Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 15 imetosha Stars, TFF yatoa tamko

Muktasari:

  • Uamuzi huo wa Samatta umechukuliwa kwa sura tofauti na wadau mbalimbali wakiwemo mastaa wanaocheza soka hivi sasa na wale waliotangulia, huku upande wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), likisema litamuita na kumsikiliza hoja zake za msingi kwani bado anahitajika kikosini.

NAHODHA na mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania maarufu Taifa Stars, Mbwana Samatta, ametangaza rasmi kustaafu kuichezea timu hiyo baada ya kuitumikia kwa takribani miaka 15.

Uamuzi huo wa Samatta umechukuliwa kwa sura tofauti na wadau mbalimbali wakiwemo mastaa wanaocheza soka hivi sasa na wale waliotangulia, huku upande wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), likisema litamuita na kumsikiliza hoja zake za msingi kwani bado anahitajika kikosini.

Wakati anatangaza kustaafu, Samatta amebainisha kuwa, uamuzi huo umekuja baada ya kutafakari kwa kina na anaamini sasa ni wakati wa kutoa nafasi kwa vipaji vipya kuifikisha timu katika hatua za juu zaidi.

Katika barua yake aliyoichapisha Julai 7, 2026 kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Samatta ameeleza kwamba amekuwa sehemu ya timu ya taifa kwa takribani miaka 15, huku akiwaongoza wachezaji wenzake kama nahodha kwa miaka 10.

"Baada ya kutafakari kwa kina, ninatangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu yangu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kuanzia leo.

"Ulikuwa wakati mzuri na wa kipekee katika maisha yangu kuwa mchezaji wa Timu ya Taifa kwa takribani miaka 15 na najisikia fahari kusema nashukuru kwa nafasi hii.

"Miaka 10 ya kuwaongoza wachezaji wenzangu kama nahodha wa Taifa Stars imekuwa yenye alama kubwa katika maisha yangu ikiwemo kufuzu fainali za AFCON mara tatu (3) na kutimiza ndoto ya muda mrefu ya kuweka historia ya kuingia hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza. Naamini huu ni wakati wa vipaji vipya kupewa nafasi ya kutufikisha kwenye hatua za juu zaidi.

"Ilikuwa safari njema iliyojaa nyakati zisizosahaulika na zenye hisia mchanganyiko, naishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwa kuhakikisha timu ya taifa ya Tanzania inakuwa tamanio na ndoto ya kila mchezaji.

"Shukrani za kipekee pia ziende kwa familia yangu, wachezaji wenzangu, rafiki zangu, wadau wa Taifa Stars na Watanzania wenzangu kwa kunionesha upendo na kuiunga mkono timu hii katika nyakati zote za furaha na huzuni.

"Nikijivunia Utanzania wangu, naahidi kuendelea kutoa mchango wangu kwa timu ya Taifa katika maeneo mengine yaliyo ndani ya uwezo na uzoefu wangu," amesema Samatta.

Moja ya mafanikio makubwa ya Samatta katika kuiongoza Taifa Stars ni kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mara tatu, pamoja na kuweka historia ya kuifikisha timu hiyo hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza AFCON 2025.

Samatta alianza kuitumikia Taifa Stars mwaka 2011, hadi anatangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo, amefunga mabao 22 katika mechi 87.

Bao lake la kwanza alifunga Machi 26, 2011 katika mechi ya kufuzu AFCON 2012 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku pia bao la 22 akilifunga dhidi ya mpinzani huyo uwanjani hapo tena mwezi kama ule, tofauti tarehe na mwaka. Safari hii ilikuwa Machi 23, 2022 ikiwa mechi ya kirafiki.

Nyota huyo anayeitumikia klabu Le Havre inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa, amekuwa mchezaji anayetazamwa zaidi na wanasoka wengi wa Kitanzania kutokana na safari yake kuanzia Tanzania hadi barani Ulaya.

Samatta aliyeanza kucheza Ligi Kuu Bara katika kikosi cha African Lyon kisha Simba SC zote za Dar es Salaam, 2011 alihamia TP Mazembe ya DR Congo ambayo ilimfungulia milango ya kwenda Ulaya mwaka 2016 akitua Ubelgiji akijiunga na KRC Genk. Pia amecheza Royal Antwerp ya hapo Ubelgiji.

Mwaka 2020, aliweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England aliposajiliwa na Aston Villa. Pia amecheza Fenerbahçe ya Uturuki na PAOK ya Ugiriki kabla ya 2025 kusajiliwa Le Havre.

Samatta amechukua uamuzi huo mwaka mmoja kabla ya Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON, fainali zitakazofanyika Juni 2027, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Uamuzi huo wa Samatta umekuja baada ya Juni 6, 2024 Mwanaspoti kuripoti kwamba TFF ilimkaushia mshambuliaji huyo katika ombi lake la kujiweka kando kufuatia barua aliyoiwasilisha katika shirikisho hilo.


MSIKIE KARIA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, akizungumzia uamuzi wa Samatta kustaafu amesema: “Nimeshtushwa. Samatta sio mara ya kwanza, alishaomba, aliandika barua mimi nikaikataa, kabla ya Afcon iliyofanyika Morocco kwa sababu bado tunamuhitaji.

“Samatta alichukua unahodha kutoka kwa Nadir Haroub ‘Canavaro’, tutaongea naye kujua sababu zake za msingi, tutamsikiliza lakini hatutaacha kumshawishi aendelee kucheza. Hayo mambo mengine Samatta ameshapevuka.

