Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Warithi wa Motsepe CAF waanza kutajwa

CAF Pict

Muktasari:

  • Majina yanayotajwa katika mijadala ya soka la Afrika ni rais wa Shirikisho la Soka Cameroon, Samuel Eto’o, rais wa Shirikisho la Soka Mauritania, Ahmed Yahya, rais wa Shirikisho la Soka Ivory Coast, Yacine Idriss Diallo, na makamu wa rais wa CAF, Souleiman Waberi, kutoka Djibouti.

RABAT, MOROCCO: MAJINA ya viongozi wanne yameanza kutajwa katika taarifa za vyombo vya habari kama wanaoweza kurithi nafasi ya rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk. Patrice Motsepe, ambaye awali alieleza kuwa hana nia ya kugombea muhula wa tatu mwaka 2029.

Majina yanayotajwa katika mijadala ya soka la Afrika ni rais wa Shirikisho la Soka Cameroon, Samuel Eto’o, rais wa Shirikisho la Soka Mauritania, Ahmed Yahya, rais wa Shirikisho la Soka Ivory Coast, Yacine Idriss Diallo, na makamu wa rais wa CAF, Souleiman Waberi, kutoka Djibouti.

Hata hivyo, hakuna kati ya viongozi hao wanne ambaye ametangaza rasmi nia ya kuwania nafasi hiyo, huku mchakato wa kumtafuta mrithi wa Motsepe ukiwa bado katika hatua za awali.

Eto’o ni miongoni mwa majina yanayotajwa kutokana na historia yake katika soka la kimataifa. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Cameroon aliwahi kucheza katika klabu kubwa za Ulaya, zikiwamo Barcelona na Inter Milan, kabla ya kuingia katika uongozi wa soka kwa kuwa rais wa Shirikisho la Soka Cameroon.

Mbali na nafasi hiyo, Eto’o ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, inayoshiriki katika uamuzi yanayohusu uendeshaji wa soka barani Afrika.

Naye Yahya, ambaye ni rais wa Shirikisho la Soka Mauritania, pia ni mjumbe wa Baraza la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Uzoefu wake katika uongozi wa soka nchini mwake na katika taasisi ya kimataifa ni miongoni mwa mambo yanayomweka katika mjadala huo.

Wakati Diallo anaongoza Shirikisho la Soka Ivory Coast na ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, nafasi zinazompa uzoefu katika usimamizi wa soka la kitaifa na Afrika.

Waberi, kutoka Djibouti, anahudumu kama makamu wa rais wa CAF na pia ni mjumbe wa Baraza la FIFA. Nafasi hizo zinamweka miongoni mwa viongozi wanaotajwa katika mijadala kuhusu mabadiliko ya uongozi wa shirikisho hilo.

Motsepe, mfanyabiashara kutoka Afrika Kusini, alichaguliwa kuwa rais wa CAF Machi 2021 na kuchaguliwa tena bila kupingwa Machi 2025 kwa muhula wa pili unaomalizika mwaka 2029.

Kauli yake ya awali kwamba hana nia ya kuwania muhula wa tatu imechochea mijadala kuhusu nani anaweza kuchukua nafasi yake baada ya kumalizika kwa uongozi wake.

Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwa muhimu kwa mustakabali wa soka la Afrika, wakati CAF ikiendelea kukabiliwa na mijadala kuhusu mfumo wa uendeshaji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na mwelekeo wa mashindano hayo katika miaka ijayo.

Pamoja na majina hayo kuanza kujadiliwa, bado haijajulikana ni nani atakayeamua kuingia rasmi katika kinyang’anyiro hicho wakati utakapowadia.


AFCON KUREJEA MIAKA MIWILI?

RAIS wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amesema wanafanyia tathmini upya mfumo wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kwa kuangalia uwezekano wa kurejesha mashindano hayo kufanyika kila baada ya miaka miwili badala ya minne.

Motsepe alitoa kauli hiyo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Cape Verde, siku ya mwisho ya Mkutano wa Mkakati wa CAF.

“Tunaangalia uwezekano wa kurejesha AFCON kufanyika kila baada ya miaka miwili. Jambo hilo bado linafanyiwa tathmini,” amesema Motsepe.

Kauli hiyo inaashiria uwezekano wa mabadiliko katika mpango uliotangazwa Desemba 2025, uliotaka AFCON kuanza kufanyika kila baada ya miaka minne baada ya toleo la mwaka 2028.

Kwa mujibu wa mpango huo, AFCON ya mwaka 2027 itafanyika Kenya, Tanzania na Uganda, ikifuatiwa na toleo jingine mwaka 2028 kabla ya mfumo mpya kuanza kutumika.

CAF iliambatanisha mabadiliko hayo na mpango wa kuanzisha Ligi ya Mataifa ya Afrika (African Nations League) mwaka 2029, mashindano yaliyokusudiwa kutoa fursa kwa timu za taifa za wanaume kushindana katika mashindano makubwa kila mwaka, isipokuwa miaka ya Kombe la Dunia.

Hata hivyo, mpango wa kuifanya AFCON kuwa ya kila baada ya miaka minne ulikumbana na ukosoaji kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka barani Afrika muda mfupi baada ya kutangazwa.

Mwezi Januari, Motsepe aliutetea uamuzi huo na kupinga madai kwamba CAF ilishinikizwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kubadilisha mfumo wa mashindano hayo.

Kauli yake ya sasa inaonyesha kuwa suala hilo bado linajadiliwa, ingawa hakutangaza rasmi kufutwa kwa mpango wa miaka minne.

Iwapo CAF itaamua kurejesha mfumo wa miaka miwili, italazimika kupitia upya kalenda ya mashindano ambayo tayari imeanza kupangwa. Shirikisho hilo limefungua mchakato wa kuomba zabuni za kuandaa matoleo ya AFCON ya mwaka 2028, 2032 na 2036.

Hadi sasa, CAF haijaeleza jinsi mabadiliko yanayoweza kufanyika yatakavyoathiri mashindano hayo pamoja na mpango wa Ligi ya Mataifa ya Afrika, wala muda ambao uamuzi wa mwisho unatarajiwa kutolewa.

Mjadala huo umefanyika katika Mkutano wa Mkakati wa CAF uliodumu kwa siku tatu nchini Cape Verde, uliowakutanisha marais wa vyama vyote 54 wanachama, wajumbe wa Kamati ya Utendaji, makocha wa timu za taifa na viongozi wa soka kujadili vipaumbele vya mchezo huo barani Afrika hadi mwaka 2030.