Conte aruka kimanga Man United
Muktasari:
- United ilichapwa mabao 4-1 na Como katika Ligi ya Mabingwa wiki hii, matokeo yaliyoendeleza mfululizo wa mechi saba bila ushindi. Carrick hajashinda tangu alipoiwezesha timu hiyo kuifunga Ipswich Town mabao 5-2 mwezi Agosti, huku mechi zijazo dhidi ya Bournemouth na Chelsea zikitarajiwa kuwa muhimu kwa hatima yake.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Antonio Conte amekanusha taarifa zinazomhusisha na Manchester United, akisema atachukua muda kutafakari kabla ya kuamua lini na wapi atarejea katika ukocha.
Kocha huyo raia wa Italia ametajwa kuwa miongoni mwa wanaoweza kurithi mikoba ya Michael Carrick, anayekabiliwa na presha kutokana na matokeo mabaya ya Manchester United.
United ilichapwa mabao 4-1 na Como katika Ligi ya Mabingwa wiki hii, matokeo yaliyoendeleza mfululizo wa mechi saba bila ushindi. Carrick hajashinda tangu alipoiwezesha timu hiyo kuifunga Ipswich Town mabao 5-2 mwezi Agosti, huku mechi zijazo dhidi ya Bournemouth na Chelsea zikitarajiwa kuwa muhimu kwa hatima yake.
Conte, aliyewahi kuzifundisha Tottenham Hotspur na Chelsea, amekuwa miongoni mwa makocha wanaotajwa kupewa nafasi ya kuiongoza United endapo klabu hiyo itaamua kuachana na Carrick.
Hata hivyo, kocha huyo mwenye mafanikio katika Ligi Kuu England na Serie A amekanusha kuwa yuko karibu kujiunga na klabu yoyote, tangu alipoondoka Napoli mwezi Juni.
Katika taarifa yake, Conte alisema: “Kutokana na taarifa za hivi karibuni zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini Italia na nje ya nchi, nimeona ni muhimu kuweka wazi msimamo wangu.
“Jina langu limehusishwa na klabu nyingi, lakini kwa sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofikia hatua ya juu.
“Baada ya kipindi kizuri na chenye mafanikio nikiwa Napoli, nitachukua muda ninaouhitaji kutafakari namna na wakati wa kurejea katika ukocha.
“Itakuwa uamuzi nitakaoufanya kwa umakini, pale nitakapoamini kuwa mazingira yanafaa.”
Conte pia amekanusha taarifa kwamba tayari amekuwa akizitaka klabu zinazomhitaji kumpa mamlaka kamili ya kusimamia timu na kukidhi matakwa yake ya kifedha.
Amesema madai hayo hayana msingi, kwa kuwa hakuna mazungumzo rasmi yanayoendelea yanayoweza kutumika kufanya tathmini kuhusu matakwa yake.
Ameongeza kuwa endapo nafasi halisi itajitokeza, ndipo atakapokaa na uongozi wa klabu husika kujadili masharti ya makubaliano yanayoweza kukidhi mahitaji ya pande zote.