“Wakati yupo kijana alipata kelele kelele akiwa na mwenzake Ulimwengu (Thomas), lakini akapita katika kipindi kile akiwa kijana na akasimama. Alishakuwa mchezaji bora wa Afrika, bado ana heshima yake.”


ANAVYOZUNGUMZWA

Mwanaspoti limefanya mahojiano na mastaa wa zamani na sasa kuhusiana na uamuzi huo ambapo wamemzungumzia Samatta namna anavyoweza kuwa chachu ya wengine kufanya vizuri endapo akitumiwa ipasavyo na kwa  heshima.

Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, amesema Samatta amefanya maamuzi sahihi na kwa wakati sahihi kujiondoa mwenyewe kabla ya kulazimishwa.

"Mashabiki wa mpira wa miguu hawana shukrani, mchezaji anaweza akakosea kidogo uwanjani, basi wanasahau mema yote aliyoyafanya wanaanza kumzomea, nampongeza Samatta amekuwa kijana mwelevu aliyechagua kulinda heshima yake," amesema Mogella na kuongeza;

"Ombi langu kwa TFF mchezaji kama Samatta ambaye amecheza nje kwa takribani miaka 16 mfululizo bila kurudi nyumbani, inapaswa kumsogeza kwa heshima katika benchi la ufundi na kuwa mshauri wa vijana ili madini yake yalifae taifa na siyo kumuacha aende zake."

Kauli yake imekwenda sambamba na ya mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi aliyesema: "Samatta ameacha somo kwa vijana wengine ambao wataendelea kuitumikia timu ya Taifa, ombi langu kwa madini aliyopata nje, basi TFF imuweke karibu kwa majukumu mengine ya kuwasaidia vijana."

Kiraka Erasto Nyoni ni kati ya mastaa waliyoitumikia timu ya taifa kwa muda mrefu, amezungumzia kustaafu kwa Samatta katika majukumu hayo akisema: "Samatta ameuheshimu mpira wa miguu na wenyewe umemrudishia heshima yake, hilo ni somo kwa vijana, mtu kuwa nahodha miaka 10 maana yake TFF iliona kitu kwake, kucheza takribani miaka 15 maana yake ana nidhamu na anajitunza."

Nyota wa Patro Eisden ya Ubelgiji, Haji Mnoga ambaye awali alikuwa Salford City ya England, amesema: "Kati ya watu waliokuwa msaada mkubwa wa mimi kufanya uamuzi wa kuichezea timu ya taifa ya Tanzania, miongoni mwao ni Samatta, anaipenda sana nchi yake, ameacha legasi kubwa kwa vijana kuiga nidhamu yake ya kazi na uongozi bora kwa wachezaji wenzake."

Kwa upande wa Simon Msuva, amesema Samatta amefanya vitu vikubwa vitakavyokumbukwa katika historia ya vitabu vya soka, akisisitiza vijana kumtumia vizuri kupata vitu vya kuwaongoza.

"Milango kwa wachezaji vijana kujifunza kwa Samatta ipo wazi, ni wao wenyewe kumtumia vizuri pia naamini hata taifa lenyewe litamtumia kwa manufaa mapana, nje alikocheza muda mrefu kajifunza vitu vingi vinavyoweza kuwafaa wengine," amesema.

Kiungo mshambuliaji Bakari Msimu anayetajwa kujiunga na Simba baada ya kufanya vizuri akiwa Coastal Union ya Tanga, amesema: "Samatta ni ‘aikoni’ kwa vijana tulio wengi, binafsi naheshimu mchango wake katika timu ya taifa na uchezaji wake katika klabu mbalimbali kwa ujumla."

Staa wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya ambaye msimu uliyoisha aliichezea Coastal Union, amesema: "Kucheza kwa kiwango ndani ya miaka 15 ni kitu ambacho kimewashinda wachezaji wengi hata katika timu zao, kusema ukweli Samatta anastahili heshima ya kipekee.”

Ameongeza: "Nimewahi kukutana naye katika majukumu ya timu ya taifa mara nyingi kipindi cha nyuma, nilijifunza jinsi anavyoheshimu muda, kaacha somo kubwa kwa vijana wengine ambao wanahitaji kufika mbali."

KAULI YA FAMILIA

Kaka mkubwa wa staa huyo, Rajabu Samatta amesema hawajashangaa kuona anafanya uamuzi huo, kwani anawapisha na wengine kulitumikia taifa lao.

"Kwanza ameiheshimisha familia lakini ni muda wake wa kutazama maisha yake ya mbele, huu mpira usipokuwa na akili unaweza ukapata umaarufu mkubwa halafu baadaye ukawa na maisha mabovu, hilo Mbwana kaliwaza mapema.

"Mbwana ni mtu anayependa ushauri, naamini ameshauriwa vitu vingi kabla ya uamuzi wake na makocha na wadau mbalimbali, kucheza kwa takribani miaka 15 siyo jambo jepesi, lakini inaonyesha wazi alijitunza.

"Kipekee kama familia tunamshukuru kocha Boniface Mkwasa ndiye aliyemwamini Mbwana kumpa unahodha na Mkwasa alifundishwa na mzee wetu mpira wa miguu, familia yetu ni soka, mimi nimechezea timu za Polisi Tanga, Mbeya, Shinyanga, kwa sababu mzee alikuwa anafanya kazi hiyo hakutaka nijikite zaidi na kazi hiyo, badala yake alitaka nisome, hivyo nikajikita katika elimu."