HERE WE GO… Mfahamu Fabrizo Romano
Muktasari:
- Fabrizio ambaye ni mwandishi wa habari za michezo kutoka Italia, huwa hana mpinzani linapokuja suala la habari za usajili za wachezaji barani Ulaya.
ROME, ITALIA: "Here we go! Ni sentensi maarufu sana hususani kwa watu wanaofuatilia mpira wa miguu. Lakini huwa inaaminika sana ikiwa itatokea katika kinywa cha mtu mmoja tu, Fabrizo Romano.
Fabrizio ambaye ni mwandishi wa habari za michezo kutoka Italia, huwa hana mpinzani linapokuja suala la habari za usajili za wachezaji barani Ulaya.
Mwandishi huyu ambaye kwa sasa ana umri miaka 32, ana uzoefu mkubwa na mara zote linapofika dirisha la usajili, mashabiki huwa haiwapiti siku bila ya kuchungulia.
Februari 21, 1993, ndipo alipozaliwa na amefanya kazi katika vyombo vikubwa vya habari, kama Calciomercato, Sky Sports, na The Guardian.
Pia anajulikana kama mwanzilishi wa SOS Fantacalcio, chombo cha habari za michezo kilichoko Italia. Lakini je, anafanyaje kazi na ni nani hasa. Msome hapa.
JINSI ANAVYOFANYA KAZI
Kama waandishi wengine, Fabrizio amekuwa akikabiliwa na changamoto ya kupata taarifa. Hata hivyo, utambulisho wake katika masuala ya uhamisho wa wachezaji unamtenganisha na wengine. Inasemekana Fabrizio huwa analala kwa saa tano tu kati ya saa 24 za kila siku wakati wa dirisha la usajili.
Kwa mujibu wa tovuti ya BR Football, Fabrizio pia ana njia tofauti ya kufanya kazi, ambayo mara nyingine humfanya kuaminika zaidi kuliko waandishi wengine wa habari katika kuripoti masuala ya uhamisho. Fabrizio anaishi na kanuni ya kutafuta jambo kwa polepole na sio kukurupuka. Huhakikisha habari anayoiandika ina uhakika wa asilimia zisizopungua 90.
Anapofanya kazi yake, Fabrizio hupiga walau simu 50 kwa siku kutafuta taarifa za uhamisho.
Mara nyingi pia hutembelea hoteli na makao makuu ya klabu kukutana na mawakala wa wachezaji au wakurugenzi wa michezo.
"Watu huuliza ni timu gani ninayounga mkono. Lakini ninasema sina. Nina furaha ninapoona wachezaji wanahama na naamini hiyo huleta msisimko zaidi kwa watu na mashabiki," anasema Fabrizio.
Twitter ni jukwaa lenye ushawishi mkubwa kwake ikilinganishwa na waandishi wengine wa michezo. Akaunti yake ina wafuasi milioni 23.4.
"Kuwa mwandishi wa habari wa namna hii si rahisi. Watu watauliza habari au kujaribu kuthibitisha baada ya kuona habari kutoka kwa waandishi wengine. Daima huwa naheshimu waandishi wengine. Hivyo basi ninapoulizwa husema tu kile ninachojua. Siwezi kusema habari hiyo ni uongo," anasema Fabrizio.
"Soko la uhamisho limebadilika katika miaka ya hivi karibuni. Zamani, mikutano na watu au mawakala ilifanyika kwa simu. Lakini sasa unaweza kuzungumza kwenye mitandao ya kijamii. Lazima niwe tayari kila wakati."
Sio kila habari anayoitoa basi imetoka kwake. Fabrizo anashirikiana na waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali duniani, pia wamiliki wa timu, mawakala na wachezaji ambao kwa pamoja huwa wanampa taarifa hizi.
Upande wa waandishi wengi wamekuwa wakiuza taarifa kwake lakini kabla ya kuzichukua hujiridhisha kwa asilimia mia.
Mawakala pia humpa taarifa za wachezaji wao wakiamini itawaongezea thamani zaidi.
MTU ALIYEMTOA
Umaridadi na ufundi wa Fabrizio unaoonekana leo pengine usingeonekana bila ya kushikwa mkono na mwalimu wake, Gianluca Di Marzio, mwandishi mkongwe wa Italia aliyejikita katika habari za usajili kabla ya Romano.
Di Marzio ni mtoto wa Gianni Di Marzio, kocha wa soka nchini Italia.
Fabrizo mwenyewe anaeleza kwamba Di Marzio ndiye aliyemfundisha na kumwandaa kuwa mrithi wake na yeye ndio aliyekuwa akimweka karibu na timu mbalimbali za Ulaya.
"Niliaanza yote haya chini ya Gianluca Di Marzio. Alinifundisha mengi," anasema Fabrizio.
"Yeye alikuwa tu hathibitishi taarifa kutoka kwa klabu, bali pia alikuwa akithibitisha kwa mawakala na watu wa mwisho katika uhamisho. Nadhani siri ni kuwa na uhusiano mzuri na kila mtu. Tuna vyanzo vingi kwa sasa."
Kuanzia Agosti hadi Desemba 2019, Fabrizio alikuwa mwandishi wa kwanza kuripoti uhamisho wa Zlatan Ibrahimovic kwenda AC Milan. Alikuwa pia mstari wa mbele katika ripoti za uhamisho wa Carlo Ancelotti kwenda Everton na Claudio Ranieri kwenda Sampdoria.
"Here we go!" Ranieri alisema kabla ya kutangazwa rasmi.
Mei 27, 2018, Fabrizio pia alikuwa mwandishi aliyeshangaza umma wa soka na habari ya Zinedine Zidane kuondoka Real Madrid.
ALIVYOANZA KAZI
Fabrizio alianza kazi yake ya uandishi wa habari akiwa na umri wa miaka 18. Katika umri huo, aliandika kwenye tovuti ndogo za Italia.
Siku moja, wakala mmoja wa Italia aliye Barcelona aliomba msaada kwa Fabrizio juu ya kuandika wachezaji wake. Hapo ndipo alipata nafasi ya kufanya kazi Barcelona, hasa La Masia.
Wakati huo, alijikita katika kuandika habari za uhamisho wa wachezaji chipukizi kutoka La Masia.
Baada ya kufanya hivyo kwa muda, mwaka 2013 ndio alianza kujipatia umaarufu baada ya kutangaza uhamisho wa Mauro Icardi kujiunga na Inter Milan ambaye alitua rasmi mwaka 2014.
Fabrizio alipata habari hii kutokana na ukaribu wake na Icardi kwa wakati huo.
Habari hiyo ilimfanya apenye katika msitu wa waandishi wengine wakubwa na kuanza kujitangaza na baada ya hapo mashabiki waliendelea kumfuatilia na kila siku alizidi kutanua mbawa zake.