Haaland ajiachia kwa vigogo wa Hispania
Muktasari:
- Mchezaji huyo anaelezwa tayari ameshafanya uamuzi mara tu hukumu itakapotolewa dhidi ya Man City, ataangukia katika mojawapo wa timu hizo mbili.
KUTOKANA na kuvutiwa naye kwa kiasi kikubwa kutoka karibu nusu ya nchi za Ulaya, Erling Haaland amepunguza machaguo yake iwapo ataondoka Manchester City na kubaki na timu mbili pekee, Real Madrid au Barcelona.
Mchezaji huyo anaelezwa tayari ameshafanya uamuzi mara tu hukumu itakapotolewa dhidi ya Man City, ataangukia katika mojawapo wa timu hizo mbili.
Awali, Manchester United, Inter Milan, Bayern Munich na PSG zilikuwa miongoni mwa zile zinazomtaka mchezaji huyo ambaye analipwa mkwanja mrefu kuliko mastaa wote katika Ligi Kuu England.
Haaland hajatoa kauli yoyote hadharani kuhusiana na kesi dhidi ya Man City, lakini watu wake wa karibu wamekuwa wakihangaika kusaka mustakabali nje ya timu hiyo.
Mchezaji huyo alisaini mkataba mpya Man City miaka miwili iliyopita unaomshuhudia akikunja Pauni 525,000 kwa wiki hadi mwaka 2030, huku timu inayomtaka ikitakiwa kulipa Pauni 170 milioni.
Haaland amekuwa na kiwango bora tangu atue Man City akitokea Borrusia Dortmund akiisaidia kubabe mataji makuba ya Uya na England.
Mchango wake wa mabao umezifanya klabu nyingi kubwa Ulaya kuiwinda saini yake bila mafanikio lakini sasa mpango wake ni kuondoka kama City itahukumiwa.
Benjamin Sesko
KUVUTIWA na Benjamin Sesko kutoka Juventus na Barcelona kumeifanya Manchester United kuweka bei ya kumuuza kuwa Pauni 64 milioni, jambo ambalo litamaanisha itapata hasara ikilinganishwa na kiasi ilicholipa kumsajili zaidi ya mwaka mmoja uliopita ilipolipa Pauni 73.7 milioni.
Micky van de Ven
MANCHESTER United iko tayari kushindana na Liverpool katika usajili wa Micky van de Ven, ingawa Tottenham Hotspur haijaonyesha nia ya kumuuza mchezaji huyo. Vilevile uwezekano wa Van de Ven kuhama Januari unaonekana kuwa mdogo sana.
Fermin Lopez
KOCHA Xabi Alonso ametoa idhini kwa uongozi kuendelea na mpango wa kutoa ofa ya Pauni 103.1 milioni kwa ajili ya nyota wa Barcelona, Fermin Lopez, ambapo Januari anatajwa kuuzwa.
Michael Kayode
LIVERPOOL imeamua kumtolea macho beki wa kulia wa Brentford, Michael Kayode, kama mchezaji kipaumbele chake katika kuimarisha safu ya ulinzi mwakani. Hata hivyo, itakabiliwa na ushindani kutoka kwa Arsenal na Tottenham Hotspur.
Jules Kounde
CHELSEA inafikiria kumsajili beki wa kulia wa Barcelona, Jules Kounde, ambaye anakabiliana na ushindani wa namba katika kikosi chake, jambo ambalo limemfanya kuanza kuonja benchi msimu huu.
Murillo Santiago
LIVERPOOL na Chelsea zinadaiwa kuwasiliana na watu wa karibu wa beki wa kati wa Nottingham Forest ili kuweka mambo sawa kwa ajili ya usajili wa dirisha kubwa lijalo, mwakani.
Mateo Kovacic
JUVENTUS inafuatilia kwa karibu mustakabali wa Mateo Kovacic kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu maisha yake ya baadaye ndani ya kikosi cha Manchester City. Mara nyingi msimu huu Kovacic amekuwa akiingia kutokea benchi.
Kim Min-jae
TOTTENHAM Hotspur imeibuka kwa kushtukiza katika mbio za kumsajili beki wa kati wa Bayern Munich, Kim Min-jae, ambaye kwa sasa hana uhakika wa kuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo ya Ujerumani.
Nico Williams
INADAIWA Athletic Club inapata ugumu wa kumudu mshahara mkubwa wa Nico Williams na inaweza kulazimika kukabiliana na changamoto ya kifedha kwa kumuuza mchezaji huyo anayefukuziwa na Manchester United.