Mitihani ya Kachwele Ulaya
Muktasari:
- Katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, Kryvbas inashika nafasi ya mwisho baada ya kucheza mechi 11, ikipata ushindi mmoja, sare nne na kupoteza sita, na kukusanya pointi saba.
MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Cyprian Kachwele, anakabiliwa na changamoto kubwa barani Ulaya baada ya klabu yake, FC Kryvbas Kryvyi Rih, kujikuta mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Ukraine, ikiwa na kazi ya kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji ili kuinusuru timu hiyo na hatari ya kushuka daraja.
Katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, Kryvbas inashika nafasi ya mwisho baada ya kucheza mechi 11, ikipata ushindi mmoja, sare nne na kupoteza sita, na kukusanya pointi saba.
Takwimu zinaonyesha changamoto inayokikabili kikosi hicho katika safu zote mbili. Safu ya ushambuliaji imefunga mabao nane pekee katika mechi hizo, huku safu ya ulinzi ikiruhusu mabao 18.
Kachwele, mwenye umri wa miaka 21, alijiunga na Kryvbas Septemba 2026 kwa mkataba wa miaka minne akitokea Halifax Wanderers ya Amerika Kaskazini. Sasa ana jukumu la kushirikiana na wenzake kuongeza kasi, ubunifu na uwezo wa kufunga mabao ili kuisaidia timu kurejea kwenye ushindani.
Endapo Kryvbas itaendelea kupoteza pointi na kuruhusu mabao kwa kiwango hicho, hatari ya kushuka daraja itaongezeka zaidi kadiri msimu unavyoendelea.
Hata hivyo, uwepo wa Kachwele katika kikosi hicho unatoa matumaini kwa mashabiki wanaosubiri mabadiliko ya matokeo. Wanatarajia umri wake, nguvu na uzoefu wa kucheza katika ligi mbalimbali za Amerika Kaskazini, pamoja na kuichezea Taifa Stars, vitasaidia kuimarisha timu hiyo.
Kwa sasa, mtihani mkubwa kwa Kachwele na wenzake ni kurejesha morali ya ushindi, kupunguza makosa ya kiulinzi yanayosababisha kufungwa mabao na kuanza kupanda katika msimamo wa ligi kabla hali haijawa ngumu zaidi.
Akizungumzia changamoto hiyo, Kachwele amesema alijiunga na klabu hiyo akiwa na dhamira ya kusaidia kuboresha hali ya timu.
“Kwa sasa timu inapitia kipindi kigumu, kwa hiyo nilikuja hapa kupigania, kusaidia klabu na kubadilisha hali hiyo kuwa bora,” amesema Kachwele.