Infantino aomba radhi FIFA
Muktasari:
- Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa Chama cha Soka England (FA), Debbie Hewitt, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa FIFA, baada ya kikao cha Baraza hilo kilichofanyika mjini Zurich, Uswisi, Alhamisi, kikiwa cha kwanza tangu kuibuka kwa taarifa kuhusu mpango wa siri wa uwekezaji uliopewa jina la FIFA Forward Enterprise (FFE).
ZURICH, USWISI: RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameomba radhi kwa Baraza la FIFA kufuatia utata ulioibuka kuhusu mpango wake wa kuuza sehemu ya haki za kibiashara za taasisi hiyo, lakini ameonywa kuwa bado hawezi kuaminiwa kuendelea kuongoza bila kuweka wazi nyaraka na kujibu maswali yanayohitaji ufafanuzi.
Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa Chama cha Soka England (FA), Debbie Hewitt, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa FIFA, baada ya kikao cha Baraza hilo kilichofanyika mjini Zurich, Uswisi, Alhamisi, kikiwa cha kwanza tangu kuibuka kwa taarifa kuhusu mpango wa siri wa uwekezaji uliopewa jina la FIFA Forward Enterprise (FFE).
Mpango huo, ambao Infantino aliusitisha ndani ya siku chache baada ya kuibuka kwa mjadala, ulilenga kutoa sehemu ya haki za kibiashara za FIFA kwa kampuni binafsi ya uwekezaji.
Katika kikao hicho kilichodumu kwa saa tatu na nusu, Infantino alikabiliwa na maswali kuhusu mpango huo, uamuzi wa kusitisha adhabu ya kadi nyekundu kwa mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, tuzo ya amani ya FIFA aliyopewa Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na namna fedha zinavyotolewa kwa vyama wanachama.
AOMBA RADHI
Baada ya kikao hicho, FIFA ilitoa video yenye maelezo ya Infantino, ambaye awali alikataa kuzungumza na waandishi wa habari.
Katika video hiyo, Infantino alikiri kuwepo kwa makosa katika namna suala la FFE lilivyowasilishwa na kujadiliwa, huku akisisitiza kuwa mpango huo haukuwa umefikia hatua ya makubaliano ya mwisho.
“Awali ya yote, ninaomba radhi kwa makosa yaliyofanyika katika mchakato wa mawasiliano na mashauriano kuhusu mradi wa FIFA Forward Enterprise, ambayo yalisababisha madhara mbalimbali,” alisema Infantino.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa FFE ilikuwa pendekezo tu na haikuwa imehitimishwa, akieleza kuwa lengo lake lilikuwa kuiwezesha FIFA kuongeza uwekezaji kwa vyama wanachama badala ya kuchukua nafasi ya misaada iliyokuwa ikitolewa kupitia vyanzo vya fedha vilivyopo.
Infantino alisema atajibu maswali yaliyowasilishwa kwa maandishi baadaye, akielezea kikao hicho kuwa kilikuwa cha kujenga licha ya kuwepo kwa mitazamo tofauti.
Lakini Hewitt amesema pamoja na kuomba radhi kwa Infantino, maswali muhimu yaliyowasilishwa na wajumbe hayakujibiwa.
“Jambo moja la kukatisha tamaa ni kwamba hatukupata majibu ya mambo tuliyokuwa tumeomba mahsusi, kwa mfano, kupata nyaraka za FFE,” alisema Hewitt.
Aliongeza kuwa alihoji sababu za nyaraka hizo kutowasilishwa, lakini wajumbe waliambiwa wawasilishe maswali yao kwa maandishi.
Kwa mujibu wa Hewitt, Infantino anatakiwa kujibu maswali hayo na kutoa nyaraka zinazohitajika ili wajumbe waweze kutathmini kilichotokea.
“Ni lazima mtu huyo ajibu maswali hayo. Asipoyajibu, basi hafai kuwa rais wa FIFA. Hilo ndilo lililosemwa katika kikao,” alisema.
UEFA HAIBADILI MSIMAMO
Hewitt amesema bado hajapokea nyaraka za FFE licha ya kuziomba mara kadhaa, akisisitiza kuwa majibu yatakayotolewa yataamua kama Infantino anaendelea kuaminika kuongoza taasisi hiyo.
Amesema pia ufafanuzi huo utasaidia kutathmini iwapo watu waliohusika katika mpango huo wanapaswa kuwajibishwa na kama kuna haja ya kuchukua hatua zaidi.
Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limekuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa uongozi wa Infantino na limekuwa likimtaka ajiuzulu.
UEFA pia imeandaa hatua za kisheria za jinai dhidi ya Infantino na kuwasilisha madai katika mahakama tatu nchini Marekani, ikitaka nyaraka zote zinazohusiana na FFE ziwekwe wazi.
