Harry Kane afunguka kurudi England
Muktasari:
- Kane, ambaye aliwahi kuchezea Tottenham Hotspur, bado ana miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa, lakini Bayern Munich tayari imeonyesha nia ya kumwongezea mkataba wakati huu na anahusishwa na timu kibao.
LONDON, ENGLAND: KAPTENI wa timu ya taifa ya England, Harry Kane, 32, amefuta tetesi za kutaka kurejea tena England na kusisitiza yupo tayari kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia.
Kane, ambaye aliwahi kuchezea Tottenham Hotspur, bado ana miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa, lakini Bayern Munich tayari imeonyesha nia ya kumwongezea mkataba wakati huu na anahusishwa na timu kibao.
Katika mkataba wake kuna kifungu maalum kinachomruhusu kuondoka mwisho wa msimu huu kwa dau la Pauni 56.7 milioni na Tottenham ina chaguo la kumsajili tena ikiwa itahitaji kufanya hivyo,
Nyota huyo wa Bayern, ambaye alitwaa taji la Bundesliga msimu uliopita, kwa msimu huu tayari amefunga mabao 19 kwa timu yake hiyo na England.
Akizungumzia tetesi za kuondoka Kane amesema: "Kuhusu kubaki hapa muda mrefu zaidi? Ndiyo, hili lipo na linaweza likatokea kwa asilimia kubwa. Sijazungumza na Bayern kuhusu hilo kwa sasa, lakini kama mazungumzo hayo yataanza, niko tayari kubaki hapa. Kwa sasa tunapitia kipindi kizuri sana, kwa hiyo sifikirii kuondoka, kuhusu kurudi Ligi Kuu England, sijui. Kama ungeliniuliza mara tu baada ya kujiunga na Bayern, ningesema kweli nataka kurudi, lakini sasa nimekaa hapa kwa miaka michache, mawazo hayo yamepungua kichwani mwangu, lakini siwezi kusema sitarudi kabisa."
"Nimejifunza katika soka fursa na nyakati hubadilika, na mambo huja kwa mpangilio wake. Kwa sasa, mimi niko Bayern na nitaipambani kwa nguvu zangu zote."
"Kama kutakuwa na mazungumzo ya kuongeza mkataba, tutaona, lakini bado nina mkataba wa kuwa hapa kwa msimu huu na mwingine mbele. Kwa hiyo hakuna presha wala haraka."