Opah aanza vizuri Saudi Arabia
Muktasari:
- Opah alifunga bao hilo dakika ya 87, wakati AlUla SC ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Neom SC, matokeo yaliyompa mwanadada huyo mwanzo mzuri katika ligi hiyo.
NYOTA wa Tanzania, Opah Clement ameanza vizuri Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia, baada ya kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza akiwa na klabu ya Al Ula SC.
Opah alifunga bao hilo dakika ya 87, wakati AlUla SC ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Neom SC, matokeo yaliyompa mwanadada huyo mwanzo mzuri katika ligi hiyo.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa AlUla SC msimu huu, katika mchezo wao wa kwanza wa ligi kukutana na Qadisiah na kupoteza kwa bao 1-0.
Bao la Opah limeendelea kuthibitisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vipaji na wachezaji wazuri wanaoweza kushindana kwenye ligi mbalimbali duniani.
Hadi sasa Saudia ina wachezaji wawili wanaokipiga kwenye Ligi Kuu ya Wanawake, Julietha Singano anayekipiga Al Nassr na Opah wa Al Ula.
Kabla ya wachezaji hao waliojiunga na timu hizo msimu huu, mshambuliaji Clara Luvanga alikuwa mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa kwenye kikosi cha Al Nassr.
Aliisaidia.timu hiyo kubeba mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu na kuibuka mfungaji bora msimu uliopita akifunga mabao 24.
Baada ya michezo miwili, AlUla SC imefikisha pointi tatu na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, huku baadhi ya timu zikiwa bado hazijacheza idadi sawa ya michezo.
Mbali na Opah nyota mwingine wa Tanzania aliofanya vizuri wikiendi ni Enekia Lunyamila ambaye anakipiga Queretaro alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 6-2.