Ibrahima Konate akaribia kusepa Liverpool
Muktasari:
- Mkataba wa Konate unatarajiwa kumalizika Julai 1 mwaka huu ikiwa hatafikia mwafaka mpya na mabosi wa Liverpool.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa Liverpool, Ibrahima Konate, anatajwa kuwa mbioni kuondoka Anfield dirisha hili la usajili baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya na klabu hiyo.
Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa alijiunga na Liverpool mwaka 2021 na amekuwa sehemu muhimu ya safu ya ulinzi chini ya makocha Jurgen Klopp na Arne Slot.
Mkataba wa Konate unatarajiwa kumalizika Julai 1 mwaka huu ikiwa hatafikia mwafaka mpya na mabosi wa Liverpool.
Beki huyo wa kati aliwahi kuhusishwa kwa karibu na kuhamia Real Madrid majira ya joto yaliyopita, lakini alibaki Anfield huku mazungumzo ya kuongeza mkataba yakiendelea kwa miezi kadhaa.
Mwezi Aprili, Konate alidokeza kuwa mazungumzo yalikuwa karibu kukamilika licha ya tetesi za kuondoka kwake kuendelea kushika kasi.
“Tumekuwa tukizungumza na klabu kwa muda mrefu na tuko karibu kufikia makubaliano. Kuna nafasi kubwa ya mimi kubaki msimu ujao kwa sababu ndiyo kitu ambacho nimekuwa nikikitaka,” amesema Konate.
Hata hivyo, sasa inaelezwa kuwa beki huyo yupo mbioni kuondoka Liverpool mwishoni mwa Juni, akiungana na nyota wengine kama Mohamed Salah na Andrew Robertson wanaotarajiwa kuondoka klabuni hapo.
Konate ameisaidia Liverpool kutwaa mataji matatu ya ndani pamoja na ubingwa wa Ligi Kuu England katika kipindi chake cha kuitumikia klabu hiyo.
Licha ya awali kuhusishwa na Real Madrid, taarifa zinaeleza kuwa Paris Saint-Germain ndiyo yenye nafasi kubwa ya kuinasa saini yake dirisha hili la usajili.
PSG tayari ina mabeki wenye majina makubwa kama Marquinhos, Willian Pacho na Illia Zabarnyi, lakini bado inaonekana kumtaka Konate kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi.
Iwapo dili hilo litakamilika, Konate atarejea jijini Paris alikozaliwa baada ya kuitumikia Ufaransa kwenye michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.