Tunkara: Nyota Lamasia anayekiwasha Kombe la Dunia
Muktasari:
- Kiungo huyo mshambuliaji wa Hispania, mwenye umri wa miaka 16, amekuwa kivutio katika michuano hiyo inayoendelea Qatar, akionyesha uwezo mkubwa wa kuchezesha timu, kupenya kwenye safu za ulinzi na kutumia mguu wake wa kushoto kutengeneza madhara kwa wapinzani.
Kutoka kucheza soka pekupeku kwenye mitaa ya kijiji cha kwao nchini Gambia hadi kuwa miongoni mwa vipaji vinavyotazamwa katika Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17, safari ya Ebrima Tunkara ni simulizi ya kipaji, uvumilivu na malezi ya soka.
Kiungo huyo mshambuliaji wa Hispania, mwenye umri wa miaka 16, amekuwa kivutio katika michuano hiyo inayoendelea Qatar, akionyesha uwezo mkubwa wa kuchezesha timu, kupenya kwenye safu za ulinzi na kutumia mguu wake wa kushoto kutengeneza madhara kwa wapinzani.
Tunkara ambaye anakulia katika akademi ya FC Barcelona maarufu La Masia, alionyesha tena ubora wake wakati Hispania ilipoifunga Morocco mabao 2-0 Novemba 26, 2026.
Katika mchezo huo, alifunga bao dakika ya 18 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Sergi Mayans, kabla ya kutumia ufundi wake kuudhibiti mpira, kuuhamishia kwenye mguu wake wa kushoto na kuachia shuti lililojaa ubora na kuipa Hispania bao.
MAISHA YA GAMBI
Safari ya Tunkara ilianza katika mazingira tofauti na anayoyaishi sasa. Alizaliwa Gambia ambako alianza kucheza soka kwenye mitaa ya kijiji chao, akitumia magoli yaliyotengenezwa kwa vifaa vya kawaida na kucheza pekupeku pamoja na marafiki zake.
Akiwa na miaka saba, alihama Gambia pamoja na familia yake na kwenda kuishi Hispania, katika eneo la Cerdanyola, mjini Mataró, Catalonia.
Rafiki wa baba yake aliyefahamika kwa jina la Abdul ndiye aliyemsaidia kujiunga na klabu yake ya kwanza, Cerdanyola, ambako alianza kujifunza misingi ya soka la Hispania.
Baadaye kipaji chake kilivutia macho ya Barcelona na mwaka 2021, akiwa na umri wa takribani miaka 11, akajiunga na akademi ya La Masia ambako ameendelea kukuzwa.
Tunkara mwenyewe amewahi kueleza kuwa anathamini uamuzi wa familia yake kuhamia Hispania, akitambua kuwa baba yake alifanya kila aliloweza kuhakikisha watoto wake wanapata maisha bora.
“Nina furaha sana kwa kuja hapa. Baba yangu alifanya kila aliloweza ili kutupatia maisha bora ya baadaye. Familia nzima ilipitia mambo mengi ili kufika hapa,” anasema.
“Nilidhani nitajiunga na timu ya kwanza. Sikuwa na ufahamu wa mambo yote yaliyokuwa yanaendelea.”
TUZO YA ULAYA
Kabla ya kuja Qatar, Tunkara alikuwa tayari amejitengenezea jina katika soka la vijana barani Ulaya baada ya kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano ya UEFA U-17 EURO 2026.
Tuzo hiyo ilithibitisha ubora wake na kuwa miongoni mwa vipaji vinavyong’aa katika kizazi chake, hasa kutokana na uwezo wa kubadilisha kasi ya mashambulizi, kuchezesha wenzake na kufanya maamuzi sahihi akiwa kwenye maeneo yenye presha.
Kocha wa Hispania, David Cubillo, alisema Tunkara amefanya maendeleo makubwa katika eneo la kufanya maamuzi, hasa kuachia mpira mapema badala ya kuendelea kuushikilia wakati wapinzani wanamzonga.
“Katika misimu iliyopita alikuwa na tabia ya kuongeza mguso mmoja wa mpira kabla ya kutoa pasi, lakini sasa hali hiyo imebadilika. Amejifunza kuwa wachezaji watatu wanapomzonga, kuna mwenzake aliye katika nafasi nzuri na anajua namna ya kumpatia mpira,” alisema Cubillo.
“Anazidi kufanya vizuri katika eneo hilo na anatakiwa kuendelea kulifanyia kazi.”
Pamoja na mafanikio hayo, Cubillo amesisitiza kuwa bado anahitaji kuimarisha uwezo wake wa kucheza mipira ya juu na kutumia vizuri nafasi anazopata kwa kichwa.
Uwezo wake wa kutumia mguu wa kushoto tayari umemfanya baadhi ya watu kumlinganisha na Lamine Yamal, lakini Tunkara mara nyingi hucheza katikati ya uwanja katika nafasi ya namba 10.
“Anatakiwa kuendelea kufanya kazi katika mchezo wa mipira ya juu kwa sababu ni mzuri sana katika kupiga vichwa, lakini bado haufanyii kazi uwezo huo ipasavyo. Ni mchezaji bora sana. Bado ni kijana mdogo, ana kipaji kikubwa na ana mchango mkubwa katika timu,”.
Aliongeza: “Ni mtoto mwenye unyenyekevu na anaelewa kuwa soka la kisasa linahitaji mchezaji kufanya vizuri katika pande zote.”