Wabongo wanavyotikisa Uarabuni
Muktasari:
- Safari hiyo haijaja kwa bahati, bali imechangiwa na viwango ambavyo wachezaji hao wamekuwa wakivionyesha katika klabu zao na timu ya Taifa ya Tanzania, Twiga Stars.
HIVI karibuni kumekuwa na ongezeko la wachezaji wa kike kutoka Tanzania wanaokwenda kucheza nje ya nchi, hasa katika Ligi Kuu ya Wanawake Uturuki, ambayo ni miongoni mwa ligi zenye ushindani mkubwa Ulaya.
Safari hiyo haijaja kwa bahati, bali imechangiwa na viwango ambavyo wachezaji hao wamekuwa wakivionyesha katika klabu zao na timu ya Taifa ya Tanzania, Twiga Stars.
Ubora huo umeanza kuzivutia klabu za nje, ambazo sasa zimekuwa zikifuatilia vipaji vya Tanzania na kuwapa nafasi ya kucheza katika ligi mbalimbali. Baadhi yao wamepiga hatua kubwa na kujenga majina nje ya nchi, huku wengine wakiwa bado wanaendelea kutengeneza njia kwa kizazi kijacho.
OPAH CLEMENT
Miongoni mwa wachezaji waliocheza Uturuki ni mshambuliaji Opah Clement, ambaye kwa sasa anakipiga SD Eibar inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Hispania. Ni Mtanzania wa kwanza kuweka rekodi ya kusajiliwa na kucheza ligi hiyo upande wa wanawake.
Akiwa Uturuki aliwahi pia kuichezea Beşiktaş kabla ya kutolewa kwa mkopo Kayseri Kadın wa miezi sita. Katika kipindi hicho alicheza mechi 10 na kufunga mabao matano, akionyesha uwezo wake wa kuitengenezea timu nafasi za kufunga na kumalizia nafasi anazopata.
Msimu wa 2023/24 alirejea Beşiktaş kwa mkopo akitokea Simba Queens, akicheza mechi 11 na kufunga mabao sita. Takwimu hizo zinaonyesha namna mshambuliaji huyo alivyoendelea kuwa na mchango mkubwa kila alipopata nafasi ya kucheza.
DIANA MSEWA
Msewa ni jina lingine la Mtanzania ambalo limeendelea kufanya vizuri Uturuki. Kiungo huyo anayeichezea Trabzonspor si mgeni katika ligi hiyo, kwani amekuwa na kiwango kizuri tangu alipojiunga na klabu hiyo msimu wa 2024/25.
Kabla ya Trabzonspor, Msewa aliwahi kuichezea Amed SK, pia ya Uturuki, ambako alicheza mechi 25 na kufunga mabao manane.
Baada ya kuhamia Trabzonspor, aliendelea na kasi hiyo. Katika msimu wake wa kwanza alicheza mechi 27 na kufunga mabao tisa, akithibitisha uwezo wake.
Pia amekuwa na mchango mkubwa Twiga Stars, jambo linaloonyesha kiwango chake cha klabu kimekuwa kikimsaidia pia anapovaa jezi ya Taifa.
NOELA LUHALA
Kabla ya kuanza safari yake katika ligi za nje, Luhala alijitengenezea jina akiwa Yanga Princess. Beki huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa na nafasi katika kikosi hicho kutokana na kiwango chake na uwezo wa kucheza kwa kujiamini.
Beki huyo alicheza nchi mbalimbali ikiwemo Israel na Lithuania. Lakini kabla ya kwenda huko, aliwahi kucheza Uturuki katika klabu ya 1207 Antalya Spor.
Licha ya kukaa kwa muda mfupi, Noela alipata nafasi ya kuonyesha uwezo wake. Alidumu katika klabu hiyo kwa takribani miezi minne kabla ya kuvunja mkataba na kuhamia MFA Žalgiris ya Lithuania.
Akiwa Antalya Spor, alicheza mechi 12 za ligi na kufunga bao moja. Hiyo ilikuwa hatua nyingine muhimu katika safari yake ya kucheza soka nje ya Tanzania.
NASMA MANDUTA
Inaelezwa kiungo huyo yuko njiani kujiunga na Antalya Spor. Manduta kabla ya hapo amewahi kucheza Yanga Princess, Baobab Queens na Ceasiaa Queens.
Iwapo dili hilo litakamilika, Manduta atakuwa Mtanzania mwingine kucheza Ligi Kuu ya Wanawake Uturuki.
Kwa mchezaji kama Manduta, hatua hiyo inaweza kuwa kubwa katika kuendeleza kipaji chake, pia inaweza kuwa nafasi nyingine kwa Tanzania kuendelea kuonyesha ina wachezaji wenye uwezo wa kushindana nje ya mipaka ya Afrika.
CLARA LUVANGA
Hata hivyo, safari ya wachezaji wa Tanzania nje ya nchi haijaishia Uturuki. Clara Luvanga ni mfano mwingine wa Mtanzania ambaye amefanya vizuri katika nchi za Kiarabu.
Luvanga kwa sasa anaitumikia Al Nassr ya Saudi Arabia na huu ni msimu wake wa nne tangu alipojiunga na klabu hiyo msimu wa 2023/24 akitokea DUX Logroño ya Hispania.
Msimu wake wa kwanza Saudi Arabia alicheza mechi 18, akifunga mabao 11 na kutoa asisti saba. Msimu uliofuata aliendelea kuwa moto zaidi baada ya kufunga mabao 21 na kutoa asisti saba.
Msimu uliopita alimaliza mfungaji bora akifunga mabao 24. Mafanikio hayo yalimfanya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo ya mfungaji bora katika ligi hiyo.
ENEKIA LUNYAMILA
Lunyamila ni miongoni mwa nyota wengine waliocheza kwa mafanikio katika ligi hizo. Kabla ya kwenda Saudi Arabia, alicheza Morocco AUSF Assa-Zag ya Morocco msimu wa 2021/22.
Akiwa Morocco, Lunyamila alikuwa na msimu mzuri baada ya kufunga mabao 49 katika mechi 41, takwimu zilizoonyesha uwezo wake mkubwa wa kufunga.
Baadaye alihamia Saudi Arabia na msimu wa 2023/24 akaichezea Eastern Flames. Katika klabu hiyo alicheza mechi 14 na kufunga mabao nane.
Haya yote yanaonyesha soka la wanawake Tanzania limeanza kukua. Kutoka Opah, Diana na Noela waliopita Uturuki, hadi Clara anayeng'ara Saudi Arabia na Enekia aliyefanya vizuri Morocco na Saudi Arabia, wachezaji wa Tanzania wameendelea kujenga jina la nchi katika soka la wanawake.
Kinachobaki sasa ni kuendelea kuzalisha vipaji, kuvipa mazingira bora na kuhakikisha wachezaji wanaopata nafasi ya kwenda nje wanatumia fursa hizo vizuri.