Haaland aanza kulalamikiwa kwa kukata nywele
Muktasari:
- Haaland mwenye miaka 26, alionekana na mtindo mpya wa nywele ndogo katika mchezo huo wa Ligi Kuu England, baada ya kukata nywele zake ndefu zilizokuwa sehemu ya muonekano wake maarufu.
MANCHESTER, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Erling Haaland amekumbana na kejeli kutoka kwa mashabiki baada ya kushindwa kufunga katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth, huku baadhi wakidai amepoteza “nguvu” zake baada ya kukata nywele.
Haaland mwenye miaka 26, alionekana na mtindo mpya wa nywele ndogo katika mchezo huo wa Ligi Kuu England, baada ya kukata nywele zake ndefu zilizokuwa sehemu ya muonekano wake maarufu.
City ililazimika kufanya kazi ya ziada kupata ushindi huo baada ya Bournemouth kuanza kwa bao, kabla ya Marc Guehi na Josko Gvardiol kufunga mabao ya kusawazisha na kuipa timu hiyo pointi zote tatu.
Haaland alipata nafasi nzuri katika kipindi cha kwanza, lakini alishindwa kuitumia na kumaliza mchezo bila kufunga, katika kile kilichoonekana kuwa moja ya mechi zake alizocheza kwa kiwango cha chini.
Baada ya mchezo huo, mashabiki walimiminika kwenye mitandao ya kijamii wakimtaka mshambuliaji huyo arejeshe nywele zake za zamani, wakidai kukata nywele kulimfanya apoteze uwezo wake wa kufunga mabao.
Shabiki mmoja aliandika: “Kama Rapunzel, Haaland amepoteza nguvu zake baada ya kukata nywele.”
Mwingine amesema: “Haaland anahitaji kurudisha nywele hizo haraka. Uchezaji huu haukuwa mzuri.”
Shabiki mwingine aliongeza: “Haaland amepoteza nguvu zake kwa kukata nywele.”
Katika mchezo huo, Haaland alipiga mashuti matano, mawili pekee yakilenga lango, kabla ya City kubadili matokeo na kuibuka na ushindi.
ZLATAN AMCHEKA HAALAND
Kabla ya mchezo huo, Haaland alishirikisha video ikionyesha baadhi ya watu maarufu wakitoa maoni yao kuhusu muonekano wake mpya.
Nyota wa zamani wa Oasis, Noel Gallagher, kocha wa zamani wa City, Pep Guardiola, na mchezaji mwenzake Jack Grealish walikuwa miongoni mwa waliouona mtindo huo mpya kupitia FaceTime.
Hata hivyo, aliyemcheka zaidi alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic.
Baada ya kumpigia simu Haaland, Zlatan alishangaa na kusema: “Umefanya nini? Hii ni nini? Umepoteza dau au nini? Nizuie na ufute namba yangu.”
Haaland aliwahi kueleza kwamba Zlatan alishawahi kumwonya asikate nywele zake, akiamini kuwa nguvu zake zilikuwa ndani ya nywele hizo.
Mshambuliaji huyo wa City amesema Zlatan alimwambia: “Usikate kamwe nywele zako kwa sababu nguvu iko kwenye nywele.”
Uchezaji huo usioridhisha wa Haaland ulianza tangu walipofunga katika kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Arsenal kwenye Ngao ya Jamii wiki iliyopita.
Sasa Haaland atakuwa na kazi ya kurejesha makali yake ya kufunga mabao wakati Manchester City itakapokutana na Crystal Palace Ijumaa.