Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Joshua aanika sababu za kukataa ‘Face-Off’ na Fury

MASUMBWI Pict

Muktasari:

  • Katika pambano hilo lililofanyika London, Fury aliibuka na ushindi kwa pointi dhidi ya Makhmudov, akionyesha ubabe wake na kurejea kwa nguvu katika ulingo.

LONDON, ENGLAND: MVUTANO wa muda mrefu kati ya mabondia wakubwa wa Uingereza, Anthony Joshua na Tyson Fury, umeingia sura mpya baada ya Joshua kueleza sababu zilizochochea kukataa kuzichapa na mpinzani wake huyo mara baada ya pambano la Fury dhidi ya Arslanbek Makhmudov.

Kauli hiyo imechochea mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa ndondi duniani kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa pambano la mafahari hao.

Katika pambano hilo lililofanyika London, Fury aliibuka na ushindi kwa pointi dhidi ya Makhmudov, akionyesha ubabe wake na kurejea kwa nguvu katika ulingo.

Mara baada ya ushindi huo, Fury alielekea moja kwa moja upande alipokuwa ameketi Joshua, akiwa na lengo la kumlazimisha kukubaliana hadharani kuhusu pambano lao linalotarajiwa kuwa la kihistoria.

Hata hivyo, tofauti na matarajio ya mashabiki wengi waliokuwa wamejaa ulingoni na wale waliokuwa wakifuatilia kwenye vyombo vya habari, Joshua alikataa kuingia ulingoni au kushiriki katika “face-off” ya moja kwa moja na Fury.

Badala yake, wawili hao walijibizana kwa maneno kutoka pande mbili tofauti za kamba za ulingo, hali iliyoongeza mvutano na kuibua maswali mengi kuhusu kama pambano hilo limekaribia au bado lipo mbali.

Baadaye, Joshua alifafanua kuwa uamuzi wake haukuwa wa dharau, bali ulikuwa ni msimamo wa kimkakati na wa kimaamuzi binafsi. Alisisitiza hakutaka kushiriki katika “shughuli za kibiashara za matangazo” ambazo hazina makubaliano rasmi ya kisheria kuhusu pambano hilo.

Joshua alisema wazi bado hakuna mkataba uliosainiwa unaomlazimisha kupigana na Fury na hivyo hakuwa tayari kuingia katika presha ya mvutano wa hadharani ambao unaweza kuleta mkanganyiko katika kazi yake ya ndondi.

MASU 06

“MIMI SIKIMBILII UMAARUFU”

Katika maelezo yake, Joshua ameonyesha kuwa na msimamo mkali akijibu kile alichokiita “kelele na presha za mitandao na vyombo vya habari”. Alisisitiza maisha yake ya mchezo yamejengwa juu ya nidhamu, muda na mipango ya kitaalamu, si matukio ya kuigiza mbele ya kamera bila makubaliano rasmi.

Kauli yake ilionekana kuwa ujumbe wa moja kwa moja kwa Fury na upande wake wa matangazo.

Joshua alieleza amekuwa kwenye mchezo wa ngumi kwa zaidi ya miaka 13 na katika kipindi chote hicho hajawahi kukimbia pambano lolote lililokubaliwa rasmi. Alisema tofauti na watu wanaopenda kuacha na kurudi mara kwa mara, yeye amebaki imara na amejenga jina lake kwa kupigana na wapinzani wakubwa duniani bila kuchagua njia rahisi.

Aliongeza haoni sababu ya kushiriki katika “hype” au mikakati ya kujitangaza ambayo haina msingi wa kisheria. Kwa mtazamo wake, kila pambano lazima lipitie mchakato sahihi wa mikataba kabla ya kuanza kujadiliwa hadharani au kuonyeshwa kama limekamilika.

Joshua pia alisisitiza hana tatizo la kupigana na Fury, lakini anataka kila kitu kifanyike kwa utaratibu sahihi. Alisema katika ngazi ya juu ya ndondi, heshima ya mikataba na maamuzi rasmi ni muhimu zaidi kuliko presha ya mashabiki au matukio ya ghafla ya ulingoni.

MASU 01
MASU 01

FURY ANALITAKA PAMBANO

Kwa upande wake, Fury ameendelea kuwa na msimamo kuhusu pambano hilo, akisisitiza yeye yuko tayari wakati wowote. Baada ya ushindi wake dhidi ya Makhmudov, Fury alionekana kutumia muda mwingi kuzungumzia Joshua, akidai pambano hilo linapaswa kufanyika bila kuchelewa zaidi.

Fury alidai ameshasaini makubaliano ya mapambano na kilichobaki ni Joshua kukubali rasmi. Kauli yake imeongeza presha kubwa kwa upande wa Joshua, hasa kutokana na ukweli mashabiki wengi sasa wanaona kama Fury ndiye anayelitaka zaidi pambano hilo lifanyike.

Alisisitiza mashabiki wa ndondi wamechoka kusubiri kwa zaidi ya miaka mitano bila kuona pambano hilo likitimia. Kwa mtazamo wake, kila linapochelewa zaidi kunapunguza ladha ya pambano hilo ambalo tayari limejijengea historia kabla hata halijafanyika.

