Timu zilizowahi kupokwa ubingwa
Muktasari:
- Kwa hukumu hiyo, Man City wako hatarini kukabiliwa na adhabu kadhaa kama kupokwa mataji, kukatwa alama nyingi au kushushwa daraja.
Klabu ya Manchester City ya England ipo hatarini kupoteza jumla ya mataji tisa baada ya kukutwa na hatia ya mashitaka 114 kati ya 115 waliyoshitakiwa nayo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari, klabu hiyo imekutwa na hatia na kamati huru ya uchunguzi juu ya matumizi haramu ya fedha kati ya 2009 hadi 2018.
Kwa hukumu hiyo, Man City wako hatarini kukabiliwa na adhabu kadhaa kama kupokwa mataji, kukatwa alama nyingi au kushushwa daraja.
Haya yote yamejadiliwa sana japo adhabu rasmi haijatangazwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo ametoa taarifa rasmi kama sehemu ya wamiliki akisema watu watulie na wao wanalifuatilia jambo hilo kwa ukaribu sana.
Endapo jambo litakuwa hivyo na Man City wakapokwa mataji yao, yatakuwa marudio ya klabu kadhaa ambayo zimeshawahi kukutana na kadhia hiyo.
JUVENTUS- ITALIA (2004-05 & 2005-06)
Bibi kizee wa Turin, Juventus, walipokwa mataji mawili ya Serie A ya misimu miwili; 2004/05 na 2005/06, kufuatilia kashfa ya upangaji matokeo iliyoitwa Calciopoli.
Kashfa hii ilifichuka mwaka 2006 na kusababisha meneja wa timu, Gianluca Pessotto, kujirusha dirishani kutoka jengo la urefu wa mita 15 la makao makuu ya klabu.
Pessoto ambaye alitoka tu kustaafu kucheza na kupewa nafasi mpya ya meneja, alifanya jaribio hilo la kujiua ili kukwepa aibu iliyokuwa inaenda kuikabili klabu yao.
Japo alinusurika, lakini klabu yake ikakutwa na aibu kubwa. Ilipokwa mataji na kushushwa daraja.
OLYMPIQUE MARSEILLE - UFARANSA (1992/93)
Wababe hawa wa Ufaransa walipokwa ubingwa wa ligi kuu msimu wa 1992/93 baada ya kubainika Rais wa klabu hiyo, Bernard Tapie, aliwahonga wachezaji wa klabu ya Valenciennes ili wasikaze kwenye mchezo wao.
Sio tu kupokwa ubingwa bali pia walishushwa daraja, japo taji la ligi ya mabingwa Ulaya waliloshinda msimu huo waliobaki nalo.
SHANGHAI SHENHUA - CHINA (2003)
Mwaka 2013 klabu ya zamani ya kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, Shanghai Shenhua, ilipokwa ubingwa wa msimu wa 2003 wa ligi kuu ya China ya Jia-A League.
Uchunguzi ulithibitisha meneja wao mkuu, aliratibu upangaji matokeo na kuwahonga waamuzi wakati wa vita kali ya ubingwa.
MAN CITY WAATAPONA KWELI?
Mwenyekiti wa Manchester City, Khaldoon Al Mubarak, ameandika waraka mrefu kwa mashabiki wa klabu hiyo kuwatoa hofu juu ya taarifa juu ya klabu yao.
Nimekuwa sehemu ya klabu hii kwa miaka 18 na kupata bahati ya kusimama nanyi dimbani Etihad, Wembley, na mjini Istanbul.
Klabu hii ina maana kubwa sana kwangu, na mmenionesha na kuniambia kila mara, tena na tena ni kiasi gani Manchester City ina maana kubwa kwenu pia.
HII NDIO SABABU NAWAANDIKIA HAYA.
Kutokana na taarifa za kwenye vyombo vya habari Ijumaa hii, wengi wenu mtakuwa mlitumia muda wenu kujibu maswali na arafa (kumbe) kutoka kwa marafiki, familia na jamaa.
NA MIMI PIA NI VIVYO HIVYO.
Hiki ndicho nilichokisema kwa familia yangu: Mchakato wa Bodi ya Ligi bado una safari ndefu ya kwenda, imani, nia yetu ya kuthibitisha kwamba klabu haina hatia ni thabiti kama ilivyokuwa mwanzo.
Kuna vitu vingi sana ambavyo ningependa niweze kuviweka wazi kwenu ili kuwasaidia kuelewa kwanini tunajiamini katika nafasi zetu.
Lakini kanuni ya kutunza siri za mambo ya kisheria na dhamira ya yetu ya kuheshimu hilo ndio vinasababisha nisiseme kitu kwa sasa.
Hata waraka huu umepitia mikono mingi ya kisheria kuhakilisha hautoki nje ya misingi.
Wakati baadhi ya watu wamekuwa na haraka ya kutoa hitimisho lao, na kumekuwa na kelele nyingi kutuzunguka, hakuna kilichobadilika. Tumezikabili changamoto kwa pamoja hapo kabla na tukavuka salama.
Bado kuna wengine wengi wanaotaka kudogosha harakati za klabu yetu...hatutowapa hiyo nafasi. Tuna nyakati nzuri na za kusisimua (mechi) mbele yetu baada ya mapumziko haya ya kimataifa.
Tutasafiri kwenda Anfield siku chache zijazo, na baadaye kuwakaribisha Paris St Germain kwenye ligi ya mabingwa nyumbani Etihad, hizi ndizo nyakati ambazo hutupa fursa ya kushangilia uimara wa familia ya Manchester City”. Ahsanteni sana, kama ilivyo mara zote, kwa sapoti yenu endelevu.” Khaldoon Al Mubarak.
Barua hii inaonyesha kwa namna gani wamiliki wa Man City bado wana matumaini ya kuipigania klabu yao na kushinda.
Tusubiri tuone itakuwaje.