Tenga: Tanzania iko tayari kwa AFCON 2027
Muktasari:
- Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ametoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Ofisi za CAF za AFCON 2027, jijini Dar es Salaam, zinazofanyika leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
MWENYEKITI wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), Leodger Tenga, amesema Tanzania iko tayari kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza rasmi Juni 19, hadi Julai 17, 2027, kwa kushirikisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.
Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ametoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Ofisi za CAF za AFCON 2027, jijini Dar es Salaam, zinazofanyika leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
"Ni fahari na heshina kubwa kwetu kwa Tanzania kupata nafasi hii muhimu, nikiri wazi tumejiandaa vizuri na tupo tayari kuonyesha kwa vitendo namna nchi yetu ilivyodhamiria kuleta mageuzi makubwa," amesema Tenga.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Ofisi za Uratibu za AFCON 2027, zilizohamishwa kutoka Nairobi Kenya hadi jijini, Dar es Salaam, zinaambatana na Shirikisho La Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kusaini Mkataba wa Ushirikiano na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Miongoni mwa wageni mbalimbali waliohudhuria ghafla hiyo ya leo ni Katibu Mkuu wa CAF, Samson Adamu,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.
Wengine ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ),Dkt. Riziki Pembe Juma na Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye.