Harry Kane afurahia maisha Bayern, atuma salamu Arsenal
Muktasari:
- Kane raia wa England, amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akionyesha mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao wa Bundesliga.
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, amesema anafurahia majukumu mapya aliyopewa katika kikosi hicho tangu alipotua klabuni hapo msimu uliopita.
Kane raia wa England, amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akionyesha mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao wa Bundesliga.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 32, amesema mfumo wa Bayern Munich unamruhusu kucheza kwa uhuru zaidi, jambo ambalo limeimarisha uwezo wake wa kufunga mabao kwa kusaidiana na wachezaji wenzake. Amedai kuwa kuzoea maisha ya klabuni hapo na mbinu za kocha Vincent Kompany, kumemsaidia kuonyesha ubora wake.
Akizungumzia mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal, Kane amesema kikosi chao kipo tayari kwa mechi hiyo itakayopigwa kesho Jumatano, Novemba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Emirates jijini London.
Amesema anaiheshimu Arsenal ambayo kwa sasa ina kiwango bora cha ushindani lakini anaamini Bayern ina uwezo wa kupambana na timu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi ya EPL.
Arsenal imeshacheza mechi nne za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Ushindi wa kwanza ulipatikana dhidi ya Athletic Club wa mabao 2–0 ugenini. Ushindi mwingine muhimu ulikuwa dhidi ya Olympiacos, ambapo Arsenal ilicheza kwa utulivu na kushinda 2–0 nyumbani.
Timu hiyo inayonolewa na kocha Mikel Arteta, pia iliiadhibu Atlético Madrid kwa kuichapa 4–0 na ushindi wa nne ulipatikana dhidi ya Slavia Praha, ikishinda 3–0 ugenini, na kuimarisha nafasi yao kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Ulaya.
Kwa upande wa Bayern Munich, imeshinda mechi nne za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, ikianza kuifunga Chelsea 3-1 nyumbani, kisha ikaitandika Pafos FC mabao 5–1 ugenini. Mechi nyingine ilikuwa nyumbani dhidi ya Club Brugge, ambapo Bayern ilitoa kichapo kikali cha 4–0. Vilevile ikaibuka na ushindi wa 2–1 ugenini dhidi ya Paris Saint-Germain, licha ya changamoto ya kucheza ikiwa pungufu.