Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jezi ya Groat Lowry kustaafishwa Januari

Muktasari:

  • Lowry, ambaye ni All-Star mara sita, pia ndiye kinara wa muda wote wa Raptors katika vipengele vya asisti, kupora mipira na mitupo ya three-point.

TORONTO, CANADA: TORONTO Raptors imetangaza kuwa jezi namba 7 iliyokuwa inavaliwa na supastaa Kyle Lowry itapandishwa juu ya paa la Scotiabank Arena katika sherehe maalumu baada ya mchezo wa Jumapili, Januari 10, 2027 wakati Raptors watakapokuwa wenyeji wa Philadelphia 76ers.

Lowry, ambaye ni All-Star mara sita, pia ndiye kinara wa muda wote wa Raptors katika vipengele vya asisti, kupora mipira na mitupo ya three-point.

Mchezaji huyo mzaliwa wa Philadelphia, Marekani ambaye baadaye alikuja kuwa sura ya kipindi chenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Toronto Raptors, aliisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa NBA 2019 na kujihakikishia nafasi ya kuwa GROAT (Greatest Raptor of All Time), yaani mchezaji bora zaidi kuwahi kuichezea timu hiyo.

Lowry alianzia maisha yake ya kikapu katika kikosi cha Memphis Grizzlies 2006 alikodumu hadi 2009 kisha akatimkia Houston Rockets kati ya 2009 hadi 2012 kabla ya kuua Toronto Raptors alikofanya balaa kuanzia 2012 hadi 2021. Kuanzia 2021 hadi 2024 alicheza Miami Heat kabla ya kukipiga Philadelphia 76ers kati ya 2024 hadi 2026 alipotangaza kustaafu kucheza.

Nyota huyo atakuwa mchezaji wa pili katika historia ya Raptors kustaafisha jezi yake, akimfuata Vince Carter ambaye jezi yake namba 15 ilistaafishwa Novemba 2, 2024. “Nimekuwa nikisubiri wakati huu kwa miaka mingi. Kila mara nilisema Toronto ni nyumbani kwangu na kwamba nitastaafu nikiwa Raptor. Kuiona jezi yangu namba 7 ikipelekwa juu katika jengo hilo kutamaanisha kila kitu kwangu,” alisema Lowry wiki hii.

“Tulijenga kitu cha kipekee hapa, mimi na wachezaji wenzangu, uongozi wa klabu, jiji, mashabiki na Canada nzima. Tulikuwa mabingwa pamoja, hivyo kuweza kushiriki usiku huu (siku ya kustaafisha jezi hiyo) na wote pamoja na familia yangu kutamaanisha mengi kwangu.”

Mashabiki wa Raptors watakuwa sehemu ya sherehe hizo, huku kukiwa na Usiku wa GROAT utakaowapa nafasi zaidi ya kukumbuka baadhi ya matukio yaliyomfanya Lowry kuwa mmoja wa wachezaji waliopendwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.

Sherehe hizo zitaanza Januari 7, wakati Raptors watakapocheza dhidi ya Minnesota Timberwolves, na kuendelea Januari 8 dhidi ya Utah Jazz. Michezo yote miwili itaanza saa 7:30 usiku kwa saa za Marekani.

Mashabiki watakaohudhuria Januari 7 watapewa fulana maalumu ya kumbukumbu, wakati wale watakaohudhuria Januari 8 watapata sanamu ndogo ya kumbukumbu yenye kichwa kinachotingishika ya Kyle Lowry. Pia kutakuwa na zawadi nyingine za kipekee katika usiku huo.

Mambo yote yatafikia kilele Januari 10, wakati mashabiki watakapoungana na Lowry, familia, wachezaji wenzake wa zamani na viongozi wa Raptors kushuhudia jezi namba 7 ikipandishwa juu ya paa la Scotiabank Arena. Katika kuadhimisha hilo, Lowry na Raptors watampa shabiki mmoja mwenye bahati nafasi ya kushuhudia wiki hiyo ya kihistoria kwa kushinda tiketi mbili za michezo yote mitatu ya Usiku wa GROAT.

Maelezo ya shindano hilo yatatangazwa kupitia mitandao ya kijamii ya Raptors na tovuti rasmi ya klabu hiyo katika siku zijazo.

Jezi ya Lowry itaning’inia sambamba na bango la ubingwa alilosaidia kulileta jijini Toronto baada ya kuitumikia Raptors kwa misimu tisa.

Katika misimu hiyo, alisaidia Raptors kufuzu hatua ya mtoano mara saba, kufika fainali za Kanda ya Mashariki mara mbili na hatimaye kutwaa ubingwa wa kwanza wa NBA 2019.