GUARDIOLA: Hii Man City bado sana
Muktasari:
- Man City ambayo wikiendi iliyopita ilishinda mabao 4-1 dhidi ya West Ham, kabla ya hapo ilishinda mbele ya Leicester City ambao ulikuwa ni mchezo wao wa kwanza kushinda baada ya mechi tano, pia ulikuwa ni ushindi wa pili tangu Oktoba mwaka jana.
MANCHESTER, ENGLAND: LICHA ya kushinda mechi mbili mfululizo, kocha wa wa Manchester City Pep Guardiola amesema bado timu yake inacheza chini ya kiwango tofauti na vile ambavyo yeye anahitaji.
Man City ambayo wikiendi iliyopita ilishinda mabao 4-1 dhidi ya West Ham, kabla ya hapo ilishinda mbele ya Leicester City ambao ulikuwa ni mchezo wao wa kwanza kushinda baada ya mechi tano, pia ulikuwa ni ushindi wa pili tangu Oktoba mwaka jana.
Pia ushindi huo uliisogeza hadi nafasi ya sita ikizidi kukaribia zile nafasi nne za juu kwa sasa ikiwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 20.
Guardiola amesema bado hajaona kile alichokitarajia na wana safari ndefu kufikia ubora wao unaojulikana.
“Tumeona kwa miaka mingi kiwango chetu na sasa hatuko katika kiwango hicho, tumeshinda nina furaha sana, na hilo linatusaidia. Ingawa watu wanatuangalia kwa matokeo tunayoyapata kwangu mimi, hatukuwa na mchezo mzuri. Siwezi kusema kama Man City ya zamani imerudi. Ukiona mchezo, utagundua hilo,” alisema Guardiola na kuongeza:
“Hatuko katika kiwango hicho, dhidi ya Everton tulitoa sare lakini tulicheza vizuri zaidi kuliko leo, ingawa tukipata sare inakuwa tabu na inabidi tupumue kwa matokeo haya, ukweli ni kwamba timu haichezi kama ilivyokuwa miaka iliyopita, hatupo hivyo kabisa.
“Hatupeani pasi, ndiyo maana tunateseka. Tunapoteza mpira kirahisi. Pia hatuna kasi tuliyokuwa nayo zamani. Hatuwezi kukimbia na mpira, tunapaswa kupeana pasi. Wachezaji huwa wanapeana pasi kwa haraka ni kama wanataka kufunga mabao manne ndani ya dakika 20, tunahitaji kutulia na kucheza kwa umakini.”
Wakati Guardiola akisema hayo, kiungo wa timu hiyo, Kevin De Bruyne ambaye kwa sasa ndio kapteni wa timu hiyo, alionekana kukerwa na hali ya mashabiki wao ambao hivi karibuni wamepoteza imani nao na hata namna wanavyoshangilia ni tofauti na vile ilivyotarajiwa.
“Sielewi kwanini,” alisema alipoulizwa kuhusu wasiwasi wa mashabiki. “Naweza kuelewa kwamba hatuko katika kiwango cha juu, lakini wanapaswa kutuunga mkono kwa sababu tunaonyesha juhudi na bado tunaendelea kushinda.”
“Sielewi kinachoendelea kwao, kwa sababu timu inajitahidi kwa kiwango cha juu kabisa, inawezekana wanahitaji kuonyeshe kiwango bora zaidi, sisi kama wachezaji tunaelewa hilo. Tunaelewa zaidi kile tulichofanya katika miaka 10 iliyopita na ugumu wake. Kwa sasa tuko chini ya kiwango hicho tofauti na hapo awali.”
Baada ya mchezo huo wa ligi, Man City itashuka dimbani tena Januari 11 kuumana na Salford City katika mchezo wa raundi ya tatu wa mashindano ya FA na baada ya hapo itarudi kwenye ligi kuumana na Brentford Januari 14.