Guendouzi achafua hali ya hewa Ufaransa
Muktasari:
- Tukio hilo lilianza baada ya kiungo wa Fenerbahce, Matteo Guendouzi, kuwabeza mashabiki wa Lyon kwa kufanya ishara za kejeli huku pia akisisitiza kuisifia klabu yake ya zamani, Marseille, ambayo ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa Lyon nchini Ufaransa.
LYON, UFARANSA: Vurugu kubwa zilitokea kwenye Uwanja wa Groupama nchini Ufaransa baada ya Fenerbahçe kuitandika Lyon mabao 2-1 na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa jumla wa 3-2.
Tukio hilo lilianza baada ya kiungo wa Fenerbahce, Matteo Guendouzi, kuwabeza mashabiki wa Lyon kwa kufanya ishara za kejeli huku pia akisisitiza kuisifia klabu yake ya zamani, Marseille, ambayo ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa Lyon nchini Ufaransa.
Kitendo hicho kiliwachochea mashabiki wa Lyon, hali iliyosababisha mzozo mkubwa ndani ya uwanja. Kocha wa makipa wa Lyon aliripotiwa kumpiga teke Guendouzi, kabla ya mashabiki kuvamia uwanja na wachezaji wa timu zote mbili kuanza kusukumana na kupigana.
Kutokana na vurugu hizo, Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) linatarajiwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya timu na watu waliohusika, huku tukio hilo likitishia kugharimu baadhi ya wahusika adhabu kali.
Licha ya vurugu hizo, ushindi huo ni wa kihistoria kwa Fenerbahçe, ambao wamefanikiwa kuvunja ukame wa miaka 18 bila kufuzu hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa, na kurejea kwenye jukwaa kubwa la soka la Ulaya msimu wa 2026/27.
MATOKEO MENGINE YA LIGI YA MABINGWA
AEK Athens 4-0 Levski Sofia
AEK Athens imefuzu kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya mchezo wa kwanza kumalizika kwa suluhu.
Viking FK 3-1 Dinamo Zagreb
Viking FK imefuzu kwa jumla ya mabao 5-3 baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini.
Slovan Bratislava 2-1 NK Celje
Mchezo huo ulihitaji muda wa ziada baada ya timu hizo kutoshana nguvu. Slovan Bratislava ilifuzu kwa jumla ya mabao 3-2, kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza.
Sabah FK 5-2 Hapoel Beer-Sheva
Sabah FK imefuzu kwa jumla ya mabao 6-4 baada ya kupindua meza, ambao ilipoteza kwa mabao 2-1 mechi ya kwanza.
Bodø/Glimt 3-0 NEC Nijmegen
Bodø/Glimt imeonyesha ubabe na kufuzu kwa jumla ya mabao 6-1.
LASK 5-1 Celtic
LASK imepindua meza kibabe baada ya kupoteza 3-0 katika mchezo wa kwanza. Ilishinda 5-1 baada ya dakika 120 na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-4.