Ghafla Bruno kawa tatizo Man United!
Muktasari:
- Bruno Fernandes ambaye alionekana kuwa mwokozi wa Man United msimu uliopita kutokana na mabao na asisti zake na kila kitu kilichofanywa na yeye kilionekana kizuri kwa msimu huo.
MANCHESTER, ENGLAND: PAUNI 206 milioni zilizotumika kwenye usajili wa mastaa wapya dirisha hili zimemweka mchezaji bora wa Manchester United kwenye matatizo makubwa.
Bruno Fernandes ambaye alionekana kuwa mwokozi wa Man United msimu uliopita kutokana na mabao na asisti zake na kila kitu kilichofanywa na yeye kilionekana kizuri kwa msimu huo.
Lakini, sasa Fernandes anaonekana kama amepotea kwenye mwonekano mpa wa kikosi cha Man United kutokana na mambo kuonekana kwenda kombo na kutishia usalama wa kocha wake Ruben Amorim.
Man United imesajili mastaa wa maana kabisa kwenye fowadi yake Benjamin Sesko, Matheus Cunha na Bryan Mbeumo. Imefanya uwekezaji mkubwa kwenye safu hiyo ili kuhakikisha mabao yanapatikana. Kuna dalili nzuri baada ya Cunha kuonekana kufanya vizuri akiwa na jezi Namba 10. Mbeumo ana kipaji, ubunifu, wakati Sesko, aliyeigharimu timu hiyo Pauni 73 milioni ana vigezo vyote vya kushinda ubora wa kuwa Namba 9 wa kiwango cha dunia.
Lakini, hakuna ubishi ujio wa mastaa hao kikosi unamfanya nahodha na mchezaji wao bora kabisa, Bruno Fernandes kuonekana kuwa mzigo. Hilo linatokana na Fernandes analazimika kushushwa kucheza kwenye kiungo ya chini, kama ambavyo alipangwa kwenye mechi ya Jumapili iliyopita dhidi ya Fulham, alipocheza pacha na Casemiro, ambaye kwa sasa miguu yake inaoneka kuchoka.
Mbaya zaidi, Casemiro anaonekana kama vile ni kadi nyekundu inayoelekea kutokea kutokana na anavyocheza, tayari miguu imechoka.
Mbadala wa Casemiro, Manuel Ugarte, naye kiwango chake kimeshindwa kumshawishi kocha Amorim ili kumpanga kwenye eneo hilo kumfanya Fernandes awe na uhuru wa kuunganisha timu. Jambo hilo limemfanya staa huyo wa Kireno kuonyesha uchovu mkubwa ndani ya uwanja. Alikosa mkwaju wa penalti, pia alishindwa kumkimbiza Emile Smith Rowe kutoka kwenye eneo la kiungo na kwenda kuifungia Fulham bao la kusawazisha.
Fernandes anaonekana amechoka, lakini kocha Amorim anashindwa kumpumzisha na kumchezesha kila mechi, jambo ambalo limemfanya aonywe asipojitazama, hiyo itamfanya apoteze ajira yake. Amorim anajaribu kumtumia Fernandes kwenye eneo la kiungo ya chini, mahali ambako staa huyo hawezi kutoa mchango unaohitajika kwa timu.
Kwenye mechi ya Fulham kuna nyakati alifikiria sana wakati mpira ulipokuwa kwenye miguu yake hadi wapinzani wanakuja kumpora na kuondoka nao.
Eneo ambalo Bruno amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu anapocheza kwenye Namba 10. Kucheza kwenye Namba 8 si eneo ambalo analimudu kwa ufasaha mkubwa, hasa ukizingatia hana uwezo mkubwa wa kukaba.
Kwenye mechi ya Arsenal, Bruno alipoteza mpira kirahisi wakati alipopigwa kipushi na Bukayo Saka. Kwa kipindi hiki, staa huyo wa Kireno ataonekana tatizo kwenye timu kwa sababu hakabi inavyopaswa huku wachezaji anaopangwa kucheza nao kwenye eneo la kiungo ya kati, uwezo wao wa kukaba umepungua kwa kiwango kikubwa.
Kwa sasa Man United inajilaumu kwa nini haijamsajili Joao Palhinha na ndiyo maana inapiga hesabu za kusajili viungo wenye uwezo mkubwa wa kukaba kama Carlos Baleba.
Pesa iliyotumika kuwasajili Mbeumo, Cunha na Sesko si rahisi kuona wachezaji hao wakiwekwa benchi ili Fernandes acheze kwenye Namba 10. Kumchezesha staa huyo kwenye eneo jingine zaidi ya hilo, litamfanya aonekane tatizo kikosini.