Gary Neville: Kerkez, Van Dijk wameiponza Liverpool
Muktasari:
- Kikosi cha Arne Slot kimepoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu ya EPL msimu huu, huku mabao kutoka kwa Bryan Mbeumo na Harry Maguire, yakiihakikishia Man United ushindi huo, huku bao la wenyeji likifungwa na Cody Gakpo.
Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, amewakosoa mabeki wa Liverpool, Milos Kerkez na Virgil van Dijk, kufuatia kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Man United kwenye Uwanja wa Anfield, jana Jumapili, Oktoba 19, 2025.
Kikosi cha Arne Slot kimepoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu ya EPL msimu huu, huku mabao kutoka kwa Bryan Mbeumo na Harry Maguire, yakiihakikishia Man United ushindi huo, huku bao la wenyeji likifungwa na Cody Gakpo.
Akizungumza na Sky Sports, Neville amesema Liverpool haikucheza vizuri licha ya wachezaji wa timu hiyo ya Anfield kuonyesha juhudi kubwa.
Neville ameeleza kuwa safu ya ulinzi ya Liverpool ilikuwa na wakati mgumu kwenye mechi hiyo, hali ambayo ilipelekea wachezaji wa Man United kuonekana kuwa na makali zaidi waliposhambulia mara kwa mara.
Hata hivyo, gwiji huyo ambaye kwa sasa anafanya kazi za uchambuzi wa soka, amemkosoa beki wa kushoto wa Liverpool, Milos Kerkez, kwa kusema bado anaendelea kuonyesha udhaifu katika uchezaji wake, na kusababisha timu kuhelemewa mara kwa mara.
Amesema beki huyo anacheza kama mtoto wa miaka kumi, hajitambui nini anachokifanya, hali ambayo inaendelea kumpa maswali mengi kuhusu thamani yake ya usajili ambayo ni Pauni 45 milioni.
“Kerkez anacheza kama beki wa kushoto wa miaka 10. Beki wa kushoto mwenye umri wa miaka 10, yuko kila mahali. Sidhani kama ameshaweza kuzoea mfumo wa Liverpool tangu ajiunge kutoka Bournemouth kwa pauni milioni 45," amesema Neville.
Katika hatua nyingine, Neville amemkosoa beki na nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk, kwa kusema hakucheza kwenye kiwango cha ushindani, hivyo naye alichangia kilichoikuta timu hiyo inayonolewa na Arne Slot.
“Van Dijk hakucheza vizuri, ameonyesha uwezo wa hovyo sana, sikutarajia kumuona akiwa kwenye kiwango kama kile, ni wazi udhaifu wake kwenye mechi dhidi ya Man United umechangia Liverpool kupoteza.
"Conor Bradley upande wa kulia alikuwa sawa tu, sidhani kama alikosea chochote, lakini Van Dijk... sijawahi kumuona akiwa na wasiwasi kama ilivyokuwa jana."
"Wakati mwingine mchezaji anapotoka mapumziko ya kimataifa, huwa ndiye anayeshikilia safu ya ulinzi, lakini jana alikuwa tofauti na kiwango chake cha kawaida." amesema Neville
Liverpool pia ilipoteza dhidi ya Galatasaray katika kipindi hiki kigumu kilichoanza Septemba 27, 2025 na hii ni mara ya kwanza tangu mwaka 2014 kwa Reds kupoteza mechi nne mfululizo.
Liverpool itakuwa na mechi mbili ugenini dhidi ya Eintracht Frankfurt kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kisha itapambana na Brentford katika Ligi Kuu ya EPL.