Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi Arsenal itakavyoshinda ubingwa msimu huu

Muktasari:

  • Mara ya mwisho kwa Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England ilikuwa ni msimu wa 2003-04, ambao ilibeba taji bila ya kupoteza mechi hata moja

MSIMU uliopita, Arsenal ilikaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa siku 248, muda mrefu zaidi kwa timu ambayo ilishindwa kubeba taji.

Ikatibua kwenye mechi saba za mwisho, ambapo ilishinda mbili tu. Manchester City wao waliwasha moto kuanzia katikati ya Februari na kwenda kunyakua taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo na tano kwenye misimu sita ya mwisho. Msimu huu, Arsenal ipo tena kweye mbio za ubingwa huo wa Ligi Kuu England.

Msimamo unavyosoma, Arsenal inashika nafasi ya tatu ikivuna pointi 55, tano nyuma ya vinara Liverpool na moja nyuma ya Man City, huku Liverpool ikiwa imecheza mechi 26. Arsenal imecheza mechi 25. Kinachovutia, Arsenal inakwenda jino kwa jino na wapinzani wake kwenye mbio hizo za ubingwa, kwani imeshinda mechi 17 sawa na Man City, kabla ya Liverpool wao kuongeza ushindi wao wa 18 msimu huu baada ya kuichapa Luton 4-1, Jumatano. Imefunga mabao sawa na Man City, 58, ikizidiwa mabao matano tu na Liverpool kwenye kufunga. Kitu kizuri, Arsenal ina wastani mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, +36, wakizidiwa na Liverpool tu yenye +38 na Man City yenyewe ina +32. Arsenal imetoka sare nne, Man City sare tano na Liverpool sare sita. Tofauti ipo kwenye mechi za kupoteza, Arsenal imepoteza nne, Man City tatu na Liverpool mbili.

Kingine kizuri kuhusu Arsenal ni kwamba haina unyonge inapocheza dhidi ya wapinzani wake kwenye mbio hizo za ubingwa. Imeshamalizana kwenye mechi zote mbili na Liverpool, ile ya kwanza iliyofanyika Anfield ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, kabla ya kwenda kuishushia kipigo cha 3-1 uwanjani Emirates.

Ilipokutana na Man City kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Oktoba mwaka jana uwanjani Emirates, mabingwa watetezi walikubali kichapo cha bao 1-0. Marudio yatakuwa Machi 31 uwanjani Etihad. Arsenal ikiokota matokeo chanya kwenye mechi hiyo ya Etihad, basi uhakika wa ubingwa utakuwa mkubwa. Rekodi zao zinaonyesha, Arsenal ya sasa inaweza kucheza na wababe wenzake. Ilipokutana na Chelsea mchezo wa kwanza Stamford Bridge ulimalizika kwa matokeo ya 2-2, wakati ilipokipiga na Man United kwenye raundi ya kwanza, wababe hao wa Old Trafford, walikwenda kukutana na kipigo cha mabao 3-1 uwanjani Emirates.

Timu nne ambazo zimefanikiwa kuichapa Arsenal msimu huu ni Newcastle United (1-0), Aston Villa (1-0), Fulham (2-1) na West Ham United (2-0).

Kwenye orodha hiyo hakuna timu hata moja ya Big Six. Hii ina maana, Arsenal imeshavuka kwenye hatua ya kuteswa na wababe wa Big Six kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kitu pekee ambacho Arsenal inapaswa kufanya ni kuwa siriazi kwenye mechi za timu za kawaida na kuzoa pointi, ambazo ndizo hasa zimekuwa eneo analozidiwa na timu wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa.

Liverpool na Man City zimekuwa zikizoa pointi za kutosha zinapokutana na timu za kawaida. Arsenal ikipawezea huko, ikizoa pointi kwenye mechi za kawaida hakuna kitu ambacho kitaizuia kutimiza ndoto za kubeba taji la Ligi Kuu England msimu huu.

Kocha Mikel Arteta amewaambia wachezaji wake, wanahitaji kuvuna pointi kati ya 96 na 100 kubeba ubingwa huo wa Ligi Kuu England msimu huu. Kwa sasa Arsenal ina pointi 55 baada ya mechi 25.

Kufikia pointi 96, Arsenal bado inadaiwa pointi 41. Kwa kucheza mechi 25, ina maana hadi msimu ufike mwisho, Arsenal bado ina mechi 13 za kucheza, sawa na pointi 39. Kitu ambacho Arsenal inapaswa kufanya, isiangushe pointi kwenye mechi zake zote zilizobaki. Kushinda Etihad kutawapa nguvu zaidi, kwa sababu hata kama Man City nayo itakuwa imeshinda mechi zake, matokeo hayo yatamfanya Arteta ampiku mwalimu wake Pep Guardiola kwenye msimamo. Mechi nyingine ngumu kwa Arsenal ni zile itakazocheza na Brighton, Man United, Aston Villa na Tottenham Hotspur, kwa sababu zenyewe zitakuwa zinasaka tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Spurs itakuwa nyumbani, Man United itakuwa nyumbani na Brighton pia itakuwa nyumbani, hapo Arteta atahitaji akili ya ziada kwenda kuchukua pointi hizo muhimu ugenini.

Kuhusu Liverpool uzuri ni kwamba yenyewe pia bado haijamalizana na Man City, hivyo watachoshana wenyewe, huku watakuwa na mechi pia dhidi ya Man United, Spurs, Aston Villa, Everton, West Ham na Brighton. Jurgen Klopp naye ana shughuli pevu kwenye kuigomea Arsenal isibebe taji la msimu huu.

Mechi tano zijazo za Arsenal ndizo zitakazoamua hatima ya ubingwa wao. Itakuwa nyumbani kucheza na Newcastle, Brentford na Chelsea, huku itakuwa ugenini kucheza na Sheffield United na Man City. Arsenal haipaswi kuangusha zaidi ya pointi mbili katika mechi hizo. Wakitoboa hapo, Arsenal itafanikiwa kupenya kwenye msako wao wa taji la ubingwa wa Ligi Kuu England.


MECHI ZA UBINGWA ARSENAL

-Februari 24 vs Newcastle (nyumbani)

-Machi 4 vs Sheffield Utd (ugenini)

-Machi 9 vs Brentford (nyumbani)

-Machi 16 vs Chelsea (nyumbani)

-Machi 31 vs Man City (ugenini)

-Aprili 2 vs Luton Town (nyumbani)

-Aprili 6 vs Brighton (ugenini)

-Aprili 13 vs Aston Villa (nyumbani)

-Aprili 20 vs Wolves (ugenini)

-Aprili 27 vs Tottenham (ugenini)

-Mei 4 vs Bournemouth (nyumbani)

-Mei 11 vs Man United (ugenini)

-Mei 19 vs Everton (nyumbani)