Fury pia alieleza alishangazwa na uamuzi wa Joshua kutokubali kuingia ulingoni mara baada ya pambano. Alisema alitarajia kuona 'face-off' ya moja kwa moja ambayo ingeweka msingi wa makubaliano ya haraka.

MASU 02

MASHARTI, CHANGAMOTO ZA MPAMBANO

Licha ya hamasa kubwa ya mashabiki, bado kuna changamoto kadhaa zinazoendelea kuzuia pambano hilo kufanyika kwa haraka. Joshua ameeleza bado yuko katika hatua ya kurejea kikamilifu ulingoni baada ya kipindi kigumu cha maisha binafsi na mapumziko ya muda mrefu.

Pia, kuna taarifa Joshua anapanga kufanya pambano la maandalizi kabla ya kukutana na Fury. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha anarudi katika kiwango chake cha ushindani kabla ya kukabiliana na mpinzani wa kiwango cha juu kama Fury.

Kwa upande mwingine, timu ya Fury inaonekana tayari zaidi kwa pambano la haraka. Wanaamini kuchelewa kunaweza kuathiri mvuto wa kibiashara na hadhi ya pambano hilo ambalo tayari lina thamani kubwa sokoni.

Wataalamu wa ndondi wanasema kuwa tofauti ya maandalizi kati ya pande hizi mbili inaweza kuwa moja ya sababu kubwa za kuchelewesha makubaliano ya mwisho.

MASU 03

MTAZAMO WA WACHAMBUZI WA NGUMI

Wachambuzi wa ndondi duniani wameendelea kutoa maoni tofauti kuhusu mustakabali wa pambano kati ya Joshua na Fury, wakisisitiza licha ya changamoto zilizopo, pambano hilo bado lina uzito mkubwa wa kibiashara na kimichezo duniani.

Mchambuzi wa ndondi wa Sky Sports, Ben Davies, amesema pambano hilo linaendelea kuwa moja ya “ndoto kubwa zaidi katika historia ya ndondi za kisasa,” akieleza kuwa hata kama mabondia wote wawili wamepoteza ubingwa wa dunia kwa Oleksandr Usyk, bado majina yao yana nguvu kubwa ya kuvutia mashabiki na wawekezaji duniani.

Davies anaongeza: “Hata kama hawako kileleni kama zamani, Fury na Joshua bado ni majina yanayoweza kuuza uwanja mzima ndani ya dakika chache. Hilo pekee linaonyesha ukubwa wa pambano lao.”

Aidha, mchambuzi wa zamani wa ndondi na mwandishi wa masuala ya michezo Cam Hogwood (Sky Sports) ameongeza kuwa mvutano wa wawili hao umekuwa ukijengwa zaidi na historia yao ndefu ya mazungumzo yasiyokamilika kuliko hata tukio la sasa ulingoni.

Hogwood anaeleza kuwa: “Hii si mara ya kwanza kwa dunia kuona Fury na Joshua karibu kukubaliana, lakini kila mara kitu hukwama. Hicho ndicho kinachofanya pambano hili kuwa na uzito wa kihistoria zaidi kila linapochelewa.”

MASU 04

HISTORIA YA MVUTANO WAO

Mvutano kati ya Fury na Joshua una historia ndefu ya mazungumzo yasiyokamilika. Mara kadhaa mazungumzo yamefikia hatua za mwisho lakini yakavunjika kutokana na masuala ya mikataba, ratiba na migogoro ya ubingwa.

Mwaka 2021, pambano lao lilikuwa karibu sana kufanyika, lakini likavunjika kutokana na kesi ya mapambano mengine ya Fury. Tangu wakati huo, mashabiki wamekuwa wakisubiri bila mafanikio.

Kila mwaka jina lao limekuwa likirudi kwenye vichwa vya habari, lakini bila uthibitisho rasmi wa pambano.

MASU 05

SASA ITAKUWAJE

Kwa sasa, mustakabali wa pambano hilo bado haujathibitishwa rasmi. Ingawa kuna taarifa zisizo rasmi zinazopendekeza uwezekano wa kufanyika mwaka 2026, hakuna makubaliano ya mwisho yaliyosainiwa.

Wataalamu wanasema mazungumzo bado yanaendelea nyuma ya pazia, lakini kila upande una masharti yake, jambo linalochelewesha makubaliano ya mwisho.

Hii inaacha hali ya sintofahamu kwa mashabiki, ambao wanaendelea kusubiri tangazo rasmi kutoka kwa promota au timu za mabondia hao.

Kwa jumla, mvutano kati ya Joshua na Fury umeendelea kuwa moja ya hadithi kubwa zaidi katika dunia ya ndondi za kisasa. Wote wawili ni majina makubwa yenye ushawishi mkubwa na kila mmoja anaamini ana nafasi ya kushinda.

Hata hivyo, bila makubaliano rasmi, pambano hilo linaendelea kubaki ndoto inayosubiri kutimia. Mashabiki duniani kote wanaendelea kutumaini siku moja, hatimaye, “vita ya Uingereza” itafanyika na historia mpya itaandikwa.