Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Graeme Souness: Urithi wa Manchester City utafutika

MAN CITY Pict

Muktasari:

  • Souness amekwenda mbali zaidi akisema mataji ambayo City ilitwaa katika kipindi kinachohusishwa na tuhuma hizo yanaweza kuhojiwa, huku akitoa hoja kwamba Liverpool inaweza kupewa baadhi ya mataji hayo.

LONDON, ENGLAND: GWIJI wa Liverpool, Graeme Souness, amesema historia ya mafanikio ya Manchester City inaweza kuingia kwenye doa kubwa endapo klabu hiyo itathibitika kuwa na hatia katika kesi yake ya ukiukaji wa kanuni za Ligi Kuu England.

Souness amekwenda mbali zaidi akisema mataji ambayo City ilitwaa katika kipindi kinachohusishwa na tuhuma hizo yanaweza kuhojiwa, huku akitoa hoja kwamba Liverpool inaweza kupewa baadhi ya mataji hayo.

Manchester City inakabiliwa na tuhuma nyingi za ukiukaji wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa katika taarifa hiyo, City imepatikana na hatia katika makosa 114 kati ya mashtaka 115 yaliyokuwa yakitajwa, ingawa mchakato bado unaelekea kwenye hatua ya rufaa na klabu hiyo imeendelea kusisitiza kuwa haina hatia.

Endapo adhabu itaamuliwa, inaweza kujumuisha faini, kupunguziwa pointi, kushushwa daraja au hata kuvuliwa baadhi ya mataji, kulingana na uamuzi wa mwisho wa kesi.

MAN 01

Akizungumza na Track Radio, Souness amesema urithi wa City utakuwa hatarini ikiwa tuhuma hizo zitathibitishwa.

“Urithi wao utakuwa umeondoka. Ikienda vibaya kwao, wataingia kwenye historia kama waliokuwa wadanganyifu,” amesema.

Souness pia alizungumzia uwezekano wa Liverpool kunufaika endapo mataji ya City yataondolewa.

Kesi hiyo ilianza rasmi mwaka 2023, wakati Ligi Kuu England ilipowasilisha mashtaka dhidi ya City, huku mchakato wa kusikiliza ushahidi ukihitimishwa Desemba 2024.


KLABU HIYO IMEKUWA IKIKANUSHA VIKALI MADAI HAYO.

Mwenyekiti wa City, Khaldoon Al Mubarak, hivi karibuni amesisitiza kuwa msimamo wa klabu hiyo wa kuthibitisha kutokuwa na hatia bado uko imara.

MAN 02

Tuhuma hizo zinahusisha kipindi kirefu cha takribani miaka 14, huku madai mazito yakihusishwa na kipindi cha miaka minane.

City inadaiwa kushindwa kutoa taarifa sahihi za kifedha kwa misimu tisa, kuanzia 2009/10 hadi 2017/18.

Pia ilidaiwa kutotoa taarifa kamili kuhusu malipo ya aliyekuwa kocha wake Roberto Mancini kati ya 2009/10 na 2012/13, pamoja na baadhi ya malipo kwa wachezaji.

Klabu hiyo pia inadaiwa kutoshirikiana kikamilifu na uchunguzi ulioendelea kati ya 2018 na 2023.

Katika kipindi kinachohusishwa na tuhuma hizo, City ilipata mafanikio makubwa, ikitwaa mataji nane ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, FA Cups nne na EFL Cups saba.

Kocha Pep Guardiola amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa anaamini klabu hiyo haina hatia.

Guardiola aliwahi kusema mwaka 2022 kwamba angeondoka kama angegundua viongozi wa klabu walikuwa wamemdanganya kuhusu suala hilo.

MAN 02 (1)

Mwaka uliofuata, amesema hata kama City ingeshushwa hadi League One, asingevunja mkataba wake kwa sababu ya adhabu hiyo.

Uchunguzi dhidi ya City ulianza mwaka 2018 baada ya tovuti ya Ujerumani, Der Spiegel, kuchapisha nyaraka zilizodaiwa kutoka kwenye mkusanyiko wa taarifa wa Football Leaks.

Madai hayo yalihusisha tuhuma kwamba mapato ya udhamini yaliongezwa kwa fedha zilizodaiwa kutoka kwa wamiliki wa klabu badala ya wadhamini waliotajwa.

Pia kulikuwa na madai kuhusu mkataba wa siri uliodaiwa kuhusisha malipo ya Mancini, pamoja na tuhuma nyingine kuhusu usajili wa wachezaji vijana.

Kabla ya hapo, mwaka 2020, City ilifungiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa misimu miwili na kutozwa faini ya pauni milioni 25 baada ya UEFA kuamua kuwa klabu hiyo ilikiuka kanuni za Financial Fair Play.

Hata hivyo, Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) baadaye iliondoa adhabu ya kufungiwa na kupunguza faini hiyo hadi pauni milioni tisa.

Sasa macho yote yanaelekezwa kwenye hatua ya rufaa ya kesi ya Ligi Kuu England, ambayo imekuwa moja ya kesi kubwa na pana zaidi za kifedha katika historia ya soka la England.

Kwa upande wake, Manchester City bado imesisitiza kuwa itaendelea kupigania jina la klabu hiyo na kuthibitisha kutokuwa na hatia katika mashtaka hayo.