabiki wajue kuwa alishiriki hisia zao, akisisitiza kuwa ingawa timu inaweza kushinda au kupoteza, namna inavyopambana na kuwakilisha klabu ni jambo muhimu.
Carrick alikataa kuzungumzia nafasi yake ya kazi, akisema hakuwaza kuhusu mustakabali wake wakati huo, bali alielekeza fikra zake kwa mashabiki na namna timu ilivyoshindwa kutimiza matarajio yao.
Hali hiyo inafanana kwa kiasi na yaliyompata Ole Gunnar Solskjaer mwaka 2021, baada ya Manchester United kufungwa mabao 4-1 na Watford, matokeo yaliyochangia kutimuliwa kwake siku iliyofuata. Baada ya kipigo cha Como, Carrick pia alionekana kukerwa, akiwafuata mashabiki huku akiinua mikono yake mara kadhaa kuonyesha masikitiko.
United sasa imefikisha mechi saba mfululizo bila ushindi, mwenendo wake mbaya zaidi tangu ilipocheza mechi nane bila kushinda chini ya Louis van Gaal kati ya Novemba 25 na Desemba 28, 2015.
Baada ya kushinda mechi 12 kati ya 17 alizoiongoza msimu uliopita na kuisaidia timu kurejea Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukosekana kwa miaka miwili, Carrick alipewa mkataba wa miaka miwili. Hata hivyo, mwanzo wa msimu huu umekuwa mgumu na United imejikuta katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ikiwa na pointi tatu tu zaidi ya Sunderland inayoshika mkia.
United ilipoteza mchezo wake wa kwanza wa ligi dhidi ya Hull, timu iliyopanda daraja, lakini ikajibu kwa kuifunga Ipswich wiki iliyofuata. Tangu ushindi huo, hata hivyo, haijaibuka na ushindi mwingine katika ligi. Ushindi wake mwingine pekee katika mechi 11 za mashindano yote ulikuwa dhidi ya Sabah FK ya Azerbaijan katika Ligi ya Mabingwa.
Katika mchezo dhidi ya Como, mshambuliaji Joshua Zirkzee alifunga bao la kufutia machozi katika dakika za nyongeza, akiiokoa United dhidi ya kupata moja ya vipigo vikubwa zaidi katika historia yake ya mashindano ya Ulaya.
Aibu hiyo iliongezeka kutokana na tofauti ya historia ya timu hizo. Manchester United ilipotwaa taji lake la mwisho la mabingwa wa Ulaya mwaka 2008, Como ilikuwa ikicheza katika Ligi ya Daraja la Nne nchini Italia.
Nyota wa Como, Nico Paz, alikuwa mwiba kwa United baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya pili, kuandaa bao la pili na baadaye kuongeza bao lake la pili katika mchezo huo. Kiwango chake kimeonyesha tofauti ya ubora kati ya timu hizo usiku huo, huku akionekana kuwa mchezaji ambaye angevutia klabu kubwa za Ulaya iwapo angepatikana sokoni.
United sasa inajiandaa kuikaribisha Bournemouth Jumapili katika Ligi Kuu England, ikiwa na kumbukumbu zisizofurahisha wakikutano hivi karibuni dhidi ya wapinzani hao. Kabla ya sare ya mabao 4-4 msimu uliopita, Bournemouth ilikuwa imeshinda mechi zake mbili zilizotangulia ugenini dhidi ya United kwa mabao 3-0 kila moja.
Wakati huo huo, mashabiki wa United walionyesha hasira zao kwa wamiliki wa klabu, familia ya Glazer, pamoja na Sir Jim Ratcliffe, kadiri usiku huo wa aibu ulivyoendelea.
Baadhi ya wachambuzi wameelekeza sehemu ya lawama kwa uongozi wa klabu, wakidai Carrick hakupata usaidizi wa kutosha katika usajili wa majira ya kiangazi.
United ilisajili viungo watatu, lakini haikuongeza ushindani wa kutosha katika nafasi ya beki wa kushoto inayochezwa na Luke Shaw na mshambuliaji Benjamin Sesko.
Mkurugenzi wa michezo, Jason Wilcox, naye ametetewa na baadhi ya watu kwa hoja kwamba alilazimika kufanya kazi ndani ya bajeti iliyopangwa na viongozi wa juu wa klabu, akiwamo mtendaji mkuu Omar Berrada.
Carrick, ambaye aliwahi kutwaa mataji matano ya Ligi Kuu England na taji la Ligi ya Mabingwa akiwa mchezaji wa United, alikiri kuwa ilikuwa vigumu kutazama kiwango cha timu yake.
"Nilikuwa na mambo mengi kichwani nilipokuwa nikitazama mchezo ule. Ilikuwa vigumu kuutazama. Si mabao tu, bali pia namna tulivyocheza katika vipindi fulani," amesema.
Alisisitiza kuwa anajitolea kwa kiwango cha juu kwa ajili ya klabu hiyo, akieleza kuwa maisha yake yote yanahusishwa na Manchester United, ingawa anakiri kuwa juhudi zake zinaweza zisiendane na matokeo yanayotakiwa.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa katika uamuzi wa uongozi wa United kuhusu Carrick kabla ya mchezo dhidi ya Bournemouth, huku kocha huyo akikabiliwa na shinikizo kubwa la kurejesha ushindani, matokeo na imani ya mashabiki.