Fury, Joshua mgawo Sh510 bilioni... Pacquiao ndani
Muktasari:
- Pambano hilo litakuwa lenye malipo makubwa zaidi katika historia ya ndondi za kulipwa za Uingereza, huku kila bondia akitarajiwa kuondoka na pauni75 milioni (Sh255 bilioni), bila mmoja kupewa mgawo mkubwa kuliko mwenzake.
CARDIFF, Wales; MABONDIA nyota wa uzito wa juu, Tyson Fury na Anthony Joshua, wanatarajiwa kugawana pauni 150 milioni (sawa na Sh510 bilioni) katika pambano lao la kihistoria litakalofanyika Desemba 11, kwenye Uwanja wa Principality, Cardiff.
Pambano hilo litakuwa lenye malipo makubwa zaidi katika historia ya ndondi za kulipwa za Uingereza, huku kila bondia akitarajiwa kuondoka na pauni75 milioni (Sh255 bilioni), bila mmoja kupewa mgawo mkubwa kuliko mwenzake.
Fury (38), na Joshua (36), ambao wamekuwa vinara wa ndondi za Uingereza kwa zaidi ya muongo mmoja, hatimaye watakutana ulingoni baada ya kusubiri kwa miaka mingi, tangu walipokubaliana kupigana mara mbili mwaka 2021, wakati wote wakiwa wametwaa mataji ya uzito wa juu.
Hata hivyo, mpango huo wa mapambano mawili ulivunjika baada ya Fury kulazimika kutekeleza mkataba wa kupambana mara ya tatu na Deontay Wilder.
Tangu wakati huo, mambo mengi yamebadilika, huku umri ukianza kuathiri uwezo wa mabondia hao, sambamba na kuibuka kwa bondia Moukraine, Oleksandr Usyk, ambaye amekuwa kikwazo kwao katika uzito wa juu.
Licha ya wote kutokuwa katika kiwango walichokuwa nacho miaka iliyopita, kampuni ya Saudi Arabia, Sela, kwa kushirikiana na jukwaa la utiririshaji la Netflix, imeweka mezani kitita cha pauni150 milioni kwa pambano hilo litakalofanyika Cardiff.
Kwa mujibu wa SunSport, kila mmoja atapata pauni75 milioni, huku kukiwa hakuna bondia atakayepewa nafasi ya kuwa na mgawo mkubwa zaidi wa malipo.
Fedha hizo zinatarajiwa kuvunja rekodi za malipo makubwa zaidi kuwahi kupatikana na kila mmoja katika maisha yao ya ndondi.
Taarifa zinaeleza kuwa Fury na Joshua kwa sasa wanalingana katika rekodi ya malipo makubwa zaidi ya maisha yao, kila mmoja akiwa amewahi kuvuna pauni65 milioni.
Pamoja na hilo, hakuna aliyekuwa na ulazima wa kupigana Desemba hii kwa sababu ya matatizo ya kifedha, kwani wote wana utajiri mkubwa na mali nyingi, kiasi kwamba vizazi vyao vinatarajiwa kunufaika kwa muda mrefu iwapo wataendelea kusimamia vizuri fedha zao.
Joshua angeweza kupata malipo makubwa zaidi kama angekubali matakwa ya Turki Alalshikh na Netflix ya pambano hilo kufanyika Madison Square Garden, New York, Marekani.
Hata hivyo, bondia huyo amesisitiza kuwa pambano hilo lazima lifanyike Uingereza, kwa mujibu wa masharti ya mkataba wake, akisema ndondi za nchini humo ndizo zilizompa kila kitu alichonacho leo.
"Ndondi za Uingereza zimenipa kila kitu, zimebadili maisha yangu. Nilikuwa naelekea njia isiyo sahihi hadi nilipokutana na Sean Murphy na Johnny Oliver katika kituo cha Finchley ABC," alisema Joshua.
Aliongeza: "Baadaye nikaenda Timu ya Uingereza (Team GB) Sheffield, ambako nilikutana na makocha wengi wazuri waliofanya kazi kila siku kwa mapenzi ya mchezo, si kwa ajili ya fedha, kwa sababu hakukuwa na fedha."
Joshua, anayefahamika pia kwa jina la Mpiganaji wa Watford, alisisitiza: "Ni Uingereza au hakuna pambano."
Akizungumzia umuhimu wa pambano hilo kufanyika Uingereza, Hearn aliongeza: "Ni jambo lililochukua zaidi ya miaka 10 kuandaliwa. Uingereza ndiyo kitu muhimu zaidi kwa AJ.
"Tumeleta pambano hili Uingereza na tutalifanya katika moja ya viwanja bora zaidi duniani, huku paa likiwa limefungwa.
"Litakuwa pambano kubwa zaidi katika historia ya ndondi za Uingereza na moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo ambayo nchi hii imewahi kushuhudia."
PACQUIAO NDANI
Bingwa wa zamani wa dunia, Manny Pacquiao (47), anaripotiwa kuwa kwenye mazungumzo ya kupambana na Shakur Stevenson, 29, katika pambano ambalo lingekutanisha vizazi viwili vya mabondia nyota.
Pacquiao hajapigana kitaaluma tangu mwaka 2025, baada ya awali kukaa nje ya ulingo kwa miaka minne, lakini sasa anatajwa kumlenga Stevenson.
Bondia mwingine anayeweza kushiriki ni Filip Hrgovic, ambaye hivi karibuni alimshangaza Moses Itauma. Hrgovic, mwenye mkanda wa IBF katika uzito wa juu, anatajwa kupambana na nyota wa mchezo wa kickboxing, Rico Verhoeven, mjini Cardiff.
Verhoeven, ambaye ni gwiji wa kickboxing, alikosa ushindi dhidi ya Oleksandr Usyk katika pambano lililozua mshangao mwezi Mei.
Aidha, bondia wa Uingereza, Jack Catterall, anafanyiwa maandalizi ya pambano la lazima dhidi ya bingwa wa WBA wa uzito wa welter, Teofimo Lopez.
Catterall anataka pambano hilo liwe sehemu ya mapambano ya utangulizi ya Fury dhidi ya Joshua, lakini Lopez anataka kuunganisha mikanda na kupambana na Ryan Garcia.
Mapambano mengine yanayotajwa ni Joe Cordina dhidi ya Abdullah Mason, pamoja na Richardson Hitchins dhidi ya Keyshawn Davis.
Hata hivyo, mapambano hayo yote bado ni tetesi, huku mapromota na Netflix wakitarajiwa kutoa taarifa rasmi hivi karibuni.