Argentina waota Messi mwingine Kombe la Dunia 2030
Muktasari:
- Kilichoamsha mjadala ni hesabu rahisi ya umri. Kombe la Dunia la mwaka 2030, litakaloadhimisha miaka 100 tangu mashindano hayo kuanzishwa, litamkuta Thiago akiwa na miaka 18, baada ya kutimiza umri huo mwezi Novemba mwaka huo.
LONDON, ENGLAND: MUSTAKABALI wa Lionel Messi unaendelea kuwa gumzo kubwa katika ulimwengu wa soka, lakini sasa mashabiki wa Argentina wameibua ndoto mpya inayomhusu nahodha huyo na mwanawe mkubwa, Thiago Messi.
Kilichoamsha mjadala ni hesabu rahisi ya umri. Kombe la Dunia la mwaka 2030, litakaloadhimisha miaka 100 tangu mashindano hayo kuanzishwa, litamkuta Thiago akiwa na miaka 18, baada ya kutimiza umri huo mwezi Novemba mwaka huo.
Hesabu iliyowapa matumaini mashabiki
Mashabiki wengi wanaamini kuwa iwapo Thiago ataendelea kukua kisoka na kufikia kiwango cha kucheza soka la kulipwa mapema, huenda akapata nafasi ya kuitwa katika kikosi cha taifa cha Argentina na kucheza pamoja na baba yake.
Kwa sasa, Thiago mwenye umri wa miaka 13 anacheza katika akademi ya Inter Miami, ambapo maendeleo yake yanaendelea kufuatiliwa kwa karibu na mashabiki wanaotamani kuona familia ya Messi ikiendelea kuandika historia.
Ndoto yake ni Argentina
Licha ya kuzaliwa Barcelona, Hispania, wakati Messi akiitumikia Barcelona, Thiago ameeleza mara kadhaa kuwa ndoto yake ni kuivaa jezi ya Argentina.
Katika mahojiano mbalimbali, kijana huyo amesema angependa kufuata nyayo za baba yake kwa kuitumikia timu ya taifa ya Albiceleste.
Pia, amewahi kukiri kuwa moja ya ndoto zake kubwa ni kushiriki chumba cha kubadilishia nguo au hata kucheza uwanjani pamoja na Messi akiwa katika timu ya taifa.
Kauli hiyo imewapa mashabiki wa Argentina sababu ya kuendelea kuota kuona baba na mwana wakicheza pamoja katika Kombe la Dunia la 2030.
Familia yenye mapenzi makubwa ya soka
Thiago si mtoto pekee wa Messi anayependa soka. Wadogo zake, Mateo na Ciro, pia wanacheza katika timu za vijana na tayari wanaonyesha dalili za vipaji vyao.
Hali hiyo imezidi kuwapa matumaini mashabiki kwamba familia ya Messi inaweza kuendelea kuwa sehemu ya historia ya soka la Argentina kwa miaka ijayo.
Bado ni mapema
Pamoja na matumaini hayo, wengi wanakiri kuwa safari ya kufikia kiwango cha juu katika soka si rahisi.
Kucheza katika timu ya taifa ya Argentina ni changamoto kubwa, na hakuna anayetarajiwa kubeba mzigo wa kulinganishwa na mafanikio makubwa aliyoyapata Lionel Messi.
Kwa sasa, mjadala huo unabaki kuwa ndoto ya mashabiki, huku muda ukiwa ndiyo utakaoamua kama Thiago atatimiza matarajio hayo na pengine kuandika historia kwa kucheza Kombe la Dunia pamoja na baba yake.