Hatari uwanja wa Sh2 trilioni Saudia
Muktasari:
- Uwanja huo wa NEOM, ambao ulipangwa kuwa moja ya alama kuu za michuano hiyo, ulikuwa sehemu ya mradi mkubwa wa The Line, mji wa kisasa wenye urefu wa takribani maili 100, uliojengwa kwa muundo wa chuma na vioo.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SAUDIA Arabia imeanza kukumbana na changamoto kubwa katika maandalizi ya kuandaa Fainali za Kombe la Dunia 2034, huku mpango wa kujenga moja ya viwanja vikubwa na vya kisasa ukionekana kusitishwa.
Uwanja huo wa NEOM, ambao ulipangwa kuwa moja ya alama kuu za michuano hiyo, ulikuwa sehemu ya mradi mkubwa wa The Line, mji wa kisasa wenye urefu wa takribani maili 100, uliojengwa kwa muundo wa chuma na vioo.
Mradi huo uliuzwa kama uwanja wa kipekee wa soka, uliokuwa umeinuliwa juu na kuwa sehemu ya maono makubwa ya Saudi Arabia ya kujenga miundombinu ya kisasa kupitia mpango wake wa Vision 2030.
Hata hivyo, taarifa kutoka jukwaa la ujasusi wa sekta ya ujenzi la MEED, lenye makao yake makuu Dubai, zinaonyesha maendeleo ya uwanja huo yamezuiwa, huku kukiwa hakuna tarehe rasmi ya kukamilika kwa ujenzi huo.
Hali hiyo imezua maswali kuhusu maandalizi ya Saudi Arabia kuelekea michuano hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa uwanja huo ulikuwa miongoni mwa miradi mikubwa na yenye gharama kubwa katika maandalizi ya Kombe la Dunia.
Saudi Arabia ilitangazwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2034 karibu miaka miwili iliyopita, huku michuano hiyo ikiwa ya kwanza kuandaliwa na taifa moja katika mfumo mpya wa timu 48.
Kwa maandalizi hayo, Saudi Arabia imepanga kujenga au kukarabati jumla ya viwanja 15 katika miji mitano, pamoja na vituo kadhaa vya mazoezi.
Uwekezaji wa nchi hiyo katika soka umeongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni kupitia mfuko wake wa utajiri wa taifa, PIF, ambao umetumia fedha nyingi kusajili wachezaji na makocha maarufu duniani pamoja na kuboresha miundombinu ya soka.
Mradi wa NEOM pia unahusishwa na klabu ya Saudi Pro League, NEOM FC, ambayo imewasajili baadhi ya nyota waliowahi kucheza Ligi Kuu England, akiwamo Alexandre Lacazette, Saïd Benrahma na Malang Sarr.
NEOM ilianzishwa kama sehemu muhimu ya maono ya Mwanamfalme Mohammed bin Salman ya kuibadilisha Saudi Arabia kupitia Vision 2030.
Kombe la Dunia 2034, linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo, lakini kusimama kwa mradi wa uwanja wa NEOM kunaweza kuongeza presha kwa waandaaji kuhakikisha viwanja vingine vinakamilika kwa wakati.
Wakati huohuo, Saudi Arabia imeendelea kukabiliwa na changamoto nyingine zinazohusiana na mivutano ya kikanda, huku usumbufu wa miundombinu muhimu na usafirishaji wa nishati ukiongeza gharama na presha kwa taifa hilo.
Kwa sasa, macho yataelekezwa kwenye maendeleo ya viwanja vingine na iwapo Saudi Arabia itaweza kukamilisha maandalizi yake kwa wakati kabla ya michuano hiyo mikubwa ya dunia.