De Paul: Tuna deni la kulipa kwa Lionel Messi
Muktasari:
- Mapema wiki hii, Messi alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu, ambao utafikia kikomo mwaka 2028, hali ambayo imedhihirisha huenda akastaafu kucheza soka akiwa na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Kiungo wa Inter Miami, Rodrigo De Paul, amekiri kuwa hatua ya Lionel Messi kukubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo, imewapa hamasa wachezaji wengine klabuni hapo ili kufikia malengo waliojiwekea msimu huu.
Mapema wiki hii, Messi alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu, ambao utafikia kikomo mwaka 2028, hali ambayo imedhihirisha huenda akastaafu kucheza soka akiwa na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
De Paul amesema kitendo cha Messi kukubali kuendelea kucheza soka klabuni hapo, ni faraja kwa kila mmoja, ambaye alitamani kumuona nahodha huyo wa kikosi cha Argentina akistaafia soka Inter Miami.
Amesema sio rahisi kwa mchezaji kama Messi kuendelea kubaki kwenye Ligi ya Marekani, ilhali kuna ligi nyingine kubwa duniani ambazo zilitamani kuwa na mchezaji kama yeye, hivyo kwa niaba ya wachezaji wengine wa Inter Miami, De Paul ameahidi kupambana na kumlipa shukurani mwenzao.
“Kujua kwamba tutaendelea kuwa pamoja na Messi kwa miaka mingine, kumetupa motisha ya ziada. Tunapaswa kuendelea kufurahia uwepo wake. Nimefurahi sana kuona kile anachofanya... Haitatokea kucheza na mchezaji kama huyu mwenye kipaji cha ajabu. Ni wajibu wetu sisi kama wachezaji wenzake kupambana na kumlipa shukurani ya kukubali kuendelea kuwa hapa,” amesema De Paul.
Wakati huo huo, Messi amezungumza kupitia tovuti rasmi ya klabu ya Inter Miami baada ya kusaini mkataba huo mpya, akieleza furaha yake kubwa kuendelea kubaki klabuni hapo.
Amesema anasubiri kwa hamu kucheza katika Uwanja mpya wa Miami Freedom Park, unaotarajiwa kufunguliwa rasmi mwaka 2026.
“Nimefurahi sana kubaki hapa na kuendelea na klabu hii, mbali na kuwa ndoto zangu kuendelea kucheza katika Ligi ya Marekani, ni uhalisia sahihi kwangu na wala sijabahatisha kufanya uamuzi huu.
"Dhamira yangu ni kupambana na kuendelea kushinda mataji nikiwa hapa, suala lingine ni kucheza katika Uwanja mpya Miami Freedom Park. Tangu nilipowasili Miami, nimekuwa na furaha kubwa, kwa hivyo nina furaha kuendelea kubaki hapa,” amesema Messi.
“Sote tumejaa hamasa kusubiri wakati ambao tutacheza kwenye Uwanja wa Miami Freedom Park. Ni Shauku ya kila mmoja, lakini kwangu niaamini ni zaidi.” amesema Messi
Messi alijiunga na Inter Miami mwaka 2023 baada ya kumaliza mkataba wake na Paris Saint-Germain (PSG). Msimu uliopita aliisaidia Inter Miami kutwaa Kombe la Ligi (Leagues Cup) na MLS Supporters’ Shield, huku akiendelea kuwa mhimili muhimu wa timu hiyo ya mji wa Florida.