Harry Kane awatuliza mashabiki Bayern, asema maisha yaendelee
Muktasari:
- Arsenal ilionyesha ubora na nidhamu ya hali ya juu, ikitawala sehemu kubwa ya mechi hiyo na kupata ushindi wa mabao 3-1 uliowapa nguvu katika mbio za ubingwa msimu huu.
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, amesema hakuna sababu ya kuingiwa na hofu licha ya timu hiyo kupata kichapo cha kwanza msimu huu kutoka kwa Arsenal katika mechi iliyochezwa usiku wa jana Jumatano, Novemba 26, 2025.
Arsenal ilionyesha ubora na nidhamu ya hali ya juu, ikitawala sehemu kubwa ya mechi hiyo na kupata ushindi wa mabao 3-1 uliowapa nguvu katika mbio za ubingwa msimu huu.
Mabao mawili yaliyowekwa kimiani katika kipindi cha pili, yaliwapa The Gunners alama tatu dhidi ya mabingwa hao wa Ujerumani baada ya kipindi cha kwanza matokeo kuwa 1-1.
Mshambuliaji huyo wa England, amesema matokeo dhidi ya Arsenal hayajabadilisha malengo ya Bayern msimu huu, hivyo wanajipanga kwa mechi zijazo ambazo wanaamini watafanya vizuri na kupata ushindi.
Amesema malengo yao ya kusaka mafanikio bado yapo wazi, na kupoteza mechi hiyo ya jana haijawapotezea ramani ya ubingwa wa Ulaya ambao wamejipanga kuuchukua msimu huu kutokana na mipango waliyojiwekea.
“Hakuna wasiwasi. Ni mechi moja tu. Tunajua tunaweza kucheza vizuri zaidi, na tutarejea kwa nguvu,” amesema nyota huyo wa England.
“Tumedhamiria kutwaa ubingwa wa Ulaya msimu huu, safari bado ipo wazi tena kwa mafanikio makubwa. Kupoteza mechi ni sehemu ya mapambano, hilo tunalijua na ndio maana wachezaji wa Bayern tunaendelea kuhimizana kila wakati ili kufikia malengo tuliojiwekea.” ameongeza Kane
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amekisifia kikosi chake kwa kuonyesha ustahimilivu na ubunifu licha ya presha kubwa ya Bayern.
“Tumepambana na timu kubwa na bora barani Ulaya. Wachezaji wangu wameonyesha ujasiri mkubwa na kutekeleza mpango wetu vizuri,” amesema Arteta.
Ushindi huo unaipa Arsenal motisha kubwa katika kampeni ya kusaka mafanikio msimu huu 2025-2026, huku Bayern ikiahidi kurekebisha makosa kabla ya mechi ijayo.