Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Europa league kila kona pamoto 

Muktasari:

  • Hatua ya ligi ya michuano ya Europa Ligi inaingia katika raundi ya tano, huku michezo 18 ikipangwa kuchezwa katika viwanja mbalimbali barani Ulaya.

MILAN, ITALIA: MABINGWA wa zamani wa Ulaya, AC Milan, Juventus na Celtic wanakabiliwa na mitihani migumu leo Alhamisi, huku Bournemouth na Ferencvaros zikisaka kuendeleza mwanzo wao mzuri katika hatua ya ligi ya Europa Ligi msimu wa 2026/27.

Hatua ya ligi ya michuano ya Europa Ligi inaingia katika raundi ya tano, huku michezo 18 ikipangwa kuchezwa katika viwanja mbalimbali barani Ulaya.

Mechi hizo zinatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na umuhimu wa pointi katika mbio za kujihakikishia nafasi nzuri kabla ya kumalizika kwa hatua hiyo.

Miongoni mwa michezo inayovuta hisia ni Olympiacos dhidi ya AC Milan, Celta Vigo dhidi ya Bournemouth, Crystal Palace dhidi ya Real Sociedad na Torreense dhidi ya Celtic.

Bournemouth na Ferencvaros zinaingia katika raundi hii zikiwa na pointi 12 baada ya kushinda michezo yao yote minne ya awali, hivyo ushindi mwingine unaweza kuziimarisha katika nafasi za juu.

Kwa upande mwingine, Milan ina kazi ya kurekebisha mwenendo wake baada ya kupoteza michezo mitatu kati ya minne ya mwanzo.

Hizi hapa ni tathmini ya michezo yote 18 ya raundi hiyo, kwa kuzingatia matokeo ya awali na mazingira ya kila timu katika mashindano hayo.


OLYMPIACOS VS AC MILAN

Huu ni mchezo unaozikutanisha timu mbili zenye historia kubwa katika soka la Ulaya, lakini zinazoingia zikiwa na mwenendo tofauti. Olympiacos haijapoteza katika michezo yake minne ya awali na imekusanya pointi nane.

Milan, chini ya Ruben Amorim, imekuwa na mwanzo mgumu baada ya kupoteza michezo mitatu kati ya minne. Kikosi hicho kinahitaji matokeo mazuri ili kufufua matumaini yake ya kusonga mbele.

Milan pia ina kumbukumbu mbaya ya kucheza ugenini dhidi ya Olympiacos, ikiwa haijawahi kushinda nchini Ugiriki katika ziara zake mbili zilizotangulia.


CELTA VIGO VS BOURNEMOUTH

Bournemouth inaingia katika mchezo huu ikiwa miongoni mwa timu zinazofanya vizuri zaidi kwenye hatua ya ligi, ikiwa imeshinda mechi zote nne na kukusanya pointi 12.

Ushindi wake dhidi ya Milan, Real Sociedad na Sparta Prague unaonyesha uimara wa kikosi hicho kinachonolewa na Marco Rose.

Hata hivyo, safari ya kwenda Hispania haitakuwa rahisi kwa sababu Celta inahitaji pointi ili kuboresha nafasi yake baada ya kuanza kwa kusuasua.

Bournemouth itategemea kasi ya washambuliaji wake na uwezo wa kutumia nafasi, huku Celta ikitafuta kutumia faida ya uwanja wa nyumbani.

VIKTORIA PLZEN VS BENFICA

Benfica inasafiri kwenda Czechia ikiwa na dhamira ya kuendeleza mwanzo wake mzuri katika mashindano hayo. Imeshinda michezo yake yote minne na kukusanya pointi 12.

Kikosi hicho kimeonyesha uwezo mkubwa wa kushambulia, kikiwamo kitendo cha kuifunga Celtic mabao 4-1 na Omonia mabao 4-1.

Hata hivyo, Viktoria Plzen itakuwa na nafasi ya kutumia uwanja wake wa nyumbani kujaribu kuizuia timu hiyo ya Ureno. Benfica inahitaji ushindi ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu moja kwa moja hatua inayofuata.


GNK DINAMO VS BAYER LEVERKUSEN

Leverkusen inakutana na mtihani mgumu ugenini dhidi ya Dinamo Zagreb, timu ambayo imeonyesha uwezo wa kupambana na wapinzani wenye majina makubwa.

Dinamo iliifunga Sunderland mabao 2-0 katika mchezo uliopita na pia imewahi kuichapa Anderlecht bao 1-0.

Leverkusen nayo ilianza kwa ushindi dhidi ya Celje, lakini imekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika michezo iliyofuata, ikiwamo kupoteza dhidi ya Marseille.

Mchezo huu utakuwa muhimu kwa Leverkusen kurejea katika mwenendo mzuri na kwa Dinamo kuimarisha nafasi yake.


BESIKTAS VS HAPOEL BEER-SHEVA

Besiktas inaingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza dhidi ya Celtic mabao 3-2 katika raundi iliyopita.

Timu hiyo ya Uturuki inahitaji kurejea kwenye ushindi ili kuimarisha matumaini yake ya kusonga mbele.

Hapoel Beer-Sheva nayo haijawa na mwanzo mzuri, ikiwa imeshindwa kupata ushindi katika michezo yake minne ya awali. Ilipoteza dhidi ya OFI Crete mabao 2-0 katika mchezo uliopita.

Faida ya uwanja wa nyumbani inaweza kuwa silaha muhimu kwa Beşiktaş, lakini Hapoel itakuwa na sababu ya kupambana kutafuta matokeo.


MARSEILLE VS LEVSKI SOFIA

Marseille inaingia katika mchezo huu ikiwa na matumaini ya kuendeleza matokeo mazuri baada ya kuifunga Bayer Leverkusen bao 1-0 katika raundi iliyopita.

Timu hiyo ya Ufaransa inahitaji kutumia faida ya uwanja wa nyumbani kupata ushindi mwingine, hasa ikizingatiwa kuwa ilianza vibaya kwa kupoteza dhidi ya Beşiktaş.

Levski Sofia nayo imeonyesha kuwa inaweza kupambana baada ya kupata ushindi dhidi ya Jagiellonia, lakini safari ya kwenda Ufaransa itakuwa mtihani mkubwa.


FERENCVAROS VS CELJE

Ferencváros ni miongoni mwa timu zilizovutia zaidi katika hatua ya ligi baada ya kushinda michezo yote minne na kukusanya pointi 12.

Timu hiyo ya Hungary pia ina rekodi nzuri ya kucheza nyumbani katika mashindano ya Ulaya, ikiwa haijapoteza katika mechi 12 zilizopita za nyumbani, ikishinda tisa na kutoka sare tatu.

Celje nayo imeonyesha uwezo wa kushindana, lakini inakabiliwa na mtihani mkubwa dhidi ya wenyeji hao.

Ferencvaros itakuwa na nafasi ya kuendeleza rekodi yake na kufikisha pointi 15.


JUVENTUS VS OMONIA

Juventus inatarajiwa kuwa na kazi ya kutafuta ushindi mbele ya mashabiki wake dhidi ya Omonia ya Cyprus.

Miamba hiyo ya Italia ilianza vizuri kwa kuifunga NEC Nijmegen mabao 5-0, lakini baadaye ilipoteza dhidi ya AZ Alkmaar na kutoka sare na Rennes.

Omonia nayo imekuwa na wakati mgumu, ikipoteza dhidi ya NEC Nijmegen mabao 3-1 katika mchezo uliopita.

Juventus inahitaji kutumia uzoefu wake wa michuano ya Ulaya na ubora wa kikosi chake kuhakikisha haipotezi pointi nyingine muhimu.


CRYSTAL PALACE VS REAL SOCIEDAD

Huu ni miongoni mwa michezo inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili.

Crystal Palace imekuwa na matokeo yanayochanganya, ikiwamo ushindi mkubwa wa mabao 4-0 dhidi ya Lech Poznan, lakini pia imepoteza dhidi ya Lyon na kutoka sare na Hoffenheim.

Real Sociedad nayo inaingia ikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Lyon.

Mchezaji wa kuangaliwa ni Sergio Gomez wa Real Sociedad, ambaye amefunga mabao matatu katika mashindano haya msimu huu licha ya kucheza nafasi ya beki wa kushoto.


UNION SAINT-GILLOISE VS LECH POZNAN

Union SG imeonyesha uimara katika baadhi ya michezo yake, ikiwamo ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Hapoel Beer-Sheva, lakini bado inahitaji matokeo mazuri ili kuimarisha nafasi yake.

Lech Poznan nayo imekuwa na wakati mgumu katika mashindano haya, ikiwamo kupoteza dhidi ya Benfica mabao 3-1 katika mchezo uliopita.

Union SG itakuwa na faida ya kucheza nyumbani, lakini Lech inahitaji matokeo yatakayoiweka katika ushindani wa kuwania nafasi za kufuzu.


SALZBURG VS ARARAT-ARMENIA

Salzburg inaingia katika mchezo huu ikiwa na hitaji kubwa la kupata pointi tatu baada ya kuanza kwa kusuasua katika mashindano hayo.

Timu hiyo ya Austria ilipata sare dhidi ya Celje katika raundi ya tatu na kupoteza dhidi ya Anderlecht mabao 2-0 katika mchezo uliofuata.

Ararat-Armenia nayo imekuwa na changamoto ya kupata matokeo mazuri, ikipoteza dhidi ya Torreense mabao 3-2 katika mchezo wake uliopita.

Huu ni mchezo ambao Salzburg inaweza kutumia ubora wa kikosi na uwanja wa nyumbani kurejea kwenye ushindi.


