Bournemouth yasaka rekodi ya ushindi wa 10 mfululizo Ulaya
Muktasari:
- Mashabiki wa Bournemouth walipokata tiketi za ndege kwenda Hispania kufuatia droo ya Ligi ya Europa mwezi Agosti, wachache walitarajia timuu yao kuwa katika nafasi ilipo sasa.
LONDON, ENGLAND: NI timu saba pekee zilizowahi kushinda mechi 10 au zaidi mfululizo katika mashindano yote zikiwa Ligi Kuu England. Je, Bournemouth inaweza kuwa klabu ya nane?
Mashabiki wa Bournemouth walipokata tiketi za ndege kwenda Hispania kufuatia droo ya Ligi ya Europa mwezi Agosti, wachache walitarajia timuu yao kuwa katika nafasi ilipo sasa.
Mchezo dhidi ya Celta Vigo, leo Alhamisi, unaipa Bournemouth fursa ya kupata ushindi wake wa 10 mfululizo katika mashindano yote. Mfululizo wao wa sasa wa ushindi tisa tayari ni rekodi ya klabu hiyo kama timu ya ligi ya soka England tangu msimu wa 1923-24.
Hata mashabiki sugu zaidi wa Bournemouth wangecheka wazo la klabu yao kushinda mechi 10 mfululizo katika mashindano yote kama wangeliambiwa jambo hilo miezi michache iliyopita. Lakini huenda tusishangae sana.
The Cherries walimaliza msimu uliopita wakiwa na mfululizo wa mechi 18 bila kufungwa katika Ligi Kuu England, ambao ulikuwa mwisho bora zaidi wa msimu kwa timu yoyote katika mashindano hayo. Mfululizo huo uliongezeka hadi mechi 19 katika mashindano yote, kwa sababu licha ya kutolewa katika Kombe la FA kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Newcastle United mwezi Januari, mchezo wa raundi ya tatu ulimalizika kwa sare ya mabao 3-3 katika Uwanja wa St. James’ Park.
Mfululizo huo wa matokeo chini ya aliyekuwa kocha Andoni Iraola ulikuwa wa kuvutia, lakini mafanikio ya Marco Rose tangu alipomrithi Mhispania huyo yanaweza kuwa bora zaidi. Mfululizo wa sasa wa Bournemouth wa ushindi tisa pia umefuatia mwanzo usio wa kuvutia wa kocha huyo mpya Mjerumani. Walishinda mechi mbili pekee kati ya nane za kwanza za mashindano rasmi msimu wa 2026-27 (wakifungwa tatu na sare tatu), huku ushindi huo miwili wote ukiwa katika mashindano ya vikombe.
Baada ya kuchapwa mabao 5-1 na Chelsea katika raundi ya sita ya Ligi Kuu England, Bournemouth ilikuwa katika eneo la kushuka daraja ikiwa na pointi tatu pekee. Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sturm Graz katika Ligi ya Europa, siku tano baada ya kipigo hicho cha Stamford Bridge, ulikuwa mwanzo wa mabadiliko.
Tangu wakati huo, Bournemouth imeshinda kila mechi iliyocheza na, kwa kushangaza, imeruhusu mabao mawili pekee, licha ya kukosekana kwa kiungo muhimu Alex Scott kutokana na majeraha. Evanilson amekuwa nyota wa mfululizo huo wa ushindi, akifunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao katika mechi zake nane.
Mchezaji huyo Mbrazili amefunga bao katika kila moja ya mechi zake tano zilizopita katika mashindano yote akiwa na klabu hiyo, huku mfululizo wake wa kufunga mabao katika mechi sita mfululizo za Ligi Kuu England ukiwa rekodi ya klabu. Huenda akawa na jicho moja kwenye rekodi ya muda wote ya Jamie Vardy ya kufunga mabao katika mechi 11 mfululizo, iliyowekwa mwaka 2015.
Mchezo wa Ulaya wa leo, Alhamisi, nchini Hispania unaipa Bournemouth nafasi ya kufikisha ushindi 10 mfululizo, lakini mfululizo huo utakuwa wa kuvutia kwa kiwango gani ukilinganishwa na mafanikio ya awali ya klabu nyingine za Ligi Kuu England? Kushinda mechi nyingi mfululizo ni jambo adimu kwa klabu yoyote ya Ligi Kuu England, achilia mbali timu ambayo haijulikani kuwa miongoni mwa vigogo wa soka la England.
Ni timu saba pekee zilizoweza kupata mfululizo wa ushindi wa mechi 10 au zaidi katika mashindano rasmi zikiwa katika Ligi Kuu England. Klabu zote hizo zimeshinda angalau mataji matatu ya ligi hiyo. Bournemouth iko katika msimu wake wa 10 pekee kama klabu ya Ligi Kuu England.
Hata hivyo, Bournemouth italazimika kushinda mechi nyingine 13 mfululizo katika mashindano rasmi ili kuvunja rekodi ya kuvutia ya Manchester City ya Pep Guardiola, iliyoshinda mechi 21 mfululizo kati ya Desemba 2020 na Machi 2021. Ikianza na ushindi dhidi ya Southampton katika Ligi Kuu England Desemba 19, 2020, City ilipata ushindi 21 mfululizo katika mashindano yote kabla ya kushangazwa kwa kufungwa mabao 2-0 nyumbani na wapinzani wao, Manchester United, Machi 7, 2021.
Arsenal ilishinda mechi 11 za mwisho za mashindano rasmi msimu wa 2001-02, kabla ya kuongeza ushindi mwingine miwili mwanzoni mwa msimu wa 2002-03. Mfululizo huo wa ushindi 13 ndio wa pili kwa urefu kuwahi kufanywa na klabu ya Ligi Kuu England katika mashindano yote.
Bournemouth inapaswa kuwa na matumaini ya kupata ushindi wa 10 mfululizo dhidi ya Celta Vigo, ambayo imeshinda mechi nne pekee kati ya 18 katika msimu wa 2026-27. Ushindi wake wa hivi karibuni ulikuwa dhidi ya klabu ya daraja la nne, Salamanca UDS, katika Kombe la Mfalme (Copa del Rey).
Ikiishinda Celta, changamoto inayofuata ya Bournemouth itakuwa kupata ushindi wa 11 mfululizo katika mchezo wake wa nyumbani dhidi ya Fulham, ambayo iko nafasi ya 15 katika Ligi Kuu England na imekusanya pointi saba pungufu ya timu ya Rose. Kumekuwapo na matukio manane pekee ya timu ya Ligi Kuu England kushinda mechi 11 au zaidi mfululizo. Je, Bournemouth inaweza kuwa ya tisa?