Hewitt amesema nyaraka hizo zinapaswa kuwasilishwa kwa Baraza la FIFA ili wajumbe waweze kuelewa kilichotokea na kutathmini hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Alipoulizwa kama msimamo wake kuhusu Infantino umebadilika baada ya kikao hicho, Hewitt alisema bado hakuna kilichobadilika.
“Kwa upande wangu, hakuna kilichobadilika. Sina taarifa mpya zinazonifanya nijisikie tofauti, isipokuwa kwamba sasa tuna rais ambaye ameomba radhi,” alisema.
ANAKABILIWA NA UCHAGUZI
Infantino anatarajiwa kuwania tena urais wa FIFA kwa mara ya tatu mwezi Machi, huku hadi sasa kukiwa hakuna mgombea mwenye nguvu aliyejitokeza rasmi kumpa upinzani mkubwa.
Aliyekuwa beki wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Uswisi, Ramon Vega, amesema ana nia ya kuwania nafasi hiyo, lakini nafasi yake ya kupata barua tano za uungwaji mkono kutoka kwa vyama wanachama inaonekana kuwa ngumu, achilia mbali kuwa mpinzani wa kweli.
Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi waandamizi wa soka barani Ulaya wamesema kuwa wangependa aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, ajitokeze kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, bado haijafahamika kama Wenger yuko tayari kuacha nafasi yake ya sasa ya kuwa mkuu wa maendeleo ya soka duniani wa FIFA na kuingia kwenye kinyang'anyiro dhidi ya bosi wake.
Hewitt amekiri kuwa UEFA na wapinzani wengine wa Infantino duniani wanapaswa kumpata mgombea atakayewasilisha jina lake kabla ya muda wa mwisho wa uteuzi, Novemba 18, 2026.
Pia amesema ni muhimu kwa FIFA kuwa na uchaguzi wenye ushindani, hasa ikizingatiwa kuwa Infantino alichaguliwa bila kupingwa mwaka 2019 na 2023.
“Ni muhimu kwa Gianni kuwa na mtu mwingine anayewasilisha sera tofauti na ni vizuri FIFA kuwa na uchaguzi huo,” alisema Hewitt.
Alisisitiza kuwa FIFA ina vyama wanachama 211 na kila kimoja kinapaswa kuwa na nafasi ya kupiga kura kulingana na mtazamo wake.
Kwa maelezo yake, rais anayefaa kuiongoza FIFA anatakiwa kuweka soka mbele, kuwaunganisha watu duniani na kuwa na ujasiri wa kufanya mageuzi.
KESI YA BALOGUN
Mbali na FFE, suala la mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, kuondolewa adhabu ya kusimamishwa mechi moja baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika Kombe la Dunia, lilikuwa miongoni mwa hoja zilizotawala kikao hicho.
Adhabu ya Balogun ilisimamishwa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuomba uamuzi huo upitiwe upya.
Kwa mujibu wa taarifa za BBC Sport, pendekezo liliwasilishwa kwa Baraza la FIFA la kurekebisha kanuni za nidhamu ili kuzuia hali kama hiyo kujirudia.
Marekebisho hayo yanapendekeza kuweka wazi kuwa kamati ya nidhamu haitakuwa na mamlaka ya kusimamisha adhabu ya moja kwa moja ya mechi moja inayotokana na kadi nyekundu.
Kamati ya sheria ya FIFA inatarajiwa kupitia suala hilo na kutoa taarifa kwa Baraza la FIFA mwezi Desemba.
Hewitt amesema namna tukio hilo lilivyoshughulikiwa, sambamba na utata wa FFE, imeiweka soka katika hatari ya kupoteza heshima yake.
“Kilichotokea Julai hakikulitendea haki soka. Iwe ni suala la Balogun au FFE, heshima ya soka iliwekwa kwenye hatari kubwa,” alisema.
Alionya kuwa pale maamuzi yanapoanza kuathiriwa na mambo ya nje badala ya misingi ya mchezo, hiyo ni siku mbaya kwa soka.
TUZO YA AMANI YA TRUMP
Tuzo ya amani ya FIFA iliyotolewa kwa Trump pia ilijadiliwa katika kikao hicho, huku Hewitt akisema tabia ya Infantino ya kuwapa kipaumbele watu mashuhuri na viongozi wengine mbele ya vyama wanachama ilikumbushwa na wajumbe.
“Anapoweka viongozi wengine mbele ya vyama vyake 211, anakuwa amepoteza maana halisi ya soka,” alisema Hewitt, akibainisha kuwa hoja hiyo haikutolewa na wazungu pekee.
FIFA imeelekeza kamati yake ya masuala ya kijamii kuchunguza namna tuzo hiyo ilivyoanzishwa na kutolewa, nani alifanya uamuzi huo na iwapo tuzo hiyo inapaswa kuondolewa au kufanyiwa marekebisho.
Kamati hiyo inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Baraza la FIFA mwezi Desemba, ambapo wajumbe wataamua hatua za kuchukua kwa kuzingatia mapendekezo yatakayotolewa.