NEC NIJMEGEN VS RENNES

NEC Nijmegen imekuwa na mwanzo mzuri katika mashindano hayo, ikiwamo ushindi dhidi ya Omonia na Dinamo Zagreb.

Rennes nayo imeonyesha uimara katika baadhi ya michezo, lakini sare ya bila mabao dhidi ya Olympiacos na kupoteza dhidi ya Ferencváros kumeifanya ihitaji matokeo mazuri.

Mchezo huu unaweza kuamua mwelekeo wa timu hizo katika mbio za kufuzu, huku NEC ikitarajia kutumia uwanja wa nyumbani kupata ushindi.


OFI CRETE VS ANDERLECHT

OFI Crete inaingia katika mchezo huu ikiwa na morali baada ya kuifunga Hapoel Beer-Sheva mabao 2-0 katika raundi iliyopita.

Timu hiyo ya Ugiriki, ambayo ni mara yake ya kwanza kushiriki hatua ya ligi ya mashindano haya, tayari imekusanya pointi sita kati ya 12.

Anderlecht nayo imekuwa na matokeo mazuri, ikiwamo ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Salzburg.

Mchezo huu utakuwa kipimo cha uwezo wa OFI kuendeleza mafanikio yake dhidi ya timu yenye uzoefu mkubwa zaidi katika mashindano ya Ulaya.


LYON VS LILLESTRØM

Lyon itakuwa na nafasi ya kutumia uwanja wa nyumbani kurejea kwenye ushindi baada ya kutoka sare na Real Sociedad katika mchezo uliopita.

Timu hiyo ya Ufaransa ilianza vizuri kwa kuifunga Anderlecht, lakini imekuwa ikipoteza baadhi ya pointi katika michezo iliyofuata.

Lillestrøm nayo inaingia katika mchezo huu ikiwa na changamoto kubwa baada ya kupoteza dhidi ya Viktoria Plzen na Real Sociedad.

Kwa ubora wa vikosi na uzoefu wa michuano ya Ulaya, Lyon inaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi, lakini italazimika kuthibitisha hilo uwanjani.


TORREENSE VS CELTIC

Celtic inasafiri kwenda Ureno ikiwa na matumaini ya kuendeleza ushindi wake wa mabao 3-2 dhidi ya Beşiktaş katika mchezo uliopita.

Timu hiyo ya Scotland ilianza vibaya kwa kupoteza dhidi ya Ferencváros na Benfica, hivyo inahitaji ushindi mwingine ili kuimarisha nafasi yake.

Torreense nayo imeonyesha kuwa inaweza kuwa mpinzani hatari, ikiwa imepata ushindi dhidi ya Lillestrøm na Ararat-Armenia.

Mshambuliaji Benjamin Nygren ni miongoni mwa wachezaji wanaotakiwa kuangaliwa katika kikosi cha Celtic, ambacho kinahitaji kuendeleza kasi ya ushindi.


SUNDERLAND VS JAGIELLONIA

Sunderland itakuwa na jukumu la kutumia uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri dhidi ya Jagiellonia.

Timu hiyo ya England imekuwa na changamoto katika kutumia nafasi za kufunga, ikiwa imepiga mashuti 39 yaliyotoka nje ya lango katika hatua hii ya ligi, idadi kubwa kuliko timu nyingine zote kwa tofauti ya mashuti manane.

Jagiellonia nayo imekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika michezo yake ya karibuni, ikiwamo kupoteza dhidi ya Levski Sofia.

Sunderland inahitaji kuboresha umaliziaji wake ili kupata ushindi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.


HOFFENHEIM VS STURM GRAZ

Huu ni mchezo mwingine unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zote kuwa na malengo ya kuimarisha nafasi zao.

Hoffenheim imekuwa na matokeo yanayochanganya, ikiwamo ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Lyon, lakini pia kupoteza dhidi ya Beşiktaş na kutoka sare na Crystal Palace.

Sturm Graz nayo imepata ushindi dhidi ya Marseille, lakini ilipoteza dhidi ya Celje katika mchezo uliopita.

Hivyo, timu zote zinaingia zikitafuta ushindi utakaorejesha matumaini yao ya kufuzu.


SPARTA PRAGUE VS AZ ALKMAAR

Sparta Prague inakutana na AZ Alkmaar katika mchezo unaozikutanisha timu mbili zenye uwezo wa kushambulia na kutengeneza nafasi za mabao.

Sparta ilianza mashindano vizuri kwa kuifunga Ararat-Armenia mabao 4-1, lakini imepoteza dhidi ya Olympiacos na Bournemouth katika michezo iliyofuata.

AZ nayo imeonyesha uwezo mkubwa, ikiwamo ushindi dhidi ya Juventus na Hapoel Beer-Sheva, lakini ilipoteza dhidi ya Sunderland.