Hesabu kali
Muktasari:
Pep ni bonge la mdadisi, anajua matukio uwanjani
KATIKA toleo lililopita, tuliona kwenye mfululizo wa Kitabu cha Pep Confidential, Mwandishi Marti Perarnau akizungumza na Carles Planchart, kiongozi wa wachambuzi na wanaofanya tathmini ya kila mechi na kuwasilisha mawazo yao kwa kocha, Pep Guardiola kuhusu nini kifanyike na mbinu ipi sahihi itumike.
Kwa kawaida kwa Pep kila mpinzani anapangiwa mbinu kulingana na uwezo wake uwanjani na aina ya wachezaji alionao. Sasa endelea…
Katika hilo kwa mfano, kunakuwa na orodha ya namna wachezaji walivyokabiliana na mipira ya juu, vichwa, chenga, pasi na mengineyo na baada ya hapo wanamwonyesha kila mchezaji picha ya video ambayo itakuwa msaada kwa mchezaji binafsi na nafasi yake au timu nzima.
Picha zote za video zinachukuliwa kwa mapana ili waweze kumchambua mchezaji na kazi anayoifanya kwa kuzingatia mbinu za kiuchezaji kwenye timu na si kwa namna anavyocheza yeye mwenyewe.
“Pep kwa wakati wote huwa anapenda kuangalia mechi yote, na mara tu baada ya mechi kumalizika huwa tunamwekea video kwenye kompyuta yake,’’ anaendelea kusema Planchart.
“Atakachofanya baada ya hapo ni ama kuangalia mechi yote au kuangalia matukio fulani muhimu ambayo tutakuwa tumeyabaini, matukio hayo huwa ni mchezaji kwa mchezaji au aina fulani ya tukio au mbinu tofauti tofauti.
“Hapo pia atakiona kile nilichokiandika kikiwa na matukio ya mechi pamoja na matukio muhimu tofauti tofauti ambayo tumekubaliana kuyamulika pamoja na kuigawa mechi kwa kuzingatia matukio, Pep anapenda kuichambua mechi peke yake na baada ya hapo kutoa tathmini yake mwenyewe.”
Tathmini na uchambuzi mwingine unahusisha kuigawanya timu pinzani, hatua muhimu katika kuifanya Bayern ichague namna au mbinu gani sahihi itumike kukabiliana na mpinzani wake, Ujerumani wana tabia ya kurekodi mechi zote za Bundesliga pamoja na zile za Bundesliga B (Ligi Daraja la Pili) na klabu zinapewa video hizo kila Jumatatu asubuhi.
Katika Ligi ya Mabingwa hakuna utaratibu unaofanana na huo, na ni vigumu mno kurekodi mechi za ligi hiyo kiasi kwamba baadhi ya klabu huamua kutumia kamera ndogo kurekodi kutoka jukwaani au kuvaa miwani zenye kurekodi.
Ni muhimu mno kurekodi mechi katika mfumo ambao utaonyesha matukio kwa mapana ili kumfanya kocha aweze kuchambua mbinu husika katika kila mechi.
“Kwa Ujerumani skauti ni sehemu ya kazi muhimu inayoheshimiwa, haichukuliwi kama ni kikundi cha watu wanaofanya uchunguzi kwa siri, klabu zina utaratibu wa kupeana video za mechi, ni jambo la kawaida hapa,’’ anaeleza Planchart.
Pia ni muhimu kumfanyia tathmini mpinzani wako ili kuchagua aina ya uchezaji, wachezaji utakaowahitaji na hata aina ya mazoezi ambayo utayafanya kama sehemu ya maandalizi ya kuelekea kwenye mechi husika.
“Wakati tukiwa Barcelona tunapokuwa na mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tunamfanyia tathmini na kumchambua mpinzani wetu kwa kuziangalia mechi zake 12 za mwisho na katika mechi za michuano mengine huwa tunaangalia kwa wastani mechi tano au sita za mpinzani wetu,’’ anaeleza Planchart.
“Katika hilo pia tunazingatia majira ya mwaka na aina ya mpinzani, ambaye mpinzani wetu amekutana naye hapo kabla kwa kila mechi, kunakuwa na utofauti wa kubaini kama kuna juhudi zinazofanyika au wanasubiri tu na kufanya mashambulizi ya kushitukiza au kama wana staili ya uchezaji inayolingana na ya kwetu na mengineyo.
Hayo ni mambo muhimu na ni lazima kuyatizama kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha tunakuwa na matokeo mazuri uwanjani.
“Kama wapinzani wetu wanacheza na timu ambayo inafanana na yetu hilo linakuwa jambo zuri kama si hivyo hapo umuhimu unakuwa umepungua,’’ anafafanua zaidi Planchart.
Baada ya kuzifanyia tathmini mechi tano au sita, Planchart anaandaa ripoti kwa ajili ya Pep, ripoti inayoandaliwa kwa kuzingatia matukio muhimu na yanayohusiana na uchezaji wa timu husika, ripoti hiyo inawasilishwa kwa kutumia video ili iwe rahisi kueleweka na kuchambuliwa kikamilifu.
Ripoti hiyo itatoa mifano mitatu kwa kila aina ya tukio, kama Pep akiona ina msaada kwake, katika kazi anayoifanya atazingatia taarifa aliyowasilishiwa na Planchart.
“Kwa kawaida mara baada ya mechi kumalizika au kitu cha kwanza kinachofanyika asubuhi ya siku inayofuata, nampa ripoti inayohusu mpinzani ajaye, nafanya kazi ya wiki mbili zijazo lakini anachofanya yeye ni kufikiria mechi ijayo tu.
Itaendelea Jumamosi ijayo…