Jamie Carragher: Kupendeza kunambeba Amorim!
Muktasari:
- Kocha huyo Mreno, Amorim alitua Old Trafford kurithi mikoba ya Erik ten Hag, Novemba mwaka jana na Man United ilimaliza msimu namba 15 kwenye msimamo, nafasi ya chini zaidi kuwahi kushika kwenye historia yake katika Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: KWELI kuishi kwingi ni kuona mengi. Beki wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Jamie Carragher amesema Ruben Amorim anabebwa tu na mwonekano wake na ndiyo maana hajaonyeshwa mlango wa kutokea huko Manchester United.
Kocha huyo Mreno, Amorim alitua Old Trafford kurithi mikoba ya Erik ten Hag, Novemba mwaka jana na Man United ilimaliza msimu namba 15 kwenye msimamo, nafasi ya chini zaidi kuwahi kushika kwenye historia yake katika Ligi Kuu England.
Msimu huu hadi sasa inashika nafasi ya tisa baada ya mechi tatu, huku ushindi wake pekee ilioupata kwenye mechi hiyo ulichangiwa na penalti ya dakika za majeruhi ilipoichapa Burnley 3-2 uwanjani Old Trafford, Jumamosi iliyopita.
Wasiwasi zaidi uliibuka baada ya timu ya League Two, Grimsby Town kuitupa nje Man United kwenye Kombe la Ligi kwa mikwaju ya penalti 12-11 baada ya sare ya 2-2.
Jambo hilo liliweka kwenye mashaka makubwa kibarua cha Amorim, lakini kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 ameendelea kudunda tu licha ya majanga yote hayo.
Na kinachoelezwa ni kwamba kwa namna anavyojiweka mbele ya kamera ndicho kitu kinachookoa ajira yake kwa mujibu wa gwiji wa Ligi Kuu England, Carragher.
Carragher, akizungumza kwenye kipindi cha The Overlap Fan Debate, kinachorushwa na Sky Bet, alisema: “Kuna hisia kubwa inapozungumzwa Jose Mourinho kurudi kwenye soka la England na kwa sababu ni maarufu anakuja na mambo yake, lakini alikuwa ni mshindi.
“Siku zote tumekuwa tukimkumbuka Brian Clough, nilipokuwa mdogo alikuwa akizungumza sana kwa sababu alikuwa mshindi.
“Tatizo la Ruben Amorim ni kwamba ni mzunguzaji mzuri kwenye mikutano ya waandishi wa habari, lakini kwa sababu si mshindi watu wanachofikiria, ‘Oh, kaa kimya. Acha kuongea.’
“Lakini, kama angekuwa anashinda, sote tungeona hilo ni jambo zuri. Kama asingekuwa anajiweka vizuri kwenye mikutano ya waandishi wa habari na asingekuwa na sura nzuri, angepoteza kazi yake mapema sana. Ukitazama matokeo yake, huoni anaponaje.”
Amorim amekuwa akizungumzia kuhusu kikosi chake kinachopata shida uwanjani na aliwahi kusema “pengine hii ni timu mbovu zaidi katika historia ya Manchester United” Januari mwaka huu. Na baada ya kiwango kibovu dhidi ya Grimsby, Amorim alisema: “Wakati mwingine nawachukia wachezaji wangi na wakati mwingine nawapenda wachezaji wangu.”
Na gwiji wa Man United, Paul Scholes alisema: “Nafanana kabisa na Ruben Amorim. Ni mtu wa haki sana na siku zote amekuwa hivyo. Anazungumza kitu ambacho kila kocha amewahi kukifikiria kwa wakati fulani, lakini sidhani kama anaweza kusema hivyo hadharani.
“Kuna makocha wengi sana wenye uzoefu kwenye Ligi Kuu England ambao wangefikiria kama yeye, lakini wasingesema hilo. Maneno mabaya zaidi kwangu mimi ni yale aliyosema baada ya mechi ya Grimsby, aliposema kwamba wachezaji wamezungumza kwa sauti kubwa, nadhani ile ilikuwa mbaya sana kwa upande wake.”