Isak wa Liverpool ana balaa
Muktasari:
- Katika video hiyo ya dakika tisa ambayo iliwekwa katika chaneli ya YouTube ya Liverpool kabla ya kusambaa katka mitandao mbalimbali ya kijamii ilimwonyesha Isak akiwa anawasili mazoezini, kisha akaenda kubadilisha nguo na kuanza kufanya mazoezi ya viungo chini ya uangalizi maalum wa kocha.
LIVERPOOL, ENGLAND: BAADA ya kuachiwa kwa video ya siku ya mshambuliaji mpya wa Liverpool, Alexander Isak, akifanya mazoezi na timu, mashabiki wengi wamekoshwa na kile ambacho staa huyo amekionyesha kiasi cha baadhi yao kutaka timu hiyo iongeze pesa zaidi katika dau la kumnunua.
Katika video hiyo ya dakika tisa ambayo iliwekwa katika chaneli ya YouTube ya Liverpool kabla ya kusambaa katka mitandao mbalimbali ya kijamii ilimwonyesha Isak akiwa anawasili mazoezini, kisha akaenda kubadilisha nguo na kuanza kufanya mazoezi ya viungo chini ya uangalizi maalum wa kocha.
Baada ya mazoezi ya viungo, staa huyo wa kimataifa wa Sweden alienda kuungana na wachezaji wengine katika kiwanja kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kuchezea mpira wakianza na kukimbia kabla ya baadaye kufanya mazoezi mengine.
Baadhi ya mazoezi hayo ilikuwa ni kumpiga chenga beki na kwenda kufunga, zoezi ambalo mara zote Isak alifaulu, pia kulikuwa na muda ambao kocha aligawa makundi mawili na ikachezwa mechi kwa muda mfupi ambapo pia Isak alifunga.
Mbali ya suala la kufunga staa huyu pia alionekana akifanya uzuiaji mara kadhaa jambo lililozidi kuwakosha mashabiki waliokuwa wanaangalia video hiyo.
Shabiki mmoja aliandika: “Huenda tumemnunua kwa bei ndogo.”
Mwingine akasema: “Alexander Isak, mshambuliaji bora duniani, akikimbia kwenye kiwanja cha chetu za mazoezi akiwa amevaa viatu vya njano ang’avu vya F50. Hizi ndizo siku tulizokuwa tukisubiri,”
Shabiki mwingine aliongeza: “Fikiria Isak akicheza sambamba na Mohamed Salah, Florian Wirtz na Cody Gakpo.” Na mwingine akasisitiza: “Bado siwezi kuamini anacheza katika klabu yangu.”
Akizungumza akiwa kambini na timu ya taifa ya Sweden wiki hii, Isak alisema kuwa watu hawana picha kamili kuhusu kuondoka kwake na mgogoro uliokuwa unaendelea dhidi ya Newcastle.
“Si kila mtu anajua kilichotokea ndani, hii ni sehemu ya soka. Siwezi kudhibiti kila kitu kinachoandikwa au kusemwa, lakini nina furaha kuwa mchezaji wa Liverpool. Hilo ndilo nililotaka na ninafurahi kwa hilo.
“Kuna mengi ya kujadili, na yanaweza kujadiliwa kwa muda mrefu. Imekuwa kama somo, na ninafurahia kilichotokea mwishoni. Nimefurahi na najivunia kuwa mchezaji wa Liverpool. Sitaki kuingia kwa undani sana kuhusu nini kilitokea, ni ukurasa uliofungwa tayari na binafsi sijawahi kuwa na tatizo na mtu yeyote.”
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden alikamilisha uhamisho wa Pauni 125 milioni akitokea Newcastle na kutua Anfield siku ya mwisho ya dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, ambapo alitangazwa rasmi kama mchezaji mpya wa majogoo hao.
Uhamisho wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 umevunja rekodi ya usajili nchini England, lakini ulijaa utata kwa sababu Newcastle ilionekana kutokuwa tayari kumuuza.
Isak alilazimika kugoma kuichezea klabu hiyo ili kulazimisha uhamisho wake, akidiriki kukosa ziara ya maandalizi ya msimu mpya na hakucheza mechi za wiki mbili za mwanzo katika Ligi Kuu England.
Mshambuliaji huyo mpya wa Liverpool anatarajiwa kuichezea timu hiyo inayonolewa na Arne Slot kwa mara ya kwanza Jumapili dhidi ya Burnley, iliyopanda daraja msimu huu.