Galatasaray yajipanga kumsajili Lionel Messi
Muktasari:
- Na hilo ndilo linaloifanya Galatasaray kwa sasa kupambana kwa nguvu zote kunasa huduma yake kwa mkopo wa miezi minne tu, akakipige kwenye kikosi chao huko Uturuki wakati ligi ya Marekani itakaposimama mwezi ujao.
ISTANBUL, UTURUKI: NANI ambaye hataki aje kwenye timu yake? Nani huyo asiyemtaka Lionel Messi kwenye timu anayoshabikia? Messi atabaki kuwa Messi bila kujali wakati.
Na hilo ndilo linaloifanya Galatasaray kwa sasa kupambana kwa nguvu zote kunasa huduma yake kwa mkopo wa miezi minne tu, akakipige kwenye kikosi chao huko Uturuki wakati ligi ya Marekani itakaposimama mwezi ujao.
Messi kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Inter Miami, lakini ligi inayoshiriki timu hiyo, MLS msimu wake ulikwisha tangu mwezi uliopita, Oktoba na sasa zinachezwa tu mechi za mtoano, ambazo zitafika mwisho mwezi ujao, Desemba.
Messi na timu yake ilipoteza 2-1 mbele ya Nashville kwenye mechi ya pili kati ya tatu zitakazochezwa kwenye mchujo huo. Staa huyo wa Kiargentina anaweza kuichezea Miami hadi Desemba 6, kama timu hiyo itafanikiwa kufika fainali ya Kombe la MLS.
Baada ya hapo, mshindi huyo wa Kombe la Dunia hatakuwa na mechi yoyote ya kucheza kwenye soka hadi hapo msimu wa MLS utakapoanza upya Machi mwakani, hiyo ina maana atahitaji uhamisho wa mkopo wa muda mfupi ili kuendelea kujiweka fiti.
Na kwa mujibu wa ripoti ya FotoMac, mtandao unaojipambanua wenyewe kuwa ni namba moja kwa michezo huko Uturuki, ukiwa na wafuasi kibao kwenye mitandao ya kijamii, imebainisha Galatasaray imeanza mchakato wa kumvuta Messi akakipige Istanbul.
Na ripoti hiyo imetolewa na mhariri mkuu, Zeki Uzundurukan, ambaye amesema Messi, 38, anafuatiliwa kwa karibu sana na mabosi wa Galatasaray.
Imeelezwa kwamba Messi anaweza kukubali ofa ya mkopo wa miezi minne kwa sababu anataka kujiweka fiti katika kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2026.
Messi kwa sasa anavuta Pauni 15 milioni kwa mwaka huko Miami, huku mshahara wake ukilipwa na Adidas na Apple. Galatasaray ipo tayari kulipa sehemu ya mshahara huo endapo kama atakubali kwenda kujiunga na kikosi chao kwa kipindi hicho cha miezi minne.
Na kinachoelzwa ni kwamba klabu hiyo ipo tayari kulipa mshahara wake wote kwa kipindi chote ambacho Messi atakuwa huko Uturuki.
Galatasaray imeonyesha kuwa na nguvu ya kiuchumi baada ya kumsajili straika Victor Osimhen kwa ada iliyoweka rekodi Uturuki ya Pauni 65 milioni na inamlipa mshahara wa Pauni 250,000 kwa wiki. Ilimsajili pia staa wa zamani wa Bayern Munich, Leroy Sane na kumsainisha dili la kibabe kabisa linaloshuhudiwa akilipwa Pauni 7.6 milioni kwa mwaka.
Kiungo wa zamani wa Manchester City, Barcelona na Borussia Dortmund, Ilkay Gundogan, naye alijiunga na klabu hiyo ya Uturuki kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi na mshahara wake kwa mwaka ni Pauni 4 milioni.
Messi ameendelea kuonyesha umahiri wake wa kufunga mabao tangu alipojiunga na Miami akitokea PSG mwaka 2023. Msimu huu amefunga mabao 40 katika michuano hiyo, akikaribia mara mbili ya mabao yake 23 aliyofunga msimu wa 2024.
Inter Miami haina hofu ya kumpoteza Messi jumla kwasababu imemsainisha mkataba mpya wa miaka mitatu utakaomfanya acheze kwenye timu hiyo hadi anatimiza umri wa miaka 41. Kwa ujumla wake kwenye kikosi hicho cha MLS, amehusika katika mabao 108, akifunga mabao 71 na kuasisti 37.