Huyu Lamine Yamal ana balaa nyie!
Muktasari:
- Winga huyo Mhispaniola alifanya balaa kubwa uwanjani wakati alipowalamba chenga wachezaji sita wa Alaves huku akiweka rekodi ya kukimbia na mpira katika mchezo huo wa juzi Jumapili na kuifikia ya Lionel Messi aliyoweka miaka 17 iliyopita.
BARCELONA, HISPANIA: STAA wa boli, Lamine Yamal amekuwa gumzo baada ya kuonyesha kiwango cha juu kabisa kwenye ishu ya kukokota mpira wakati alipoisaidia Barcelona kupata ushindi muhimu dhidi ya Alaves kwenye La Liga.
Winga huyo Mhispaniola alifanya balaa kubwa uwanjani wakati alipowalamba chenga wachezaji sita wa Alaves huku akiweka rekodi ya kukimbia na mpira katika mchezo huo wa juzi Jumapili na kuifikia ya Lionel Messi aliyoweka miaka 17 iliyopita.
Barca ilishinda 1-0 uwanjani Estadi Olimpic Lluis Companys shukrani kwa bao pekee la kipindi cha pili la straika Robert Lewandowski.
Hata hivyo, Yamal ndiye aliyekuwa steringi wa mchezo huo na alifanya matukio 10 ya kukokota yaliyokamilika kati ya 20.
Kwa kufanya hivyo, anakuwa mchezaji wa pili wa Barca kufanya hivyo kwenye kukokota mpira mara nyingi kweye mechi moja tangu rekodi za takwimu hizo zilipoanza kurekodiwa msimu wa 2005/06. Messi ndiye mchezaji pekee aliyewahi kufanya hivyo kabla ya Yamal, alipotamba kwenye mechi ya Mallorca, Aprili 2007, alipokamilisha matukio 10 ya kukokota mpira kati ya 20.
Kwenye matukio 10 ya kukokota mpira, moja alifanya balaa baada ya kuwalamba chenga karibu nusu ya timu ya Alaves.
Baada ya kupokea mpira kutoka kwenye nusu ya upande wa Barca, alikimbia na mpira kwa kuwalamba chenga mastaa kibao wa Alaves kabla ya kupiga pasi kwenye wingi ya kushoto.
Licha ya kwamba hakufunga bao dhidi ya Alaves, kinda huyo amefunga mabao 10 katika mechi 29 katika michuano yote. Kinda huyo Mhispaniola ameasisti mara 15 pia katika mechi hizo huku ushindi dhidi ya Alaves umewafanya kupunguza pengo la pointi dhidi ya vinara Real Madrid kubaki kuwa pointi nne.
Barca inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga, pointi tatu nyuma ya Atletico Madrid inayoshika nafasi ya pili.